Nashukuru Rev. Kishoka kwa kuanzisha thread hii.
Nikianzia kwenye siasa inayofuatwa na CCM. Kwa kweli sidhani kuwa CCM ya sasa inafuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, wala Azimio la Arusha. Vyote viwili vimeshafunikwa na hakuna hata kiongozi mmoja anaeweza/thubutu kuviongelea licha ya kuvitekeleza.
Mapenzi ya waTanzania kwa CCM ni mapenzi ya Plastic. Ni mapenzi yanayotokana na uoga, tamaa ya mali (hasa fedha) na kutokuwepo kwa uimara wa vyama mbadala. Vile vile yanatokana na hisia kuwa CCM ya zamani inaweza kurudi tena. Subira yavuta kheri.
Watanzania wengi bado wanaamini kuwa wapinzani hawana uwezo wa kuongoza nchi. Hawaoni kama wapinzani wako makini katika kujenga hoja zinazoweza kuwapa wananchi imani ya maisha bora endapo wataamua kuwapa heshima ya kuongoza Taifa hili. Uoga walionao waTanzania endapo chama kingine zaidi ya CCM kitapewa madaraka unatokana na hofu inayopandikizwa na wanasiasa ndani na nje ya CCM.
Kama wengine walivyosema hapo juu, kuna wananchi ambao wanafaidika kwa namna moja au nyingine kwa CCM kuwepo madarakani. Kuna mambo mengi ambayo CCM huyaachia kufanyika ambayo wananchi wanaona ni udhaifu wenye manufaa kwao. Mambo kama takrima, ujenzi holela, biashara zisizodhibitiwa n.k. yanachukuliwa kama fursa ya maisha ya nafuu kwa wananchi. Hivyo wengi wao kuunga mkono CCM ili hali hiyo iendelee kudumu, nao waendelee kujinufaisha. Vile vile CCM imekuwa ikilazimisha wafanya biashara wakubwa kujiunga nao ili wafanikiwe katika biashara zao. Wale waliojaribu kushirikiana na wapinzani walipata matatizo katika shughuli zao na hatimaye kulazimika kujiunga na CCM ili mambo yao yaendelee kuwa mazuri.
Upinzani pia unachangia kuipa CCM nguvu za kuendelea kupata ushabiki. Upinzani imara bado haujaonekana nchini. Kuna mambo mengi yanayokwenda vibaya ambayo wapinzani hawajayatumia ipasavyo kujijenga kisiasa au kuonyesha njia mbadala inayoweza kufanya kero hizo kuepukika na kuleta ustawi kwa Taifa.
Mtazamo wangu ni kwamba, CCM inatumia njia nyingi zenye kuteka hisia za waTanzania katika kujiimarisha. Inatakiwa vyama vya upinzani navyo kuelewa mahitaji ya waTanzania, na kujibu maswali mbalimbali yanayowakera waTZ ili nao wapate nguvu ya kuweza kuleta challenge inayohitajika. Waswahili wanasema "Wengi wape? Hata kama wanaopewa si sahihi.
Upinzani unatakiwa kubuni mbinu za kupata wananchama wengi zaidi ili kupata nguvu za kushindana na CCM katika kila chaguzi, na hatimaye kuweza kuongoza nchi. Wananchi wengi wanakerwa sana na kauli za vitisho, kejeli na matusi kutoka kwa wanasiasa (hasa wa upinzani). Hii inaipa CCM uhalali kwa kuonekana kuwa ni wastaarabu kuliko wapinzani, na hivyo kuungwa mkono na wananchi wengi.