Tanzania ni nchi yenye usiri mkubwa mno, na bahati mbaya sana wananchi wengi tuna kasumba ya kushindwa kusoma nyakati. Kuhusu kutokea wakina Sankara, tayari hilo lishafanyika mwaka 2021 sema kwasababu ya mihemko ya kisiasa wengi tulishindwa kulitazama katika mapana yake. Mwendazake alienda, wengine waliumia, wengine walifurahia.
Tatizo lipo sehemu moja tu, katika lugha za kiusalama nchini Tanzania, Raisi ni alama muhimu mno ya ustawi wa nchi. Awe mzuri au awe mbaya, ni lazima dola lifanye kazi ya ziada kumlinda hadi pale anapomaliza muda wake. Tulikubaliana kwamba ni miaka kumi kwa kila Raisi. Huu utaratibu uvunjwe tu kwasababu asilia, lakini kama ni sababu za kisiasa au mkono wa mtu, nchi ni lazima iingie kwenye matatizo. Inaweza isiwe leo au kesho, lakini lazima matokeo myaone tu.
Mzee Nyerere alitengeneza mfumo wa aina yake hapa nchini. Hadi kufika mwaka 1985 alifanyiwa majaribio mengi na watu waliotaka kuwa wakina Sankara, Rawlings na Gaddafi. Mara zote alipona, siyo kwasababu ya kuwa na mfumo wenye nguvu, ila kwasababu wengi ndani ya mfumo walifahamu madhara ambayo yangetokea endapo mtu kama Nyerere angeondolewa kiholela. Hata wale ambao walikuwa hawakubaliana na sera zake walifahamu vizuri madhara yake ukizingatia hali ya siasa za Afrika wakati huo. Dola ilifanya ilihakikisha mzee anakuwa salama, na mambo yalivyoenda kombo walimpa ushauri ang'atuke.
Baada ya kung'atuka ukajengeka utamaduni kwamba Raisi hawezi kugusika. Hivyo tutashika sharubu za watu wote lakini siyo za Raisi. Wengi akiwemo Mzee Nyerere hawakumkubali Mzee Mwinyi, lakini kuheshimu taratibu za nchi na kudumisha amani, ilikuwa ni lazima amalize muda wake akiwa salama. Alitoka Warioba na baraza zima lakini Mwinyi akabaki. Huu utaratibu ulienda hadi kwa Mzee Kikwete, ambaye mbali na kuwa na kashfa kibao za ufisadi, walitolewa kafara wengine lakini yeye dola lilimlinda.
Hata wale wasiomkubali Mzee Kikwete na kuyatambua madhaifu yake, walimlinda kwasababu ya utaratibu uliowekwa nchini, kwamba Raisi hagusiki. Hili wanasiasa, wanausalama na raia tunalifahamu vizuri. Hata Tundu Lissu wakati wa kashfa ya TEGETA ESCROW alisema dhahiri, kwamba Raisi akitolewa madarakani utatokea mtikisiko mkubwa nchini, hivyo tushughulike na hawa watu wa chini yake. Wanausalama wengi waliishia kumkomesha tu kwa kuvujisha taarifa za kinachoendelea Ikulu, lakini waliacha amalize salama.
Utaratibu ulienda vizuri, mpaka pale ulipoharibiwa mwaka 2021. Kuna madhara makubwa kwenye makosa yaliyofanyika mwaka 2021. Mfano mbaya mno umewekwa, A bad precedent, kwamba Raisi anaweza akatolewa madarakani kwa namna yoyote ile bila madhara kutokea. Kama mwendazake ambaye alilindwa kuliko maraisi wote aliondoka na hayajatokea madhara yoyote, nini kitazuia mwingine asitolewe endapo kundi fulani ndani ya chama tawala au taasisi za kiusalama litataka mtawala atoke ?
Watanzania wengi, hasa wale wa kwenye vyombo vya usalama ambako mara zote watu aina ya Sankara na Rawlings hutokea huko wameshakula A Forbidden Fruit, hivyo macho yao ya kutambua mema na mabaya yamefunguka. Aheri wangeendelea kuaminishwa kwamba Raisi hagusiki, na akigusika yanaweza kutokea madhara. Kinyume chake wameoneshwa kwamba hakuna ambaye hagusiki hapa nchini. Siku za mbeleni, wanaweza wasiwe hawa mnaowaita Sukuga-Gang, bali genge jingine kabisa ambalo litazua taharuki kubwa, chama tawala ndivyo kilivyo.
Katika mahojiano na wahaini wa mwaka 1982, walikiri kuogopa madhara ambayo yangetokea kwa serikali yao endapo Mzee Nyerere angekutwa na jambo baya, kuuwawa au kutolewa madarakani. Katika taarifa zao wanasema kwamba Tanzania ingevamiwa na nchi jirani kama Msumbuji, Angola na Uganda ambazo maraisi wake walikuwa ni wafuasi kindakindaki wa Mzee Nyerere. Walikuja na mkakati kwamba pindi wamepindua nchi, basi kuidhibiti Msumbijia wangeanzisha mahusiano na magaidi ya Renamo na kuidhibiti Angola wangeanzisha mahusiano na UNITA. Haya yangetokea Tanzania isingetawalika.
Kule dola la Roma, kuna kipindi walipitia majanga kwa zaidi ya miaka 50, The Third Century Crisis. Kipindi hiki hakuna mfalme ndani ya dola la Rumi aliyefanikiwa kukaa kwenye kiti zaidi ya miaka saba bila kuuwawa au kupinduliwa na wanajeshi wake. Mambo yalianza kimzaha mzaha baada ya wanajeshi na majasusi kumuua mfalme Severus Alexander na kumuweka mtu mwingine. Wanajeshi na majasusi baada ya kuona kwamba wanaweza kumtoa mfalme ambaye alikuwa anachukuliwa kama mungu mtu, huu ndiyo ukawa utamaduni wao mpya kwa miaka zaidi ya hamsini.
Msihangaike na upinzani, chama tawala kimegawanyika kuliko wakati wowote ule. Huku ndiko upinzani utaanzia. Kuna watu wanaviziana na endapo kundi linalotawala leo hii litafanya makosa kidogo tu, basi tunaweza kuongelea mengine. Baada ya mwendazake lilifanyika jaribio kubwa ambalo halikufanikiwa. Huu ni ushahidi tosha kwamba nyumba imegawanyika, ndiyo maana inatumika nguvu kubwa mno kumsifia mtawala wa sasa huku tukimchafua mtawala wa zamani.