Biashara (kuuza na kununua au kubadilishana bidhaa) imedumu duniani tangu enzi za kuumbwa kwa dunia. Kazi hii imekuwa ikifanywa na watu wa kila aina. Hapo awali biashara ilifanyika kwa kubadilishana bidhaa (barter). Mwalimu wa sayansi ya jamii (Anthropology) Prof.
Chapurukha Kusimba kutoka chuo cha Wamarekani (American University) anaeleza mwanzo hafifu wa fedha kama njia ya kurahisisha biashara. (
When – and why – did people first start using money?)
Hata hivyo zama zimebadilika sana na sasa iliuweze kuingia katika kazi hii inayopendwa na wengi ya kuuza na kununua (biashara) unahitaji fedha! Kila kitu katika biashara kinahitaji fedha. Uwe unauza mawe mpaka uwe unauza rockets fedha ni muhimu sana.
Changamoto kubwa inayokabili watu wengi wanaotaka kuanza biashara ni mtaji. Hii ni changamoto kwa kuwa sio wengi wanauwezo wa kupata mitaji (fedha au mashine) kutoka kwa familia zao, marafiki au wenye bahati nasibu. Ni dhahiri kuwa unakubaliana na mimi hasa kwa nchi zinazoendelea kuwa mchango wa serikali kwa wananchi wake hauridhishi sana katika kuwezesha hasa vijana kupata mitaji ya kibiashara na hii inatokana na hali halisi za serikali husika au kukosa Imani kwa wananchi wake au vinginevyo.
Kupitia waraka huu utaweza kuchagua namna ya kupata mtaji wa kuanzisha biashara au kukuza biashara yako
Kujenga tabia ya kuwa wavumilivu na kuweka akiba;
- Jambo hili tulitazame kwa namna ya kipekee na kuzingatia hali halisi ya mtu/watu husika. Wengi wetu hatuna hii tabia kabisa ya kuweka akiba, na hii husababishwa na kukosa kipato endelevu na hali zisizo tabirika (majanga kama magonjwa, nk). Kuweka akiba yako binafsi ndio njia ya kwanza ninayopendekeza kwa kuwa utaanza biahsara yako kwa uhuru sana na bila kuwa na mashaka (stress) kuhusu mauzo au marejesho. Hata hivyo ni muhimu sana kuwa na nidhamu ya pesa kama unataka kujiona mbali kimafanikio katika biashara yako. Naamini kuwa kila mmoja kwa namna yake anapambana kufanya jambo lolote linalokupa kipato halali. Kama nilivosema kuweka akiba (Savings) ni ngumu sana kwa tuliowengi. Akiba kila mtu anaweza kujiwekea kulingana na kipato chake. Fanya yafuatayo ili kuweka akiba; -
- Jifunze kuishi maisha chini ya kiwango wakati ukipambana kufikia kiwango cha juu unachotaka kufika ili kuweza kuweka akiba.
- Epuka matumizi yasiyo ya lazima kwa wakati maalumu. Kulingana na mazingira yako kuna vitu ambavyo havina umuhimu sana kwa wakati maalum, jifunze kuwa mbahili. Nikisema ubahili namaanisha nidhamu ya fedha, sina maana usile, usiende hosipitali ukiumwa (uhai ni kila kitu, tunaweza kufanya yote kwakuwa tunauhai, hivyo zingatia uhai kwanza), usitoe sadaka (kwa Imani yako) au mambo mengine ya msingi sana. Ikiwa kuna matumizi ambayo huwezi kuyapunguza tafuta urahisi mbadala. Kila kitu kina mbadala wake ambao unaweza kuwa rahisi kidogo. Sasa simaanishi kama unakunywa bia uanze kunywa mbege au gongo au mnazi! la hasha! Kama unakunywa/kuvuta jaribu kuacha au kama haiwezekani punguza kadiri uwezavyo (kumbuka nilisema sio jambo rahisi kuweka akiba) na hii ni gharama ili kufikia malengo.
- Weka malengo ya kuweka akiba. Hii husaidia sana katika kuweka akiba, usijekuta unaweka akiba kwa miaka bila kujua ni lini hasa lengo la akiba yako litatimia. Weka akiba kwa mwaka, au miaka miwili au mitatu kutegemea na kiwango cha pesa unachowekeza na unachotaka kufikia.
- Weka taarifa zako sawasawa; Akiba unayoweka isiwe tu ya gizani gizani. Hii itakusaidia pia kujua lengo limefikiwa au la! Pia rekodi zitakupa angalizo ikiwa umezembea na lengo halitafikiwa kwa muda uliotamani kuwekeza.
- Andaa bajeti yako mapema kabla ya kufanya matumizi na kumbuka kutoa akiba kabla ya jambo lolote. Kama unafanya kazi ya kulipwa kwa siku, wiki au mwezi, jambo lako la kwanza ni akiba (siongelei Imani), kisha mengine yafuate. Epuka kwenda manunuzini (shopping) bila bajeti utatumia fedha yote na unaweza kurudi nyumbani na deni.
- Weka fedha zako sehemu salama. Sishauri kuhifadhi fedha ndani hata kama unaishi mwenyewe. Do it at your own risk! Bank mbalimbali zinaruhusu kufungua akaunti za akiba ambazo zinaweza kuwa na makato kidogo sana au wakati mwingine hazina makato kabisa, kazi yako ni kuweka tu fedha zako hadi utimize lengo. Wakati wa kuchagua bank ya kuhifadhia fedha fanya uchunguzi kwa bank nafuu zaidi lakini bank ya kuaminika. Bank hizi pia husaidia kukuwekea malengo kwa kutoruhusu fedha kutolewa hovyo kwenye akaunti za akiba. Hivyo fedha hizo hazitakuwa kimbilio la haraka kwenye shida.
- Fanya mwenyewe! Namaanisha fanya wewe mwenyewe au kama unafamilia ishirikishe malengo yako ya kuweka akiba hii pia itapunguza maswali ya matumizi ya fedha. Ninaposema fanya mwenyewe ni kuwa baadhi ya marafiki wanaweza kukushawishi vibaya wakijua unafedha za akiba mahali. Na mambo mengine yanayokuzuia usiweke akiba jaribu kuyapunguza kama sio kuyaacha kabisa.
- Jiunge kwenye vyama vya wajasiriamali, vikoba au vyama vya ushirika. Vyama hivi kujiwekea uhalali wa uanachama hakikisha chama kimesajiliwa. Kwenye vyama hivi kunamikopo yenye riba kidogo na muda wa marejesho ni wakutosha kulinga na uhitaji wako. Kama hakuna chama chochote karibu mnaweza kujiunga wanachama mkaandaa mwongozo (katiba) ya chama chenu mkafuata utaratibu wa usajili. Napendekeza vyama hivi kwa kuwa mwanachama huweza kukopa mara mbili au tatu ya uwekezaji wake kulingana na katiba ya chama. Pia kuepuka kukopesha mtu fedha ambazo hakuna uhakika kama ataweza kurejesha, mwanachama anatakiwa aanza na mkopo mdogo mara ya kwanza, mara ya pili aongeze kidogo na hatimae kufikia lengo ya mara mbili/tatu ya uwekezaji (huu ni ushauri tu kwa vyama vipya). Kukopa ni njia ya pili ya kulazimishwa kuweka akiba kwa gharama ya riba. Hivyo nashauri pia watu kujiunga ili kuweza kutimiza malengo yao kwa wakati.
- Kukopa kunafaida zifuatazo: -
- Kufikia malengo kwa haraka. Badala ya kudunduliza kidogo kidogo kwa mwaka au miaka miwili ili kufikia lengo Fulani, unaweza kujiunga kwenye vikundi na baada ya miezi sita au saba, utaweza kupewa fedha za malengo ya akiba yako na kuendelea kuweka akiba kidogokidogo kwenye kikundi.
- Fedha huja maramoja hivyo kuweza kufanya jambo lako bila kuungaunga.
- Masharti ni nafuu, dhamana kidogo au hakuna zaidi ya mashahidi
- Unaweza kukopa tena baada ya kulipa mkopo wako na hivyo kuwa jambo endelevu kujiendeleza.
- Wanachama hufahamiana vyema, hivyo ni rahisi kushauriana na kutoa maamuzi ya viwango vya mikopo kulingana na hali bila kubaguana.
- Hasara za mikopo
- Kukopa bila mipango kunaweza kukufilisi na hata kufikishwa mahakamani ikiwa utashindwa kulipa fedha ulizokopa
- Riba kubwa hugeuka mzigo mzito kwa mkopaji. Hivyo kabla ya kukopa zingatia kujua riba ya mkopo, marejesho ya mkopo na muda wa uhai wa mkopo. Taarifa hizi zitakusaidia kuweka bajeti ya mkopo wako.
- Fedha ya mkopo ikitumika nje ya mipango huleta hasara ya fedha za kesho. Kumbuka kukopa ni kutumia leo fedha yako ya kesho.
- Mikopo ya vyama mara nyingi haina bima, hivyo mkopaji awe makini sana anapoingia mkataba wa mikopo ya aina hii.
- Mambo ya kuzingatia kabla ya kukopa fedha
- Kwanini ukope? Andaa malengo yako kwanza kabla kupata mkopo! Ukipata mkopo fanya jambo lilelile ulilofanyia tafiti kibiashara. Usikope fedha za kununua gari, kujenga nyumba (isiyoingiza chochote) au kufanyia sherehe au mambo kama hayo mara nyingi kulipa ni ngumu sana. Kama hujajipanga, USIKOPE!
- Unafahamu utaratibu wa marejesho ya mkopo? Je! Ucheleweshwaji wa marejesho yanamadhara gani? Ni mambo muhimu kuzingatia kwa kuwa unaweza kuchelewa kurejesha mkopo ukajiongezea faini au riba au kushindwa kumaliza mkopo kwa muda uliopangwa, hivyo kila mara kumbuka kukopa fedha unazoweza kulipa. Sio kwa kuwa wanakopesha milioni 10 ukope milioni kumi. Je waweza kurejesha? na mambo mengine kama hayo.
- Sehemu nyingine ambapo unaweza kupata mikopo ni katika bank mbalimbali. Hapa nchini bank mbalimbali zinatoa mikopo kwa wateja wao kwa kuzingatia sheria zilizowekwa na bank husika. Kila bank inamasharti yake kwa wakopaji. Hivyo bank zinatoa mikopo kwa wateja waliotimiza masharti hayo.
- Faida ya kukopa fedha bank
- Taasisi ya kuaminika! Hivyo kwa vigezo/masharti, bank humpima mkopaji kama anauwezo wa kulipa mkopo.
- Bima ya mikopo ipo na hupunguza mzigo kwa familia ikiwa mkopaji amepatwa na janga la ulemavu au kifo.
- Fedha huja mara moja na kuweza kukamilisha jambo maramoja
- Fedha zinaweza kutosha bajeti yako
Hasara za mikopo ya bank
- Riba inaweza kuwa kubwa na inayoweza kubadilika bila taarifa kwa mkopaji kulingana na kupanda au kushuka kwa thamani ya fedha.
- Masharti huweza kuwa magumu kwa wajasiriamali wadogo na inahitaji dhamana kubwa kulingana na kiwango cha mkopo.
Mambo ya kuzingatia kabla ya kukopa (angalia juu sehemu ya vyama vya mikopo)
- Wakopeshaji walioidhinishwa na kusajiliwa na mamlaka husika (serikali)
- Kuna taasisi nyingi zilizosajiliwa kama watoaji wa mikopo kwa wajasiriamali wadogo. Watu/taasisi hizi wa/zinapatikana mikoa yote, mfano wa taasisi hizo ni Platnum credit, tunakopesha Ltd, etc
- Faida za mikopo kutoka kwa taasisi hizi: -
- (soma faida za bank hapo juu)
- Hasara za mikopo kwenye taasisi hizi: -
- Riba ani kubwa na kandamizi kwa baadhi ya taasisi, mkopaji asome vizuri masharti ya mkopo.
- Huhitaji dhamana ya vitu vyenye thamani zaidi ya mkopo
- Hakuna bima ya mikopo (kwa walio wengi)
- Inachagua wakopeshwaji na mikopo huwa ya muda mfupi.
Umesoma namna ya kujipatia mtaji kwa njia za kawaida na halali na natumaini utaweza kuchambua vyema ni sehemu gani hasa inakufaa na kuchukua hatua. Nasisitiza; chukua mkopo kwa uangalifu sana ili ukufaidishe. Kuna sehemu zingine nyingi za kujipatia mitaji kama kilimo, ufugaji, kazi, etc. Andiko langu litakalofuata litahusu kilimo na ufugaji.
Asante kwa kusoma na Mungu akubariki!