Na Jackson Odoyo
WAKATI mjadala wa Mahakama ya Kadhi ukizidi kupamba moto, balozi wa Kenya nchini, Mutinda Mutiso, ameionya serikali ya Tanzania kuwa inapaswa kuwa makini katika suala hilo, akikiri kuwa limeshaanza kuwasumbua kwao.
Nchini Kenya ambako idadi ya Waislamu ni asilimia 10 ya watu wote, Mahakama ya Kadhi imeruhusiwa, lakini inafanya kazi kwenye maeneo yaliyo na Waislamu wengi hasa ukanda wa pwani; Mombasa na visiwa vya Lamu na Malindi.
Akizungumza na Mwananchi jana katika mahojiano maalumu ofisini kwake, Balozi Mutiso alisema suala la Mahakama ya Kadhi linapaswa lifanyiwe kazi kwa kina zaidi kuepuka serikali kuingia kwenye lawama baadaye.
"Ninaunga mkono kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyoitoa hivi karibuni juu ya kuundwa kwa kamati akitaka pande zote mbili (serikali na viongozi wa Kiislamu) ili zikae pamoja na kufikia mwafaka kabla ya Kadhi kuruhusiwa," alisema Mutiso.
"Suala hili ni nyeti sana na lina umuhimu wake katika ngazi ya serikali na kijamii, hivyo haipaswi kukimbiliwa na kugeuzwa la mzahamzaha ni lazima kwanza serikali ikajifunze kutoka nchi nyingine na historia kamili ya mahakama hiyo katika nchi hizo."
Mutiso alifafanua kwa kusema: "Kenya, suala la Mahakama ya Kadhi liko kisheria kwa sababu iko ndani ya katiba ya nchini na iliingizwa katika katiba hiyo tangu enzi za Waingereza, na si serikali ya Kenya."
Alisema sehemu ya pili ya katiba ya Kenya inaeleza mahakama nyingine mbali na zile za kiraia, ikiitaja Mahakama ya Kadhi kuwa mojawapo ya mahakama hizo.
Katika sehemu hiyo, kifungu cha 65 kinaeleza: "Bunge linaweza kuunda mahakama zitakazokuwa chini ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Kijeshi, na mahakama itakayoanzishwa, kwa kuzingatia katiba hii, ina mamlaka na nguvu kulingana na itakavyopewa na sheria yoyote."
Kifungu hicho kinaendelea kusema kuwa, "Mahakama Kuu itakuwa na mamlaka ya kusimamia kesi yoyote ya kijinai au ya madai kabla ya mahakama ya chini yake au Mahakama ya Kijeshi, na inaweza kutoa amri, kutoa hati ya kuitwa mahakamani na kutoa maagizo kwa kadri itakavyoona kuwa sahihi kwa lengo la kuhakikisha kwamba haki inasimamiwa vizuri na mahakama hizo."
Kifunga cha 66 (1) cha katiba ya Kenya ndio kinaunda Mahakama ya Kadhi kikisema: "Kutakuwa na Kadhi Mkuu... wa makadhi wengine wote kama itakavyoelezwa au chini ya Sheria ya Bunge."
Balozi Mutiso alifafanua kuwa, suala hilo la Kadhi halina budi kuangaliwa kwa makini kabla ya kuanzishwa kwa kuwa lina mambo mengi ya kuzingatiwa.
Awali, katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu kuanzishwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki, balozi huyo alitaja mambo mbalimbali yanayopaswa kufanyiwa kazi kabla ya kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.
Alitaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na wafanyabiashara kutowekewa mfumo mzuri wa soko, hususan soko la pamoja.
"Suala la soko la pamoja haliwezi kufanikiwa kabla ya mfumo wa biashara kurekebishwa; mfano," alisema na kuongeza: "Wafanyabiashara kutoka Kenya wakitaka kufungua akaunti hapa ni lazima wawe na kibali cha kufanya kazi pamoja na pasi ya kusafiria, kitu ambacho ni kikwazo."
Mbali na suala hilo, balozi huyo alisema kuwa mfumo wa huduma ya kutoa pesa kwenye ATM sio mzuri kwa sababu ATM zote zinatoa fedha za Kitanzania tu, wakati Kenya kuna mfumo wa dola na shilingi ya Tanzania na Kenya kwa wakati mmoja:"
"Mfumo huu unaotumika Kenya ni mzuri na unasaidia sana kwa sababu wafanyabiashara ni watu wenye matumizi ya haraka, hivyo hayo ni kati ya mambo ambayo yanapaswa kufanyiwa kazi haraka," alisema.
Source: Mwananchi 21 July 2009