"Siku moja, Aligamishi, tajiri mkopesha pesa, alikuja kwa msimamizi wa mji na kuomba apate nakala ya sheria ya tisa. Alisema kuwa anataka kazi yake ikamilike ndani ya siku mbili. Niliambiwa nikifanikiwa kufanya kazi hiyo kwa siku mbili nitapewa zawadi ya sarafu mbili za shaba."
"Nilifanya kazi kwa bidii lakini sheria ya tisa ilikuwa ndefu sana. Algamishi alipokuja na kukuta kazi yake haijaisha alikasirika sana. Kama ningekuwa mtumwa wake hakika angenipiga. Lakini kwa kujua kuwa msimamizi wa mji asingemruhusu anipige, sikuogopa, nikamwambia "'Aligamishi wewe ni tajiri sana. Niambie jinsi ya kuwa tajiri nami nitafanya kazi yako usiku kucha, asubuhi itakuwa tayari.'
"Akatabasamu na kusema, 'we mjanja sana, basi na iwe hivyo'
"'Usiku kucha nilikesha nikiandika, japo mgongo uliuma na harufu ya utambi iliniumiza kichwa na hadi macho yakawa hayaoni vizuri. Alipofika asubuhi kazi yake ikawa tayari."
"Hapo nikamwambia, 'niambie ulichoniahidi'
"Kijana wangu umefanya sehemu yako kwa ukamili,' aliniambia kwa upole. 'Sasa ngoja nami nitimize sehemu yangu. Nitakwaambia ujuzi huo kwasababu nimezeeka na ulimi wa wazee hupenda kuongea Vijana wanapoomba ushauri kutoka kwa wazee, hupata hekima ya miaka mingi. Lakini mara nyingi vijana hufikiri kuwa hekima ya wazee imepitwa na wakati, hilo linafanya wakose kufaidika.
"Kumbuka hili jambo, jua lililowaka wakati wa baba yangu ndilo hilo hilo litakalokuwa linawaka mjukuu wangu wa mwisho atakapokufa.
"Mawazo ya ujana,' akaendelea kusema, 'ni kama mwanga mkali wa kimondo kinachopita angani kwa kasi. Lakini hekima za wazee ni kama nyota inayoangaza siku zote kiasi kwamba mabaharia huitegemea kuwaongoza.
"Nisikilize kwa makini nitayokueleza na uelewe, vinginevyo kazi yako ya usiku kucha itakuwa ni kazi bure.
"Hapo aliniangalia kwa makini kwa macho yake yaliyokuwa yamefunikwa na makunyanzi, kwa sauti ya chini lakini thabiti, akaniambia.
'''Niliipata njia ya kwenda kwenye utajiri nilipoamua kwamba sehemu ya kumi ya kipato changu ni yangu, na wewe unatakiwa ufanye namna hiyo."
"Hapo akaendelea kuniangalia kwa macho ambayo nilihisi kuchomwa lakini hakuendelea kuongea.
"Ni hilo tu?' nikamuuliza.
"Hilo liliweza kubadilisha mchunga kondoo kuwa mkopesha pesa,' akanijibu.
"Lakini mbona kila ninachopata ni changu mwenyewe?' nikahoji'
"Unajidanganya,' akasema, 'je humlipi mshona nguo? Humlipi mtengeneza makubazi? Haulipii vitu unavyokula? Unaweza kuishi Babiloni bila kutumia pesa? Una nini cha kuonyesha kutokana na kipato chako cha mwezi uliopita? Vipi mwaka uliopita? Unalipa watu wote, kasoro wewe mwenyewe. Usiye na akili! Unafanyia wengine kazi. Ni sawa tu na kuwa mtumwa na kufanya kazi kwa yule anayekupa chakula na mavazi.
"Iwapo ungetunza sehemu ya kumi ya pato lako, ungekuwa na kiasi gani kwa miaka kumi?'
"Hesabu bado zilikuwa zinachaji kichwani mwangu, 'itakuwa sawa na pato langu la mwaka mmoja', nikajibu
"Kwa kiasi fulani upo sahihi' akasema. 'Kila kipande cha dhahabu ulichojilipa ni mtumwa wa kukufanyia kazi. Kila senti unayopata ni mtoto anayetakiwa kukuzalishia. Ili kuwa tajiri, kile unachotunza kinatakiwa kikuzalishie, na watoto wake wakuzalishie pia. Hilo ndilo linaweza kukufanya ufikie matamanio yako ya kuwa na mali.'
"Unaweza dhani nakudanganya na umekesha bure, lakini ninachokupa kina thamani mara elfu ya kazi uliyofanya. Unatakiwa tu kuwa na akili ya kuelewa.'
'''Lazima ujilipe sehemu fulani ya pato lako. Haitakiwi kuwa chini ya sehemu ya kumi ya pato lako hata kama pato lako ni dogo kiasi gani. Lakini inaweza kuwa zaidi ya hapo kulingana na uwezo wako. Lazima ujilipe kwanza na panga matumizi yako vizuri, usinunue nguo na viatu kwa pesa nyingi hadi ukakosa pesa ya kutoa misaada na sadaka.
"Utajiri ni kama mti, unakua kutoka kwenye mbegu ndogo sana. Pesa kidogo unayoanza kutunza ndiyo mbegu ya mti wa utajiri wako. Unavyopanda mapema ndivyo na mti utakua mapema. Na kadri unavyotunza mti wako kwa kuumwagilia kwa kutunza pesa ndivyo utakavyokaa na kufurahia kivuli chake mapema,'
"Baada ya kusema hayo, alichukua mabamba yake na kuondoka."
"Nilifikiria kwa makini kile alichokuwa ameniambia na nikaona kinapatana na akili, nikaazimia kukifanyia kazi. Kila mara nilipolipwa, nilichukua sehemu ya kumi ya pato na kuitunza. Jambo la ajabu ni kwamba sikupata shida yoyote ya mahitaji yangu. Tofauti ilikuwa ndogo sana na baadaye nikazoea.
Akiba yangu ilipoanza kukua nikaanza kupata kishawishi cha kuitumia. Nilitamani kununua vitu vizuri vilivyoletwa na meli na ngamia kutoka kwa wafoenike lakini nikajizuia'
"Baada ya miezi 12 toka Algamish aondoke, akarudi tena. Akaniuliza 'kijana, ulifanikiwa kujilipa sehemu ya kumi ya pato lako kwa mwaka uliopita?'
"Ndiyo mkuu, niliweza," nilijibu kwa kujidai.
'''vema sana,' akajibu akiwa kafurahi, 'umefanyia nini?'
'''Nimempatia Azmur, mfyatua matofali. Aliniambia atafanya safari kwenda nchi za mbali na akifika Tiro ataninunulia vito adimu kutoka kwa wafoenike. Akirudi tutauza kwa bei kubwa na kugawana faida,'
'''Kila mpumbavu anatakiwa kujifunza,' alifoka Algamish, 'kwanini umemuamini mfyatua matofali kwa jambo linalohusu vito? Unaweza kwenda kwa muoka mikate kuuliza kuhusu mambo ya nyota? Hapana! Utaenda kwa mnajimu iwapo una akili. Akiba yako imeshapotea, umeng'oa mti wako wa utajiri. Lakini unaweza panda upya. Jaribu tena na wakati mwingine ukitaka habari za vito nenda kwa sonara. Ukitaka kujua kuhusu kondoo, nenda kwa mfuga kondoo.
Ushauri mara nyingi ni kitu ambacho hutolewa bure lakini kuwa makini na hakikisha unachukua ule unaofaa tu. Anayechukua ushauri kuhusu akiba yake kutoka kwa mtu ambaye hana uzoefu ataipoteza kwanza ndipo atajua kuwa haufanyi kazi'. Baada ya kusema hayo akaondoka.