Unapolalamika kulea mimba, basi mhurumie Nii Ordatey Lamptey

Unapolalamika kulea mimba, basi mhurumie Nii Ordatey Lamptey

O Diafro

New Member
Joined
Mar 13, 2021
Posts
3
Reaction score
5
image_search_1787506781276.jpg

"Nilipokwenda kuchukua majibu kwa daktari aliniuliuliza ni miaka mingapi tuko pamoja[kwenye ndoa], nikamwambia miaka 21. Kisha akaniambia moja kwa moja: 'watoto siyo wako'. Nilikuwa natetemeka...". Aliongea Lamptey aliyeshindwa kuyazuia machozi mara kwa mara katikati ya kipindi cha Tv, cha "GHOne TV's Cheers Show" jijini Accra wakati akifanya mahojiano na mwanadada Nana Aba Anomah, Juni 2017, wiki mbili tu baada ya hukumu ya kesi kutoka.

-------------------
Kwa mwanaume; utafanya nini endapo ukijua kwamba katika miaka 21 ya ndoa ulikuwa unalea watoto wote ambao si damu yako, ukidhani ni wako?

Fikiria kwamba; utajiri wa jasho lako, ujana wako, imani yako, upendo wako, na hata nguvu yako ya uzazi umevitumia barabara, tena kwa moyo mkunjufu kwa watoto wasio wako.

Fikiria kwamba; ulijinyima, uliwanyima wazazi wako ili tu, uwape malezi mazuri na ya furaha watoto wa mwanaume mwenzio.

Basi kuna kisa cha rafiki yangu mmoja wa zamani[wa shuleni], baada ya miaka kadhaa ya kutotiana machoni, alinitafuta. Tulipiga stori mbili-tatu. Lakini katika stori zetu, akanisimulia kisa cha miaka minne nyuma, cha yeye kulea mimba isiyo yake. Na baada ya mwanamke kujifungua, baba halisi wa mtoto alifahamika.

Ndipo hapa ilinibidi kumkumbusha kisa kingine cha kusikitisha zaidi, cha Nii Ordatey Lamptey - mchezaji wa zamani wa Ghana na vilabu kadha wa kadha Ulaya, Asia, Amerika na Afrika.

Baada ya kumsimulia, nilimwambia kama wewe unalalamika ulilea mimba isiyo yako, je, huyu Nii Lamptey asemaje? Suala la huyu rafiki yangu likanifanya niandike makala yenye huzuni kumuhusu Lamptey ili tupate kujikumbusha. Makala ambayo ni funzo kubwa kwetu wanaume kupitia maisha yake, hususani katika malezi, familia, utafutaji, mahusiano, na maisha ya ndoa.

Basi ni nini kilimfikisha mwanaume huyu katika hatima mbaya ya ndoa namna hii? Bila shaka, malezi na mkuzi, na safari yake ya soka iliyojaa mikosi; ambavyo hakuna budi kuvijua.
---------------

Naam, kizazi[generation] "X" na "Millennials"(1965-1996) wafuatiliaji wa mpira wa miguu, bila shaka ukitaja jina la Nii Ordatey Lamptey, kinachowajia akilini ni kipaji chake, hususani katika kombe la Dunia la vija chini ya umri wa miaka 16 mwaka 1989 nichini Scotland, na kauli ya gwiji wa soka wa Brazil, Edson Arantes de Nascmento - almaarufu kama 'Pele' iliyofuatia baada ya mashindano haya, ya kwamba huyu ndiye 'Pele' mpya ajaye baada ya Lamptey 'kukiwasha' kwelikweli katika mashindano haya.

Ni jina ambalo wengi wanalifahamu kupitia soka lake lililojaa mikosi. Lakini vilevile ni jina ambalo wengi hawalijui katika upande wa maisha yake ya ndoa ambayo nayo yalijaa mikosi na hata kufikia kutaka kumuua miaka ya hivi karibuni.

Ni nani hasa mtu huyu?

Nii Odartey Lamptey alizaliwa Disemba 10, 1974 katika ukanda wa pwani ya Ghana, ndani ya mji wa Tema, mashariki mwa Accra. Na akitumia asilimia kubwa ya maisha yake katika miji miwili ya nchi hiyo - Accra na Kumasi.

Kwa Lamptey, ilikuwa ni neema kwake kuja Duniani; vilevile ilikuwa ni taabu kwake kuwa katika mikono ya wazazi ambao hawakujali mustakabali wake wa baadaye.

Wazazi waliompiga vipigo vizito mara kwa mara katika umri mdogo - kwa kosa dogo au pindi alipotoka kusakata kandanda mtaani, hali iliyomfanya akimbie nyumbani, na mara nyingi usiku alilala nje kwenye vibanda vya biashara ama chini ya uvungu wa magari yaliyoegeshwa ili kukwepa vipigo na hata wazazi wake hawakujali.

Hali hii iliathiri maendeleo yake ya elimu kwa kuacha shule mwanzoni kabisa, na kupelekea ukubwani asijue kusoma wala kuandika, hasa lugha ya kiingereza na ikiwa ni chanzo cha kudhulumiwa katika maisha yake ya soka.

Na hata hivyo, wazazi wake ambao pia walikuwa wamekosa elimu, hawakutilia maanani juu ya elimu yake. Hasa baba yake aliyekuwa mlevi wa pombe wa kupindukia, na ambaye alimpiga mara kwa mara na mkanda wa suruali. Na alipoona amekuwa sugu, alibadili mbinu na kuanza kumchoma kwa sigara mwilini mwake mara kadhaa, na ambapo hata sasa ukubwani yu ngali na makovu ya moto wa sigara.

Kama desturi yao, mama yeke mzazi kama mumewe, hakubaki nyuma kumshushia kipigo. Muhimu kwake alihakikisha anafanya kazi za nyumbani hasa kuchota maji ya matumizi ndipo apate chakula pasipo na kumuhimiza kuhusu masomo yake.

Wazazi hawakuona umuhimu wa elimu kwa mtoto; mtoto naye hakujua umuhimu wa elimu kwake kwa baadaye. Alikata tamaa, akacha shule.

Maisha ya nyumbani yalizidi kuwa machungu hasa baada ya wazazi wake kutalikiana mwaka 1982 akiwa na umri wa miaka 8. Hivyo baba yake aliondoka naye kutoka Accra na kuhamia mji wa Kumasi mtaa wa Aboabo 2, ambako alienda kuishi na mwanamke mwingine - mama wa kambo.

Maisha na mama wa kambo nayo yalikuwa ni changamoto nyingine kwake. Mama ambaye hakupenda kuwa katika ndoa mpya na misukosuko ya mtoto ambaye si wake. Asingeweza. Hivyo Baba yake ili kumkunja, aliendeleza kipigo hali ambayo ilimjengea usugu.

"Ilikuwa ni ndoa mpya, na mimi kuwepo pale ilikuwa ni kero kwake[mama wa kambo]. Mke wake mpya hakutaka usumbufu. Baba aliendelea kunipiga na sikuendelea kulia tena. Hivyo alikuwa ananichoma na sigara aliyokuwa anavuta". Lamptey alinukuliwa na Jonathan Wilson, mwandishi wa gazeti la Indipendent, 2017.

Licha ya misukosuko ya makuzi na malezi aliyokutana nayo yu ngali mdogo, hakuacha kusakata kandanda kila alipopata nafasi. Wakati mwingine baba yake alimfuata kiwanjani na kipigo kilianzia hapohapo. Lakini kwake, Kandanda ilikuwa ni faraja pekee iliyobakiwa nayo.

Wakati akisakata kandanda katika mtaa huu wa Aboabo Na.2, alionwa na mdau mmoja wa soka aliyeitwa Yahayu 'Gbegbee'(marehemu). Ambaye alimchukua kwa ridhaa ya baba yake mzazi aliyeona ni fursa kufurahia penzi na mke mpya bila bughudha za mtoto msumbufu. Yahayu aliondoka na Lamptey na kwenda kuishi naye mtaa mwingine wa Aboabo 1.

Lakini haikuchukua muda mrefu, Yahayu alikuwa anaondoka nchini Ghana kwenda Ivory Coast kutafuta malisho mapya katika soka. Hivyo alimkabidhi Lamptey mikononi mwa rafiki yake - kitwasi na mdau mwingine wa soka la Ghana, Alhaji Njei, ili amuendeleze kisoka na malezi.

Huyu Alhaji Njei ni nani? Basi huwezi kuudharau mchango wake katika uwekezaji wa kandanda la Ghana, hususani kuibua vipaji. Anafahamika kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1970 akimiliki klabu ya kupika vipaji ya Kaloum Stars hapo Kumasi aliyoianzisha mwaka 1979, na wachezaji wengi wakifuliwa hapo.

Anakumbukwa mwishoni mwa miaka ya 1990 kwa kuingia makubaliano na klabu ya Galatasaray ya Uturuki kwa aajili ya kuizalishia angalau wachezaji wawili kila mwaka kutoka Ghana. Pia anafahamika vema kwa kujihusisha na klabu ya Asante Kotoko akiwa mjumbe wa bodi wa klabu hiyo kwa kipindi fulani.

Basi yeye; ndiye hasa aliyekitambulisha Duniani, na kukiendeleza kipaji cha Lamptey baada ya kwenda kumpika vilivyo katika klabu yake ya Kaloum Stars hapo Kumasi. Klabu ambayo ilikuwa na wachezaji wote wa kiislamu, wengi wakitokea katika shule ya kiislamu ya Kamaria iliyopo hapo hapo Kumasi. Basi naye hakuwa na budi ya kubadili dini ili aendane na mazingira.

Alibadili dini na kupewa jina la kiislamu - aliitwa Nasiru. Jambo hili lilizidisha kutofautiana zaidi na baba yake mzazi. Lakini Lamptey alikuwa ameamua hivyo ili kuendeleza kipaji chake cha soka, ambacho ndicho faraja pekee iliyokuwa imebakia kwake. Vilevile aliona yupo katika mikono salama tofauti na nyumbani, na hata tabia yake yake ya kitoto ilianza kutoweka.

Akiwa hapa anajifua katika klabu ya vipaji ya Kaloum Stars, alifahamiana na binti wa kiislamu aliyekuwa anasoma shule ya Kamaria, aliyeitwa Zakiya. Binti huyu wa kiislamu alitokea katika familia ya kifukara, alikuwa rafiki, na mtu wa karibu sana wa Lamptey.

Hisia za kupenda huja bila kujali umri. Na hawa wawili walishibana wangali wadogo katika wakati ambao Lamptey alianza kujitafuta kisoka. Na wakaendelea kukua pamoja kama mfupa na nyama. Na urafiki huu, Njei aliufahamu na kuubariki kama mlezi wa kisoka, kiimani na kimaadili wa Lamptey.

Basi kwa uwezo wake wa kusakata kandanda akiwa na umri wa miaka 14 tu, mwanzoni mwa mwaka 1989, Njei alimpeleka kwa mkopo katika klabu ya Young Conerstone iliyokuwa daraja la kwanza ili akapate uwezo zaidi. Na ndipo hapa, mwaka huohuo jicho la kocha wa timu ya taifa ya vijana ya Ghana, mbrazil Paulo Luiz Campos, likamuona.

Aliitwa katika timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 16 iliyokwenda nchini Scotland kushiriki mashindano ya JVC ya kombe la Dunia la vijana chini ya umri wa miaka 16 yaliyofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 24 Juni, 1989.

Katika michuano hii, Ghana ikiwa kundi A pamoja na mwenyeji Scotland, Bahrain na Cuba. Ilishika nafasi ya tatu na kushindwa kufuzu baada ya kujikusanyia alama 2.

Licha ya kutolewa mapema, lakini sifa kutoka kwa macho ya watazamji zilikuwa juu ya Lamptey. Hata mfalme wa soka Duniani Edson Arantes de Nascmento, almaarufu kama 'Pele', alimsifu mtoto huyu na kudiriki kusema amepata mrithi wake baada ya kumtazama mara mbili katika michuano hii akiwa na umri wa miaka 14 'akikimbiza gozi la ng'ombe' kwa kasi. Kama Pelé angelijua mikosi iliyoizingira safari ya mtoto huyu, basi angeliweka maneno yake kuwa akiba.

Baada ya timu hii ya vijana kurudi Ghana, Lamptey alianza kupata mshawasha wa kwenda kucheza soka Ulaya katiaka umri huu mdogo. Hadithi alizosikia kuhusu kucheza soka Ulaya na sifa alizomwagiwa katika michuano hii ya kombe la Dunia, havikuacha fikra zake huru kwa kuunusa utajiri wa haraka.

Hasa baada ya kuzungumza kwa simu na nohodha wa timu ya taifa ya Nigeria na mchezaji wa klabu ya Anderlecht wakati huo, Stephen Keshi, aliyemuhamasisha kwamba akatafute malisho ya soka Ulaya ili asipoteze kipaji chake kilichoanza kuwashangaza watu.

Chama cha soka cha Ghana(FA) kilikuwa kwenye mkakati wa kuhakikisha timu ya taifa[Black Stars] inaundwa na wachezaji wanaocheza ndani. Walibaini dhamira ya Lamptey ya kutaka kwenda Ulaya kuendeleza kipaji chake mara waliporudi kutoka Scotland. Hivyo waliishikilia 'paspoti' yake ili kumzuia, kwa sababu walitaka kuunda timu kupitia yeye katika mashindano mengine yaliyofuata.

Lakini kunyang'anywa 'paspoti' hakukuzuia ndoto yake. Alipojua kwamba Keshi na wakala wake wapo Nigeria wakijiandaa na safari ya kurudi Ubeligiji, hakufanya ajizi, alimjulisha kwamba anamfuata Nigeria ili ampeleke Ulaya. Alikuwa tayari na posho kibindoni aliyopata toka chama cha soka cha Ghana alipokwenda na timu ya taifa katika kombe la Dunia, Scotland.

Agasti 15, 1989, alikwenda hadi kituo cha mabasi jijini Accra. Alimtafuta dereva wa taxi na kumwambia kwamba hana 'paspoti' wala kibali, ila angependa amsafirishe hadi Lagos Nigeria kwa kuvuka kinyemela mipaka ya nchi tatu; Ghana-Togo, Togo-Benin, Benin-Nigeria. Walielewana kiasi cha malipo ya fedha kwa kazi hii ya hatari hasa kwa Lamptey ambaye hakuwa na 'paspoti'. Ambapo dereva alimwambia atamfanya kama mtoto wake.

Waliondoka Ghana kuelekea Nigeria na Lamptey akiwa ameketi kiti cha nyuma ya dereva. Na kila walipofika mpakani, alijificha kwa kuinama kisha mbele aliinuka tena. Hadi walipofika Lagos Nigeria, ambapo alipokelewa na wakala wa Keshi, ambaye muda huohuo alimjulisha Keshi kwa simu kwamba "kijana yupo hapa", jambo lililomfanya Keshi afurahi hadi Lamptey akimsikia furaha yake kupitia mazungumzo hayo ya simu.

Basi siku ya kuondoka kwenda Ubeligiji, Keshi aliondoka na Lamptey ambaye hakuwa na 'paspoti', hivyo alitengenezewa 'paspoti' feki ya ki-Nigeria na kufanywa kama mtoto wake.

Walipofika Ubeligiji, Lamptey aliishi nyumbani kwa Keshi miezi sita na akimuhudimia kwa kila kitu.

Haikuchukua muda, Keshi iliiomba klabu ya Anderlecht imfanyie majaribio mtoto huyu waliyedhani ni ndugu yake. Lakini baadhi ya watu katika klabu hiyo walikuwa wanaifananisha sura ya mtoto huyu mfupi na mchezaji aitwaye Lamptey waliyemuona akifanya maajabu katika fainali za kombe la Dunia la vijana nchini Scotland.

Klabu hii ilikubali na kumfanyia majaribio na timu ya wakubwa siku ambayo Rais wa klabu hiyo na viongozi wake wengine walikuwepo uwanjani kushuhudia. Alipogusa mpira mara mbili-tatu, kila mtu alithibitisha kwamba mtoto huyu ndiye Lamptey waliyemsikia na kumshuhudia.

Klabu hii kwa haraka ilipagawa na kipaji chake, na hivyo kuanza kufanya mchakato kuhakikisha anacheza kikosi cha kwanza mapema iwezekanavyo.

Ilipofika mwaka 1990 mwishoni wakati anatimiza umri wa miaka 16, kanuni za ligi kuu Ubeligiji zilibadilishwa kwa aajili yake ili kuruhusu wachezaji wa umri wa miaka 16 kucheza ligi. Na mwaka huohuo alisaini kandarasi ya miaka mitano akisimamiwa na Keshi, kabla ya mikataba iliyofuata kusimamiwa na wakala wa kiitaliano, Antonio Caliendo aliyemtapeli akitumia ujinga wake wa kutokujua kusoma na kuandika kiingereza.

Utapeli ambao huenda anglieuepa kama mlezi wake, Alhaji Njei nagelisimamia mikataba yake yote. Lakini kwa bahati mbaya hata yeye hakuagwa na Lamptey pindi alipopata mchecheto wa kwenda Ulaya akitorokea kupitia Nigeria. Na manung'uniko ya Njei kwa kitendo hiki yalikuwa kama laana moja wapo iliyomuandama katika soka lake.

Akicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, misimu yake miwili ya kwanza na klabu ya Anderlecht, alicheza mechi 30 na kutupia nyavuni magoli 9 kabla mambo hayajaanza kuharibika katika safari yake ya soka.

Mikosi ilimuandama katika maisha yake ya kwaida; mikosi ilimuandama katika soka. Yeye mwenyewe alikiri baadaye mwaka 2008 kwamba anaona mambo mawili ndiyo yalisababisha mikosi hii. Kwanza, ni kuondoka bila kuaga na kukata mahusiano na baba yake mlezi, Alhaji Njei, aliyekuwa amewekeza kwake kisoka, na akimlea kimaisha alipomchukua mikononi mwa Yahayu wakati alipochokwa na baba yake mzazi. Kwa Lamptey kwenda kusaini mkataba na klabu ya Anderlecht bila ridhaa ya Njei, lilikuwa jambo lililomuumiza huyu mlezi wake.

Njei aliwekeza kisoka kwa Lamptey, lakini hakupata kitu, badala yake akafaidi Caliendo ambaye hakuwekeza kitu. Ni kanuni ya kiasili tu. Ili ule, ni kawaida kuliwa. Sasa Lamptey alikula vya Njei, lakini hakumpa nafasi Njei kula vya kwake. Alimbania riziki.

Jambo la pili, ni kufunga ndoa na Gloria Appiah mwaka 1994, jambo lililoikasirisha familia yake - wazazi na kaka zake - kwa kuoa mwanamke ambaye hakuwa ridhaa yao, wa kabila la "Fante", nje ya kabila lake la "Ga". Si familia yake tu iliyokasirika kwa hili, pia Njei ambaye licha ya kinyongo alichokuwa nacho juu yake kuhusu maslahi, lakini aliweza kumuonya juu ya Gloria baada ya kuona Lamptey ameanzisha naye mahusiano mara aliporudi kutoka Ulaya.

Njei aliona mchezaji huyo anafanya usaliti kwa dini ya kiislamu iliyomuhifadhi wakati wa dhiki kwa kurejea dini yake ya awali ya ukristo ili amuoe Gloria. Pia aliona ni usaliti kwa Zakiya, rafiki na baadaye mchumba aliyemvumilia wakati wa dhiki na mateso, na waliyeanza pamoja mahusiano zamani wakati wa utoto angali bado yupo mikononi mwake kabla ya kwenda Ulaya.

Lakini waswahili wanasema kipenda roho hula nyama mbichi. Kusema kweli Lamptey alikula nyama mbichi kwa Gloria. Hakusikiliza ya mwadhini wala ya mnadi swala. Na huenda pia, labda kusilimu au kuwa na Zakiya yalikuwa ni maamuzi yaliyosukumwa na akili za kitoto? Hatujui kwa kuwa hakuwahi kusema hili.

Ila ni kwamba Lamptey hamkumchagua Zakiya, badala yake akazama penzini na mwanamitindo, 'sista du' na malaya aliyeficha makucha, Gloria, almaarufu akifahamika Ghana kama 'Glo Glo'.

Kitendo chake cha kufunga ndoa na Gloria rasmi mwaka 1994, ndiyo ulikuwa msumari wa pili na wa mwisho katika jeneza la maelewano yake na Njei.

Punde baada ya kumuoa mwanamke aliyekuja kumpa donda la maisha baadaye, aliuza vyombo vyake vya ndani katika nyumba aliyopanga mjini Kumasi katika mtaa wa Aboabo 1 na kuhamia jijini Accra alikoishi na mkewe katika jumba la kifahari, wakati huu akichezea klabu ya PSV Eindhoven kwa mkopo. Aliuza vyombo vya ndani na kupuuza makubaliano ya Bodi ya klabu ya Asante Kotoko ambayo Njei alikuwa mjumbe wake, iliyoomba kwamba endapo angelitaka kuuza vyombo vyake, basi ingelinunua, lakini hakuwaambia.

Basi ungelimwambia nini kijana aliyeanza kucheza soka nje, tena akiwa miongoni mwa wachezaji wa kwanzakwanza wa Ghana kwenda Ulaya kwamba asitimize ndoto yake kwa kuishi katika nyumba nzuri katika mitaa ya vitwasi ya East Legon jijini Accra akiwa na mwanamke aliyemuona mjanja machoni mwake? Ujana maji ya moto.

Basi Ile miaka mitatu ya kwanza, kuanzia katika soka, mwaka 1990 -1993, ilionekana kuwa nyota yake ndio kwanza ilianza kung'ara, kumbe ndio ulikuwa mwanzo wa kuzima na kutangatanga katika vilabu vingi kwa muda mfupi kama kuku anayetaka kutaga. Katika miaka hiyo mitatu ya kwanza alikuwa mchezaji tegemeo hasa katika timu ya taifa ya vijana ya Ghana akiitwa mara kwa mara kuichezea, na huenda hii pia ni sababu nyingine inayosemwa kuwa ilichangia kumaliza soka lake mapema kuchilia mbali masuala ya mikosi..

Ambapo mwaka 1991 aliitwa katika michuano ya kombe la Dunia la vijana chini ya umri wa miaka 17 iliyofanyikia nchini Italia, na Ghana kuibuka bingwa. Katika michuano hii, Lamptey alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mashindano.

Februari 1993, aliitwa katika michuano ya kombe la Afrika chini ya umri wa miaka 20 iliyofanyikia katika visiwa vya Mauritius na Ghana kuibuka bingwa kwa kuizaba Cameroon magoli 2-0. Alijumuishwa tena katika michuano ya kombe la Dunia chini ya umri wa miaka 21 Machi mwaka huohuo wa 1993 nchini Australia ambapo Ghana ilifika fainali na kupoteza mbele ya Brazil kwa magoli 2-1. Katika michuano hii ya timu za taifa, aling'ara na kuzifunika nyota za wachezaji kama Juan Sebastian Veron, Alessandro del Piero, Josep 'Pep' Guardiola, Samuel Kuffor na wengineo, na kuchukuliwa kama mchezaji bora ajaye kutoka Afrika.

Lakini kuanzia katikati mwa mwaka huohuo wa 1993, nyota iliyoanza kung'aa na kutabiriwa makubwa, ilianza kufifia. Hali iliyofanya wakala wake bwana Caliendo kumpeleka kwa mkopo katika klabu ya PSV Eindhoven ya Uholanzi msimu wa 1993-1994 ambako alicheza mechi 22 na kufunga magoli 10 katika msimu huo, akiwa mfungaji kinara wa klabu hiyo, na watu wakidhani kuwa huenda Lamptey aliyetegemewa ameanza kuonekana tena.
image_search_1787512784424.jpg

Hapa ndipo klabu ya Aston Villa ya Uingereza ilipovutiwa naye na kumsajili. Usajili ambao wakala wake, Antonio Caliendo alitaka fedha zote za "signing-on fee" asilimia 25 ziingie mfukoni mwake kama alivyozoea kumtapeli bila Lamptey kujua. Badala yake kocha wa Aston Villa, Ron Atkinson 'alisanua mchongo' Lamptey. Aliamuru pesa hiyo ya usajili ya mchezaji kuingizwa moja kwa moja katika akunti ya Lamptey, jambo lililomkasirisha bwana Caliendo.

Hata Lamptey baada ya kupewa pesa hizo na Aston Villa, hakuwahi kujua kabla ya kwamba kuna kiasi cha pesa za usajili ambazo alitakiwa kupata. Ni hadi leo, Lamptey huwa anamkumbuka na kumshukuru sana kocha huyu, na kumlaani bwana Caliendo kama tapeli na mmoja wa aliyechangia kuharibu maisha yake ya soka.

Kusema kweli Caliendo alimmiliki Lamptey kama bwana anavyommiliki mtumwa wake. Alimuhamisha hovyo hovyo katika vilabu mbalimbali ili apate pesa sa usajili alizotakiwa kupata Lamptey. Hata haki za matangazo na picha za Lamptey, alinufaika nazo.

Basi akiwa Aston Villa hakuwika kama ilivyotarajiwa baada ya msimu huo wa 1994-1995 kucheza mechi 10 bila kufunga goli. Ligi kuu ya Uingereza ilikuwa kama ubakaji kwa mwili wake mdogo. Alishindwa kumudu maguvu ya ligi hiyo licha ya mbinu na kasi katika akili na miguu yake. Hivyo akamua kumfuata Atkinson aliyehama kutoka Aston Villa na kwenda kufundisha Coventry. Ambapo akiwa Coventry katika msimu wa 1995-1996, alicheza mechi 6 tu, bila goli lolote.

Mwaka 1997 ulionesha dalili mbaya zaidi kwa mchezaji huyu aliyekuwa na umri wa miaka 22 baada ya kuchezea vilabu vinne ndani ya msimu mmoja. Alipotoka Coventry alijiunga na klabu ya Venezia ya Italia akicheza mechi 5 bila goli. Kutoka Italia alipaishwa na Caliendo kupelekwa bara la Amerika Kusini kutimiza ndoto za kuchezea klabu ya gwiji wa soka Duniani, Diego Maradona; klabu ya Boca Juniors ya Argentina, ambako hakuweza kucheza kwa sheria kuibana klabu hiyo kwa kuzidisha wachezaji wa kigeni, hivyo alitolewa kwa mkopo katika klabu ya Unión Santa Fe, pia ya nchini humo akiichezea mechi 6 bila goli.

Alivyochemka alirudi tena barani Ulaya na kujiunga na klabu ya Ankaragücü ya Uturuki akiichezea mechi 10 na kufunga goli moja.

Lakini akiwa bado nchini Argentina katika klabu ya Unión Santa Fe kabla ya kwenda Uturuki, alikumbwa na balaa la kufiwa na mtoto mdogo wa kiume na wa tatu, aliyeitwa Diego.

Mkewe Gloria, na wanaye wawili walimfuata hotelini mjini Buenos Aires alikopanga na kujibanza hapo ili kumuuguza mtoto huyo - jina alilopewa kutokana na Lamptey kumuhusudu sana gwiji wa soka, Diego Maradona. Hivyo muda mwingi alitumia kumuguuza mwanaye na kupunguza kulitumikia soka.

Diego alikaa hospitali miezi miwili na nusu na kufariki kwa kushindwa kupumua kutokana na maradhi ya mapafu. Lamptey alipotaka kuusafirisha mwili wa mwanaye akamzike nchini Ghana, mamlaka za Ghana zilimzuia. Jambo hili lilimuumiza sana.

Aliumia zaidi pindi alipodhani kuwa bado anamilikiwa na klabu ya Anderlecht ya Ubeligiji, baada ya kumpigia simu makamu wa Rais wa klabu hiyo kwamba alitaka kuondoka nchini Argentina na kurudi katika klabu hiyo ili atulie na kuonesha uwezo wake badala ya kuhangaishwa hovyo katika vilabu vingi ndani ya muda mfupi.

Ni kwamba, Lamptey alijua bado anamilikiwa na klabu ya Anderlecht, na kwamba ndiyo iliyokuwa inamtoa kwa mkopo, kumbe wakala wake tapeli, bwana Caliendo yeye ndiye aliyekuwa anammiliki na kumtafutia hovyo vilabu ili aweze kutengeneza fedha kwa jasho la mchezaji huyu akitumia udhaifu wake wa kutojua kusoma na kuandika.

Baada ya makamu wa Rais wa klabu ya Anderlecht kupokea simu ya Lamptey kutoka Argentina, alimjibu kuwa "sisi hatukumiliki, unamilikiwa na Caliendo". Jibu hili lilimuumiza sana Lamptey ambaye tayari muda si mrefu alikuwa amempoteza mwanaye, amepoteza kiwango chake kwa kuhangaishwa, na sasa alijua anamilikiwa na wakala wake tapeli.

Aliamua kuachana na Caliendo, hakutaka kumsikia wala kumuona machoni. Alirudi nchini Ghana nwaka huohuo wa 1997 na kumpumzika soka kwa muda mfupi ili akili ikae sawa. Badala yake Caliendo alimlazimisha asaini mkataba mwingine, lakini alimkatalia.

Huyu Antonio Caliendo; wakala tapeli na mnyonyaji wa jasho la Lamptey akitumia mwanya wake wa kutojua kusoma na kuandika, alimlaghai Lamptey kwa mara ya kwanza alipompa mkataba asaini katika njia ya doti("dotted line") uliomfanya kuwa mtumwa wake kwa kummiliki. Pia alikuwa ni wakala wa wanasoka nguli kama Carlos Dunga wa Brazil na Roberto Baggio wa Italia ambao hakuweza kuwahangaisha wala kuwanyonya kama alivyomfanyia mchezaji huyu kutoka Ghana. Hadi sasa analaaniwa vikali na Lamptey kwa unyonyaji aliomfanyia.

Ukiachana na ya Caliendo, maumivu mengine katika soka yanayomuumiza hadi leo ni kuacha kuitwa timu ya taifa ya Ghana kuanzia mwaka 1996 baada ya Ghana kupoteza katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Afrika Kusini katika michuano ya kombe la Afrika ambapo aliwalaumu wachezaji wenzake kutojituma, jambo ambalo liliwakasirisha sana. Tokea hapo, katika umri wa miaka 21, hakuwahi kutwa tena kuichezea "Black Stars" licha ya kudai kwamba alikuwa na uwezo wa kulichezea taifa lake katika michuano ya kombe la Dunia 2006, hata katika michuano mataifa ya Afrika iliyofanyika Ghana mwaka 2008 wakati akiwa na umri wa miaka 33.

Lamptey ambaye 'haziivi chungu kimoja' na gwiji wa soka wa Ghana, Abed Ayew Pele, na ambaye hajawahi kuweka wazi sababu, huwa haendi uwanjani kutazama mpira pindi timu ya taifa inapocheza, badala yake anajifungia ndani na kutazama katika runinga peke yake kwa sababu ya kujisikia vibaya. Mara nyingine huwa anajifungia ndani na kulia sana kwa mikosi inayomsakama na hili la kutokuitwa timu ya taifa hali alijiona na uwezo wa kuisaidia nchi yake.

Basi baada ya kupumzika kwa muda mfupi nchini Ghana, chini ya wakala mwingine alijiunga na klabu ya União Leiria ya Ureno, katika msimu wa 1998-1999 ambapo alicheza mechi 7 bila goli. Misimu miwili iliyofuata ya 1999-2001, wakala wake wa kijerumani alimpeleka katika klabu ya nchini kwake, ya Greuther Fürth akaichezea mechi 36 na kutupia nyavuni goli 5 ambako alifiwa tena na mtoto wa pili wa kike aliyeitwa Lisa, naye alifariki kwa tatizo lilelile la maradhi ya mapafu.

Alipotoka Ujerumani alitimkia bara la Asia, nchini China. Akiwa China katika msimu wa 2001-2002, aliichezea klabu ya Shadong Luneng mechi 37 na kufunga magoli 7. Msimu wa 2003-2004 alijiunga na klabu ya Al-Nasr Dubai ya falme za kiarabu. Baada ya hapo alirudi Afrika alikostaafia.

Akiwa Afrika alijiunga na klabu ya nchini mwake ya Asante Kotoko katika msimu wa 2005-2006. Kisha katika misimu miwili, 2006-2008 aliitumia katika klabu ya Jomo Cosmos ya Afrika Kusini na kustaafu mwaka huo bila matunda mazuri ya kifedha kutokana na uharamia aliofanyiwa na mawakala waliotumia udhaifu wake wa ukosefu wa elimu.

Baada ya kustaafu, akitumia kiasi kidogo alichokusanya katika safari yake ya soka, mwaka 2008 alianzisha kituo("academy") cha soka cha watoto kinachoitwa "Golden Lion Soccer" kilichopo jijini Accra, akifua vipaji huku akitoa elimu ya mpira ili kuwaepusha watoto hao wasipitie kile alichopitia. Pia anamiliki shule ya kutoa elimu ya kitaaluma inayoitwa "Glow Lamp International School", ambayo nayo ipo jijini Accra. Pia anaishi katika jumba lake la vyumba saba lililopo mtaa wa East Legon hapo Accra.
---------------

Naam. Sasa basi, vitimbi katika ndoa yake na mkewe Gloria vilikolea zaidi kuanzia mwaka 2013, mwaka ambao alianza kufikiria kujiua.

Kabla ya mwaka 2013, Lamptey alipewa taarifa za tabia umalaya wa mkewe. alipomtuhumu, mambo yalianza kwenda mrama na mkewe akianza kugusia suala la kuachana.

Lamptey hakuwa tayari kuachana kwa sababu ya mambo mawili. Kwanza, hakutaka kuvunja familia, kwa kudhani watoto alionao ni damu yake. Pili, hakutaka hata mali chache alizochuma katika 'karia' yake zigawanywe. Alijishusha na akawa tayari kuvumilia huku ukubwani ili waishi pamoja, asijue kwamba mwenzake anampigia mahesabu ili kukamilisha mission yake.

Sasa basi, kuanzia mwaka 2013, Gloria alitengeneza zaidi mazingira ya ugomvi ili lengo la 50/50 litimie. Juhudi za Lamptey kwamba wasuluhishwe hazikufua dafu. Gloria alitaka talaka.

Ili kupata talaka, alianza kwa kudai kiasi cha £26,000, zaidi ya slilingi milioni 85 za kitanzania ili mtoto mkubwa wa kwanza akasome chuo nchini Uingereza. Lamptey alipodai hana uwezo wa fedha hiyo, alimpa sababu nyingine mkewe.

Ikumbukwe kwamba, Lamptey na Gloria walikuwa na watoto watatu kuachana na wale wawili - Diego na Lisa waliofariki kwa matatizo ya mapafu - na haijulikani kama na wao walikuwa wa kwake.

Masikini! Ili kunusuru ndoa yake, na aliodhani ni wanaye wasikose elimu bora kama yeye alivyokosa kabisa, Lamptey alijikamua kifedha na baadaye kumudu kuwapeleka wote wawili katika chuo kizuri nchini Ghana walau pia mkewe aridhike na kupooza mgogoro. Aliwapeleka chuo kikuu cha Ashesi jijini Accra. Na huyu mdogo alisoma shule nzuri ya sekondari.

Bado Gloria alikoleza mgogoro zaidi kwasababu tu, Lamptey alishindwa kutoa ada ya mtoto wa mwanaume mwingine ili akasome Uingereza. "How a devil woman can kill a man from behind!".

Gloria alifungua kesi ya madai ya talaka mahakamani mwaka huohuo wa 2013 ili apate 50/50 ya mali za Lamptey. Na akiongeza jambo jingine jipya ili kuipa uzito kesi yake, kwamba Lamptey alipoteza uwezo("impotent") kitandani.

Kwa tuhuma hizi za kupoteza uwezo kitandani, naye alishauriwa na jamaa zake wa karibu kwamba akachukue vipimo vya DNA ili kujua kama watoto hao ni wake na hasa wakiongezea na tabia ya umalaya ya mkewe.

Hizi tuhuma za umalaya wa mkewe, Lamptey alizijua, ila hili la kwamba huenda watoto siyo wake, lilimshtua sana. Na kwanza hakujua kabisa masuala DNA kutokana na ukosefu wa elimu.

Hivyo, alilichukulia hili kwa uzito mkubwa. Alikutana na mwanasheria wake ili amshauri vema kuhusu hili la DNA, na hasa kwa kuwa kesi ya talaka ya mkewe ilikuwa tayari mahakamani. Mwanasheria wake alimwambia kuwa achukue vipimo hivi kwa siri bila mkewe kujua, na kwa namna ambayo watoto hawawezi kujua lengo lake. Alimshauri kuwa matokeo ya vipimo yanaweza kutumiaka katika hukumu ya kesi.

Ili kupata vipimo vya watoto, na wao wasishitukie mchezo huu, alikwenda chuoni kwao na shuleni alikosoma mdogo, akijifanya kama amekwenda kulipa ada huku akiambatana na daktari. Alikutana nao na kuwaambia kwamba ana maambukizi katika koo lake, hivyo ni vema na wao wakachukuliwa vipimo ili wajue kama wanamaambukizi kama yake ili watibiwe mapema.

Walikubali, na daktari alichukua sampuli ya mate kwa wote watatu, na yeye Lamptey alichukuliwa hospitali. Ambapo kwa wote wanne, alilipia gharama ya kiasi cha fedha za Ghana, GHc2000. Na jambo hili Gloria hakujua.

Daktari alimuahidi kwamba baada ya wiki mbili majibu yatakuwa tayari. Lakini aliongeza tena muda wa kuchukua majibu hadi mwezi mmoja ili yakitoka yawe ya uhakika kwa sababu yatakuwa muhimu kuunganishwa katika maamuzi ya kesi mahakamani.

Alhamdulillah! Siku ya kupata majibu yake ilifika.

"Nilipokwenda kuchukua majibu kwa daktari aliniuliuliza ni miaka mingapi tuko pamoja[kwenye ndoa], nikamwambia miaka 21. Kisha akaniambia moja kwa moja: 'watoto siyo wako'. Nilikuwa natetemeka...". Aliongea Lamptey aliyeshindwa kuyazuia machozi mara kwa mara katikati ya kipindi cha Tv, cha "GHOne TV's Cheers Show" wakati akifanya mahojiano na mwanadada Nana Aba Anomah, Juni 2017, wiki mbili tu baada ya hukumu ya kesi kutoka.

Na baada ya majibu anadai alishindwa kuendesha gari na kumwambia mwanasheria wake amsaidie kwa kuwa alikuwa hajiwezi.

Alifikiria kujiua kwa aliyokuwa anapitia wakati kesi ipo mahakamani. Anasema saizi angekuwa amezikwa na kusahaulika kabisa. Lakini alimshukuru Mungu kumuepusha na jambo hili.

Kwa kuepuka kwake kujiua kwa sababu ya misukosuko ya maisha na dhulma alizopitia, anatukumbusha msemo mmoja wa wenzetu usemao: "If life does not give you all that you want, rejoice that you are alive" - kwa tafsiri isiyo rasmi, kwamba 'kama maisha hayajakupatia vile ulivyotarajia, inatosha kushangilia au kushukuru kuwa u mzima''

Kwa sasa Lamptey amepata mfariji wa kweli wa maisha yake. Amemuoa muigizaji na mwanamitindo waliyeanza mahusiano mwaka 2016, aitwaye Ruweida Yakuba, ambaye amezaa naye watoto watatu hadi sasa, kwa kuwa akiwa katika mahojiano ya kipindi hiki cha TV, mkewe alikuwa na ujauzito wa mtoto mmoja, akitarajiwa kuongeza idadi kwa mapacha wawili na kuwa watatu.
image_search_1787512928470.jpg

Kuna wakati katika mahojiano haya alisema kwa huzuni, "Swali moja ambalo ningependa kupata jibu[kama nikikutana na mke wangu wa zamani Gloria Appiah] ni kwamba: 'nilifanya kosa gani kustahili haya?'

Basi baada ya majibu ya DNA na kujulikana kuwa watoto siyo wake, mwanasheria wake alimuasa kuwa kwa muda ambao wanasubiri maamuzi ya mahakama, aishi hotelini na kumuacha Gloria peke yake nyumbani. Kwani kuwa naye karibu lolote linaweza kutokea na likavuruga uelekeo wa ushindi wa kesi kwa upande wake. Akafafanya kama alivyoagizwa na mwanaseheria wake.

Hatimaye siku iliyosubiriwa kwa muda mrefu ilifika, siku ya hukumu. Ilikuwa Juni 14, 2017, baada ya kesi kuwa mahakamani kwa takribani miaka minne. Hukumu iliyosomwa na Jaji wa mahakama kuu, Cecilia Don-Chebe Agbevey kwa kumpa ushindi Lamptey hasa akizingatia majibu ya vipimo vya DNA.

Mahakama ilimwamuru Gloria kuondoka katika jumba la Lamptey la vyumba saba katika mtaa wa East Legon jijini Accra. Na matarajio ya Gloria kupata mgawo wa 50/50 yakafia hapo.

***

Makala ya kisa hiki cha Nii Ordatey Lamptey inakumbusha na kufunza mambo machache ya muhimu kwa mwanaume.

Kwanza; suala la malezi bora kwa watoto. Malezi bora kwa watoto ni ya muhimu sana, kwani ndiyo humjenga au kumbomoa mtoto hapo baadaye. Kwa Lamptey, kupigwa na kuchomwa na sigara si kwamba vilimuathiri kisaikolojia, kiimani na kimwili, bali pia vilifanya aanze kulala nje na kuacha kabisa shule.

Katika makala hii, Lamptey atanabaisha alivyotapeliwa na wakala wake bwana Caliendo katika mikataba yake ya soka kutokana na kutojua kusoma wala kuandika. Kutokuwa na shule kichwani, hakujua kwamba kuna vipimo vinaweza kupima vinasaba ili kujua ukweli juu ya watoto aliokuwa anawalea.

Pili; makala hii itakumbusha kuwa hata kama mwanaume upo katika ndoa jipende kwanza kwa kijijenga kiuchumi. Kwani kuna wakati ukitengana na mkeo, hata watoto wako wanaweza kuwa upande wa mama yao na wasikusaidie hata kiuchumi, licha ya kwamba umewajenga kimasha kwa upendo na nguvu zako za ujana.

Uwekezaji usiishie katika familia tu, bali pia nje ya familia ili hiyo nje ikufaae baadye pindi likitokea la kutokea. Huku ndiko kujipenda. Lamptey aliipenda sana familia yake kuliko alivyojipenda yeye.

Kwani kwa sasa tunaona mifano ya wanaume wengi Duniani wenye ukwasi, hususani mashuhuri kwa maarufu jinsi wanavyojibakishia akiba ya upendo ili iwafae baadye kwa kuzingatia jinsi sheria za talaka na ndoa zilivyokatili kwa mwanaume katika nchi nyingi linapokuja suala la mgao wa mali.

Tumeona kwa mwanasoka wa klabu ya PSG na Morocco, Ashraf Hakim, tumeona makubaliano ya ndoa ya Cristiano Ronaldo na mkewe Georgina jinsi walivyoamua kucha nafasi ya kujipenda.

Tumeona pia wengine walioshindwa kujipenda kwanza, kama akina Emmanuel Eboue wa Arsenal na Ivory Coast, ambaye almanusura ajiue kama ilivyokuwa kwa Lamptey.

Kuna wanaume wengine wameenda mbali zaidi na kuamua kutoa kabisa, mifano ni mingi.

Si kwa umuhimu sana, kisa hiki cha Nii Ordatey Lamptey, kinafanana sana na kisa cha mwanasoka mstaafu wa Cameroon na Chelsea, Jeremy Njitapu, ambaye naye katika miaka 12 ya ndoa, alipakaziwa watoto wawili mapacha, kumbe ni wa mshikaji wa zamani wa mkewe.
image_search_1787247599643.jpg
 
Back
Top Bottom