Wakuu, leo baada ya kuamka na kutaka kusafisha kinywa nikagundua mswaki wangu ni wa kitambo sana sijaubadilisha, JamiiCheck kuna madhara yoyote naweza kupata kutokana na kutumia mswaki mmoja muda mrefu?
- Tunachokijua
- Mswaki ni kifaa muhimu katika utunzaji wa afya ya kinywa kutokana na kutumika kwenye kusafishia meno, lakini mara nyingi baadhi ya watu wamekuwa si wepesi wa kubadili mswaki hasa unapokuwa umechoka kwa matumizi.
Je, ni baada ya muda gani unabadili mswaki wako? na Unazingatia nini mpaka kufikia kuubadili?
Wataalamu wa afya wanashauri kubadili mswaki angalau kila baada ya miezi mitatu mpaka minne ili kuwezesha ufanisi wa kusafisha meno na kuepuka athari za kutumia miswaki isiyo bora.
Kutokana na matumizi ya mara kwa mara, mara kadhaa kwa siku, ni kawaida kabisa kwa miswaki kuchoka na kupoteza ufanisi wake. Nywele za mswaki hupoteza umbo lake la awali na kuanza kufunguka. Tunapoona kwamba nywele za mswaki zimeanza kuharibika, huo ni wakati sahihi wa kubadilisha mswaki au kichwa cha mswaki wa umeme hata kama hatujafikia muda wa miezi mitatu unaopendekezwa na madaktari wa meno.
Tovuti ya Mayo Clinic inaeleza unapopiga mswaki, unasaidia kuondoa mabaki ya chakula na plaki (plaque) kwenye meno yako. Plaki ni ute mweupe wenye kunata unaoundwa juu ya meno. Ute huu una bakteria ndani yake. Baada ya kula chakula au vitafunwa vyenye sukari, bakteria waliopo kwenye plaki huzalisha asidi zinazoshambulia enamel, yaani gamba gumu la nje linalofunika meno.
Kadiri muda unavyopita, asidi hizo huvunja enamel na kusababisha matundu kwenye meno (cavities). Plaki inapoendelea kubaki kwenye meno, hugeuka kuwa tartar (uchafu mgumu). Uchafu huu unapokuwa mwingi, inakuwa vigumu kusafisha meno vizuri. Pia, tartar inapojaa karibu na fizi husababisha uvimbe na maambukizi yanayosababisha ugonjwa wa fizi.
Mayo Clinic inashauri kubadili mswaki kila baada ya miezi 3 hadi 4, Ikiwa nywele za mswaki zimechoka, zimepinda au zimevunjika, ibadilishe mapema kabla ya muda huo.
Kadhalika tovuti ya Laboratorios KIN inabainisha kuwa wataalamu wa afya ya kinywa wanapendekeza kubadilisha mswaki kila baada ya miezi mitatu ya matumizi, hata kama unaonekana bado uko katika hali nzuri.
Inaelezwa kadiri mswaki unavyotumika, bakteria na vijidudu kutoka ndani ya kinywa hukusanyika kati ya nywele za kichwa cha mswaki. Bakteria hawa wanaweza kukua haraka katika mazingira yenye unyevunyevu, na kurudi tena mdomoni kila mswaki unapotumika ambapo wanaweza kusababisha magonjwa mbalimbali yanayoathiri afya ya fizi, meno, na afya ya mwili kwa ujumla.
Katika chapisho lake Mark Stapleton daktari wa meno anaeleza kuwa kulingana na kituo vya kudhibiti na kuzuia Magonjwa (CDC), unapaswa kubadilisha mswaki wa kawaida kila baada ya miezi mitatu hadi minne. Ukitumia mswaki wako kwa muda mrefu zaidi ya hapo, nywele zake huanza kuchanika na kuchoka, na hivyo kupunguza uwezo wake wa kuondoa uchafu unaojikusanya kwenye meno ambapo huchochea hatari ya meno kuoza na kupata magonjwa ya fizi huongezeka.