Umoja wa Walimu Wasio na Ajira Tanzania (NETO) umetangaza kuwa uko tayari kukutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, kwa ajili ya majadiliano kuhusu ajira za walimu nchini. Hata hivyo, NETO imesisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama wa viongozi wake kufuatia vitisho wanavyodai kupokea kupitia simu na jumbe mbalimbali.
Chama ca Walimu Wasio na Ajira (NETO) kimesema kimepokea wito wa Waziri George Simbachawene wa kufanya mazungumzo kuhusu usaili wa walimu uliofanyika kati ya Januari 14 na Februari 24, 2025, lakini kimeomba kuhakikisha kunakuwa na ulinzi wa kutosha kwa washiriki wa mkutano huo.
Katibu Mkuu wa NETO, Daniel Edigar Mkinga, amesema lengo lao ni kushinikiza serikali kutoa ajira kwa walimu wasio na kazi na kufanyia kazi mapendekezo yao. Pia, NETO imeomba mazungumzo hayo yahusishe viongozi wa dini na wawakilishi wa mikoa mbalimbali ili kuhakikisha yanafanyika kwa uwazi na amani.
“Lakini kutokana na vitisho tunavyopokea kwenye simu na jumbe mbalimbali zinazozidi kutupa hofu juu ya usalama wetu, tunaomba kuhakikishiwa ulinzi na usalama wetu katika mkutano huo”, imeelezwa katika barua hiyo.
Mara baada ya mkutano huo, viongozi wa NETO wanatarajia kwenda kuwaeleza walimu wenzao kuhusu maazimio ya mazungumzo hayo, wakibeba matumaini mapya kwa mustakabali wa ajira zao.