SoC02 Uongozi wa Wilaya na namna wanavyofanyiwa Wananchi

SoC02 Uongozi wa Wilaya na namna wanavyofanyiwa Wananchi

Stories of Change - 2022 Competition

Happybirthday

New Member
Joined
Jun 12, 2021
Posts
1
Reaction score
0
Ni kweli jamii inapaswa kujituma katika kuleta maendeleo yao wenyewe, lakini nyuma ya pazia wananchi wanatumikishwa ili kuleta maendeleo.

Ikumbukwe maendeleo na uchumi bora hutokana na wananchi wenyewe lakini sio wananchi kuwa utumwani kwaajili ya uchumi wao wenyewe. Leo kuna baadhi ya mazingira katika Tanzania yetu wananchi wamekua watumwa katika vijiji vyao wengine kulazimika hadi kuhama na kukimbia familia zao yote ni kwaaajili ya kuukimbia utumwa kwenye suala Zima la kujenga uchumi wa nchi.

Swali ni je, lini viongozi wataacha kuwatumikisha wananchi katika kila jambo? Hili ndio kusudio kuu la makala hii. Viongozi kuanzia Watendaji wa vijiji, Kata, Wakurugenzi Wilaya kuna maeneo bado wanawatumikisha wananchi kwaajili ya maendeleo.

Rai yangu ni kwamba, ingefaa zaidi kwa viongozi hawa hususani vijijini kabla ya kufanya hayo maendeleo wanayoyataka ni vema kuhakikisha wananchi wanakua na uelewa vizuri kuhusu mipango hiyo na sio kuwafanya kuwa watumwa kwenye mambo waliyokosa uelewa au kushindwa kuwa ya msingi kabisa.

Masuala kama vile;

1. Wananchi kuchangishwa michango isiyo na msingi
Kuna wakati serikali inatoa fedha kwaajili ya kukamilisha ujenzi wa madarasa na kimsingi serikali huwa inajua gharama ya kitu kinachoenda kujengwa, lakini kwasababu tu shughuli inafanyika kijijini hivyo viongozi kutumia fursa hiyo kuwachangisha pesa zaidi wananchi hadi kiasi cha Tsh. 10,000/= hii ni kwasababu wananchi wanakua hawajaelewa.

2. Suala la walimu kung'ang'ania kufundisha muda wa ziada (maarufu kama TUITION).
Kimsingi wajibu wa mwalimu ni kumfundisha mwanafunzi kwa muda kama ilivyopangwa na wizara ya elimu, inapofika hatua walimu hawafundishi vyema mda wa darasani na wengi wao wanakuja kutaka wanafunzi wasome mda wa Ziada (mda wa likizo) kwa kuwachangisha pesa wananchi kwa lazima kwa sababu ya kuwa mda wa masomo unaisha na wanafunzi kutokumaliza mtaala, na ajabu zaidi walimu hao huendelea kufundisha mtaala wakati wa likizo kitaalamu wakati ilitakiwa wafundishe ziada.


NINI KIFANYIKE.

Kuna mambo kadha wa kadha ambayo yanahitajika kufanyika na serikali kwaajili ya kuwatoa wananchi kutoka utumwani kwenye mambo wasioyajua na kuteseka nayo kwa sababu tu kiongozi au mtumishi wa umma hataki, au hajatekeleza kile kilicho takiwa akifanye katika ofisi yake au kazi yake.

1. Watumishi wa umma kulinda na kuheshimu mipaka ya kazi zao
Hii itakaa vizuri zaidi, mfano mwalimu anapojua wajibu wake ni kumfundisha mwanafunzi kwa kadili mtaala unavyotaka itakua rahisi zaidi kumaliza Mada kwa wakati na kuacha kulazimisha wazazi kuchanga pesa kwaajili ya kuwalipa walimu wanaofundisha mda wa ziada.

2. Watumishi wajue kuwa kazi zao na ofisi zao hazipo kwaajili ya maslahi yao binafsi bali ni kwa umma
Hapa ndipo wananchi wanateseka na kiukweli ndipo viongozi na watumishi wengi wa halmashauri kuanzia kitongoji hunenepesha matumbo yao na kusahau maslahi ya wananchi, watumishi wa umma wanahitajika kutambua thamani yao na kuaminiwa kwao na serikali kufanya kwaajili ya wananchi na sio kutumia ofisi kwa maslahi yao binafsi hii itawqepusha wao kutoka kuwalazimisha wananchi kutoa pesa zisizo na msingi.

3. Wananchi wanatakiwa kufanyiwa na sio kutumikishwa
Kwa maendeleo wananchi wanatakiwa wafanyiwe na viongozi pamoja na watumishi na sio viongozi na watumishi kuwatumikisha wananchi katika majukumu yao au ya serikali kwaujumla. Kuna wakati wananchi wanajitoa kufanya shughuli flani, Mfano. Katika halmashauri ya wilaya ya Ludewa, kata lugarawa, Kijiji cha shaurimoyo Serikali iliamua kujenga kituo cha afya cha kata, licha ya kuwa cha Kata ni wananchi wakijiji cha shaurimoyo wamejitoa kuweza kujenga kituo cha Afya hadi kutoa michango hadi Tsh. 40,000/= kwa kila mwananchi. Kitu ambacho kimsingi kilitakiwa kushukuriwa zaidi na serikali, ila inapofika hatua viongozi na watumishi wa umma wanapoingizia siasa kwenye maendeleo inakua haileti taswira nzuri kwa jamii.

4. Watumishi wa umma kufanya kazi zao kwa weledi na maarifa kama walivyotakiwa kufanya
Hii inakua nzuri zaidi kwa maana sahizi nafasi ya kutumikia umma inageuzwa kuwa biashara na sio utumishi tena kama kazi yenyewe inavyotaka, mtu akipata nafasi anageuza kuwa ni sehemu ya kujipatia kipato kiholela kutoka kwa wananchi, hapa viongozi wengi ndio hufeli kwenye suala Zima la kuleta maendeleo kwa jamii hivyo hushindwa hata kusimamia miradi ya serikali kwa ufanisi hadi kufikia hatua ya kutaka pesa kutoka kwenye mifuko ya wananchi tena pasi kuzingatia matumizi bora ya fadha za umma zilizotolewa na serikali na kuwachangisha pesa wananchi wakati pesa zilizotolewa na serikali zinatosha kabisa kuendesha mradi.


Madhara ya uongozi mbaya

Wananchi kuishi kama watumwa,
hiki ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo. Inapofika hatua watumishi wa umma wanakua simba kwa wananchi wao ni ishara tosha kwamba eneo hilo haliwezi kuwa na maendeleo. Maendeleo yawe ya mtu binafsi au ya jamii yote kwa yote utayari wa wananchi huwa ni ishara ya mwanzo ya kupata maendeleo wayatakayo na sio kulazimishwa.

Miradi kujengwa chini ya kiwango kama ilivyotarajiwa na serikali. Watumishi wengi wanatumia pesa za serikali zinazotolewa kwa ajili ya kukamilisha miradi kwa maslahi yao wenyewe na kutegemea miradi hiyo kukamilishwa kwa michango ya wananchi, hivyo pesa kutokutosha na mwishowe miradi kuwa mibovu. Hivyo badala ya watumishi kuleta maendeleo kwa jamii wanazozitumikia wanageuka kuwa sababu ya ubovu wa miradi inayopangwa na serikali katika maeneo hayo.

Wananchi kutokua na Imani na viongozi wao, hii ni moja ya athari kubwa zaidi ambayo inapoteza kabisa dira ya serikali kwenye kuyafikia maendeleo na uchumi kukua, kutokana na uongozi mbovu wa watumishi wa umma kwa raia wao unapelekea panda hizi mbili kutokuaminiana kabisa kwenye miradi inayotaka kufanyika na hatimaye serikali kuonekana kama haifanyi kazi na kushindwa kutekeleza matakwa ya katiba Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Wananchi kutoheshimu na kudharau jitihada za serikali, hii inasababishwa na viongozi wenyewe kufanya mambo kinyume na ilivyotakiwa au kufanya vibaya kwa maslahi yao binafsi pamoja na kufanya chini ya kiwango kama kama ilivyotarajiwa. Na inapofika hatua kwamba wananchi hawaheshimu tena jitihada za serikali ndio wakati huu uchumi wa nchi hudorola na maendeleo kushuka kwa ujumla.

Hitimisho.
Kimsingi, maendeleo ya wananchi ndio maendeleo ya taifa kwa ujumla, hivyo maendeleo ya taifa yasiyojali maendeleo ya wananchi ni sawa na bure, uchumi wa nchi kukua pasipo furaha mioyoni mwa wananchi na yenyewe ni sawa na bure.


Makala hii Imeandaliwa na:
ESSAU EDWARD YALUMA
Email Address: yalumaessau1@gmail.com
Phone no. +255 765 508 581
 
Upvote 0
Back
Top Bottom