Kitambulisho cha taifa ni nyaraka muhimu inayokuthibitisha na kukutangaza kama raia wa nchi husika kwa mamlaka zote zilizoko katika eneo la Tanzania. Msingi wa kutolewa kitambulisho cha Taifa ni cheti chako cha kuzaliwa ambacho, kwa hakika ni tangazo linaloelezea kuwa tarehe na mwezi katika mwaka fulani ulizaliwa mahali fulani katika jamhuri hii kwa kuwataja wazazi wako wote wawili.
Pasi ya kusafiria ni nyaraka inayotolewa na serikali kwa kukutambulisha wewe kama raia wa nchi hii pale tu unapohitaji kufanya safari nje ya mipaka ya nchi yetu, pale ambapo hakuna utaratibu wa kikanda uliowekwa kama mbadala. Ili upate pasi ya kusafiria ni lazima uthibitishe kuwa wewe ni raia wa nchi hii kwa kutoa cheti cha kuzaliwa. Hapa ndipo mamlaka ya uhamiaji inapoingia kazini.
Kwamba mamlaka ya uhamiaji imepewa mamlaka ya kuchunguza uhalali wa cheti cha kuzaliwa kwa kuchunguza asili ya wazazi wako kwa kuangalia wazazi wako, babu/bibi zako na hata ukoo wako hadi vizazi vitatu ili kujiridhisha kama unastahili kutambulika kama raia na kwa kuwa unasafiri kutambulishwa huko ugenini kama raia wa Tanzania.
Kwa waliotutangulia usajiri wa mtoto hufanyika mara tu anapozaliwa kuanzia namba ya mtoto kati ya watoto waliozaliwa kwa siku hiyo, wodi aliyozaliwa au kama ni nyumbani, namba ya mkunga aliyemhudumia katika mtaa, hospitali tajwa na mkoa husika. Taarifa zote huingizwa kwenye kanzidata ya taifa ili mamlaka zingine zitakapozihitaji ziweze kurejewa. kwa kawaida huwa hawatoi cheti cha kuzaliwa zaidi ya kopi tu ya taarifa zako. Mtoto anapofikisha miaka 18 anatambulika kama mtu mzima na hivyo ni lazima apewa kitambulisho cha Taifa lake mbali na vitambulisho vingine vya shule, kazi au vilabu mbali mbali.
Kwa Tanzania mamlaka za juu zilikuwa hazitunzi vizuri taarifa za vizazi na vifo kama inavyotakiwa, taarifa za kuzaliwa zilikuwa zinafahamika vyema kwa wazazi wenyewe na wakati mwingine kwenye nyumba za ibada na mashuleni.Kwa sasa serikali inataka kutunza taarifa hizi katika sehemu moja ili iwe rahisi kutumika pale zinapohitajika.
Mkanganyiko unaojitokeza sasa hivi kwenye utoaji wa vitambulisho vya taifa, unatokana na ukweli kwamba tunafanya mambo ukubwani huku serikali ikitegemea taarifa sahihi kutoka wetu kwa kuwa haikuwahi kuzikusanya na kuzitunza vizuri tangu ilipozaliwa Tanzania. Mfumo uliotayarishwa kupokea taarifa hizi unahitaji kuunganishwa na mifumo mingine ili taarifa zote zinazohitajika zipatikane kutoka sehemu moja..Watendaji kwa kiasi kikubwa ni watu wazima ambao mambo haya ya kufanya kazi kimtandao ni kitu kigeni kwao hata kwa vijana wetu wa leo pia.