SoC02 Uongozi sio umungu mtu

SoC02 Uongozi sio umungu mtu

Stories of Change - 2022 Competition
Joined
Jul 29, 2022
Posts
16
Reaction score
15
Dhana ya uongozi katika nchi nyingi za Afrika,imekuwa ikitafsiriwa na kumaanishwa tofauti na dhana halisi. Uongozi umekuwa ukichukuliwa kama daraja la kujitwalia ukwasi(utajiri),utukufu(umungu Mtu) kwa miaka mingi tangia kipindi cha mkoloni hata baada ya uhuru.

Dhana hii potofu ya uongozi imejitwalia nguzo na misingi iliyothabiti miongoni mwa wanao tawaliwa na watawala wenye;viongozi wengi hawajali maslahi ya waliowachagua,viongozi hawapendi kukosolewa, na hali inaenda mbali zaidi,unakuta watawaliwa wakiendelea kubariki dhana hiyo ya potofu kwa kuwasifu na kuwapigia debe hao viongozi.

CHANZO CHA UMUNGU MTU KATIKA UONGOZI.

Katiba mbovu ni kiini (kitovu) cha umungu mtu kwa viongozi wengi wa afrika. Ukifuatilia katiba nyingi za afrika zinabariki na kuchochea viongozi wengi kuwa miungu watu. Katiba nyingi zinawapa viongozi waliochaguliwa au teuliwa mamlaka na madaraka makubwa, jambo linalochochea umungu mtu kuzaliwa,kukua, na kuenea miongoni mwa viongozi.

Wananchi (watawaliwa) hawawezi achwa kama chanzo kikuu cha umungu mtu. Kwa sababu sisi tunaoongozwa tumekuwa na tumeendelea kuwatukuza na kuwavika viongozi wetu umungu mtu,viongozi nao wameendelea kuenenda mithili ya miungu watu kwa miaka kenda.hawajali kabisa kuhusu sisi bali maslahi yao yatokanayo na jasho letu na damu zetu. Sio aibu wala ajabu kusikia kiongozi mkubwa wan chi anaongoza na kubariki mauuaji ya wanaonenda kinyume nae, na bado wananchi tunakaa kimya kama hatujui kinachoendelea. Kwa mfano nchini Tanzania, watu wamekuwa wakiuwawa kwasababu tu kukinzana na serikali,.lakini wananchi tupo kimya zaidi ya kujinong’ona tu vijiweni na mitaani,lakini hamna hatua zinazochukuliwa. Jaribu kuwakumbuka watu kama daudi mwangosi,Ben Saanane,jwani mwaikusa na wengine wengi walionyang’anywa haki zao za msingi (haki ya kuishi). Watu wanateswa kwa kutumia vyombo vya dola ,lakini hamna hatua zozote za kisheria zinazo chukuliwa dhidi ya waliotenda hayo

NINI KIFANYIKE KUTOKOMEZA UMUNGU MTU KWA VIONGOZI?

Ningependa kutoa rai kwa wananchi (umma),Viongozi na serikali kiujumla kuchukua hatua zifuatazo ili kuhakikishwa umungu mtu unatokomezwa kabisa barani Afrika, (na mahsusi Tanzania ):

Dhana ya uongozi bora ianze kufundishhwa katika Nyanja zote za elimu. Hii kwasababu mitaala mingi ya elimu imekuwa ikilenga kuandaaa wananchi watiifu kuliko kuwapatia dhana kamili ya utawala bora,hivyo basi imechochea wananchi wengi kubariki matendo maovu ya viongozi,na kuogopa kabisa kupinga au kukosoa waziwazi serikali nna viongozi wake. Hivyo basi mitaala

Viongozi (ngazi za juu) waondolewe kinga ya kutoshtakiwa baada ya kutoka katika nyadhifa walizokuwa wakizitumikia. Katiba na sheria nyingi zimekuwa zikizuia viongozi wa juu kuwajibishwa kisheria pale wanapokosea,dhana hii imechochea viongozi wengi kuenenda na kutenda watakavyo kwa kujua kuwa hamna sehemu yoyote watakayoshtakiwa au kubanwa hata baada ya kumaliza mihula ya uhongozi wao. Hivyo lazima wananchi tuungane ili kuhakikisha mabadiliko kadhaa yanafanyika katika sheria na katiba kiujumla,ili kuhakikisha watu wote tunakuwa sawa katika vyombo vya sheria.

Madaraka na mamlaka ya viongozi yapunguzwe kuendana na dhana ya utawala bora. Viongozi wa ngazi za juu wametunukiwa madaraka makubwa;madaraka ya kuteua na kutengua viongozi wengi wa serikalini . jaribu kufikiri, Raisi anapewa madaraka na mamlaka ya kuteua au kutengua nafasi ya mkuu wa mkoa,mkuu wa wilaya, jaji mkuu,viongozi wakuuu wa tume ya uchaguzi n.k, hivyo ieleweke wazi kuwa kitendo cha kiongozi kuwa na mamlaka na madaraka ya kiwqango cha juu kiasi hicho, huchochea zaidi umungu mtu kwa wateuliwa na mteuaji ;wateuliwa hawatadiriki kumkosoa mteuaji kwa kuhofia kupoteza maslahi yao. Hivyo , lazima madaraka na mamlaka ya viongozi ya kuteua yabinywe ili kukomesha umungu mtu.

Watawaliwa(wananchi) lazima tuamke; tuachane na ushabiki wa hovyo wa siasa. Kiufupi,wananchi wengi tumekuwa sehemu na kitovu cha umungu mtu wa viongozi,na tumekuwa tukiwalinda,kuwatetea na kudhihaki wale wote wanao jaribu kukosoa uongozi husika kwa minajiri ya ushabiki wa kisiasa. Jaribu kutembelea kurasa kadhaa za kisiasa na maoni ya wachangiaji utaelewa ninachokisema,lakini pia chukua tathmini ndogo kipindi cha chaguzi mbalimbali zinazofanyika nchini. Unakuta matukio yapo wazi kabisa kuwa kiongozi flani kafuja mali za umma,kapokea na kutoa rushwa,kaharibu haki za binadamu(kaua) na mengineyo, lakini bado unagundua kuwa wananchi wanamshabikia,wanamlinda,na kumpigia debe wakati wa chaguzi mbalimbali. Hivyo basi, kuamka kwetu, ndio usalama na mustakabali mwema wa nchi zetu.

Vilevile, viongozi husika wajifunze kuwajibika. Pale inapoonekana kuwa kiongozi husika ameenenda ndivyo sivyo,jambo la busara ni kuwajibika kwa kujiuzuru. Najua ya kuwa kujiuzuru limekuwa jambo gumu sana kwa viongozi wengi wa Afrika,hata pale inapodhihirika waziwazi kuwa wamefanya madudu. Basi sisi(wananchi) tuna wajibu wa kuwawajibisha viongozi husika kwa kuwalazimisha kujiuzuru kwa njia zote(kupitia maandamano,kuwafungulia mashtaka,na kutowapigia kura nyakati za chaguzi). Kwa kufanya hivyo kutachochea dhana ya umungu mtu kutokomea. Vilevile, natambua kuna baadhi ya viongozi wanaweza wakajiuzuru kwa minajiri ya kuzimisha na kukwamisha kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria,hivyo basi lazima wananchi tuhakikishe viongozi husika hawaishi kujiuzuru tu, bali na hatua zaidi za kisheria zichukulkiwe dhidi yao.

Mwisho , ningependa kutoa rai kwa serikali na wananchi kiujumla; kwa kuhakikisha mabadiliko ya katiba yanafanyika ili kuhakikisha dhana ya utawala bora ina enziwa vyema katika nchi husika. Nimelisema hili mwishoni haimanishi halina uzito,bali lina uzito mkubwa sana, kwasababu katiba ndio mwongozo wa utawala/uongozi,hivyo kama katiba inabariki umungu mtu,basi usitarajie viongozi watakuja kuwa viongozi bora. Vile vile, katiba ikiwa bora katika dhana ya utawala bora,tarajia viongozi wake kuwa bora pia.ikumbukwe ya kuwa katiba ndio hutoa muongozo wa aina gani ya taifa tunalo hitaji kuwa nalo,hivyo lazima turejee na kuifufua rasimu ya katiba ya Jaji Joseph Warioba ili matakwa na mapendekezo ya raia yatekelezwe.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom