Uchaguzi Serikali za Mitaa ngumi mkononi
[Source Tanzania Daima]
na Mwandishi Wetu
UCHAGUZI wa Serikali za Mitaa, uliofanyika jana, uliingia dosari kutokana na kutawaliwa na vurugu katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika eneo la Kigamboni Tuamoyo, jijini Dar es Salaam baadhi ya wapiga kura walifanya vurugu baada ya kutoona majina yao kwenye ordha iliyokuwa imebandikwa ukutani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wapiga kura hao walilalamikia utaratibu uliowekwa kituoni hapo ambao kwa kiasi kikubwa umewasababishia usumbufu.
"Kwenye ukuta majina yameandikwa bila kufuata mpangilio, pia kuna watu wengi, kila mmoja anataka kuangalia jina lake hali inayoleta usumbufu," alisikika mmoja wa wananchi hao akilalamika.
Hali hiyo ilisababisha wananchi kuondoka vituoni hapo bila kupiga kura ingawa walijiandikisha awali kwa ajili ya zoezi hilo.
Aidha, katika kituo hicho mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Nasoro Haji Mohamed, mkazi wa Mjimwema alitaka kupiga kura, lakini alizuiwa na askari waliokuwapo.
Kitendo hicho cha kumzuia kupiga kura, kilisababisha mabishano na hatimaye mwananchi huyo alijikuta akipigwa na askari waliokuwapo kituoni hapo.
Hata hivyo, mpaka unafika muda wa mwisho wa kupiga kura jana, wananchi wengi walikuwa bado hawajapiga kura, huku baadhi ya mawakala wakishinikiza kufunga zoezi hilo na wengine wakipinga.
Hali hiyo iliibua mzozo baina ya mawakala hao, hali iliyosababisha baadhi yao kushikana mashati mpaka polisi walipoingilia kati.
Katika kituo cha Shule ya Msingi Kiwalani, wananchi walilalamikia utaratibu mbovu wa mpangilio wa majina ambao haukufuata alfabeti, hali ambayo imeshabisha usumbufu mkubwa kwa wapiga kura kuona majina yao.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wengi walitumia muda mwingi kutafuta majina yao huku wengine wakiondoka bila kupiga kura.
"Kwa kweli ni usumbufu, binafsi nilikwenda kwa lengo la kupiga kura ili baadaye niende kazini, lakini mpangilio mbovu wa majina umenisababishia usumbufu, hivyo nimeamua kuondoka bila kuona jina langu wala kupiga kura," alisema mmoja wa wapiga kura katika eneo hilo.
Katika Mtaa wa Karakata, Kata ya Kipawa, wananchi walilazimika kupiga kura bila usiri, hali ambayo ilichangia baadhi ya wapiga kura kususia zoezi hilo.
Tanzania Daima ilishuhudia majina ya wagombea yakiwa yameandikwa ubaoni kwa chaki, huku kila chama kikiwa kimeyatenga majina yake pembeni.
Hali hiyo ilisababisha usumbufu kwa wapiga kura, kwani kila aliyekuwa akipiga kura, wagombea pamoja na mawakala walikuwa wanamjua amemchagua mgombea wa chama gani, kwani walikuwa wakionekana wakitazama upande gani wa majina ya wagombea na chama husika.
"Kwa jinsi hii mimi siwezi kupiga kura, kwani kila mgombea atajua nimempigia nani kwa sababu wapo madirishani wanachungulia, wakiniona nimekaza macho kuangalia upande wa kulia au kushoto watajua ni chama kipi nimekipigia kura. Hii ni kujenga uadui sasa," alisema Mzee Nassor wakati akiondoka kwenye kituo cha kupigia kura.
Kutokana na zoezi hilo kuwa la wazi, wapiga kura wa kituo hicho wameilalamikia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushindwa kuandaa karatasi zenye picha za wagombea, ili iwe siri wakati wa kuwachagua.
Katika eneo la Kimara, hali ilikuwa tofauti kwani licha ya wapiga kura kujitokeza kwa wingi vituoni, karatasi za kupigia kura za wajumbe zilikuwa chache na kusababisha zoezi hilo kuendeshwa kwa mizengwe.
Mbali na dosari hiyo, Tanzania Daima ilishuhudia watu wengi wakiondoka bila kupiga kura kutokana na usumbufu wa kutafuta majina kwa muda mrefu bila kuyaona kwa hayakuwekwa kwa mpangilio wa kufuata alfabeti.
Mmoja wa wapiga kura hao ambaye alikuwa apige kwenye kituo cha Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Kimara alisikika akisema ameondoka baada ya kushindwa kuona jina lake.
Wakala wa CUF, Said Mbegu alisema wakazi wengi wa eneo la Kimara, wameitikia wito, lakini tatizo ni msongamano wa kutafuta majina na upungufu wa karatasi za kupigia kura.
"Tume irekebishe utaratibu huu wa kutafuta majina kwa kuwa watu wengi wanasusia na wengine hawajui kusoma," alisema Mbegu.
Katika Kituo cha Zahanati, Kimara Mwisho, kulikuwa na mwitikio mkubwa wa wapiga kura, ingawa kulikuwa na tatizo la watu wasiojua kusoma na kuandika ambao walichelewesha wengine kupiga kura.
Hata hivyo, tatizo la kukosekana kwa karatasi za kupigia kura kwa wajumbe, lilionekana kuwa kubwa na kuleta mzozo, huku baadhi ya mawakala wa vyama wakitishia kugomea matokeo hayo.
Katika Jimbo la Kawe, Wilaya ya Kinondoni, hali nayo haikuwa shwari kwani katika vituo vya Kawe Ukwamani, vurugu zilitokea baada ya baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa kuanza kupiga kampeni katika vituo vya kupigia kura.
Hatua hiyo ilisababisha Mkuu wa Kituo cha Polisi Kawe kufika katika eneo hilo akiwa na askari na kusimamia usalama.
Hadi majira ya saa 7:30 mchana, idadi ya wapiga kura ilikuwa kidogo katika kituo hicho. Muda wa kupiga kura mwisho ilikuwa ni saa 10.00 jioni.
Eneo la Mbagala, Mtendaji wa Mtaa wa Kizuiani, Magafu Maiko, alishambuliwa na wafuasi wa CCM na kulazimika kuokolewa na mgambo wa jiji.
Akizungumza na Tanzania Daima, Maiko alisema suala hilo lilimalizika baada ya askari polisi kufika eneo hilo na kuimarisha usalama.
Alisema katika kituo hicho wapiga kura walijitokeza, lakini tatizo kubwa ni wananchi wengi kutokujua kusoma, hali ambayo ilisababisha mpiga kura mmoja kukaa katika chumba cha kupigia kura kwa zaidi ya dakika 10.
Katika kitongoji cha Madenge, wananchi walilalamikia utaratibu na kuhofia kuwapo kwa udanganyifu mkubwa, hali itakayosababisha kupatikana kwa viongozi wasiofaa.
Mmoja wa wapiga kura hao, Hamza Salehe alisema utaratibu wa kupiga kura, hasa kwa wasiojua kusoma na kuandika, umewapa tabu kutokana na kukosekana kwa picha za mgombea.
Pia alilalamikia utaratibu wa ubandikwaji majina ya wapiga kura ambao haukufuata alfabeti, hali ambayo imewapotezea muda wingi wananchi na hata wengine kufikia hatua ya kukata tamaa.
"Unakuta mtu anatumia muda mwingi kutafuta jina lake, huu utaratibu hata sijui wameutoa wapi. Ni usumbufu tu, " alisema.
Pia alisema utaratibu huo umeruhusu udanganyifu kwa kuwa watu wasiojiandikisha wameweza kwenda kupiga kura kwa kutumia majina ya watu waliojiandikisha ambao hawakufika katika zoezi hilo.
"Naiomba serikali kubadili mfumo huu ambao unaweza kuleta madhara baadaye katika chaguzi zijazo, kwa kuweka utaratibu ambao hautakuwa na njia za udanganyifu," alisema Salehe.
Katika Mtaa wa Madenge kulikokuwa na upinzani mkubwa, kulitawaliwa na mvutano mkubwa kati ya wafuasi wa CCM na CUF ambao walikuwa wakiongoza mtaa huo.
Kutoka jijini Mwanza, Mwandishi Wetu anaripoti kuwa, wapiga kura walilazimishwa kutoa vitambulisho vya makazi ndipo waruhusiwe kupiga kura katika Kituo cha Mirogo.
Huku hali hiyo ikitokea, mmoja wa wagombea uenyekiti wa Mtaa wa Mabatini Kusini, Yohana Mnono maarufu Obama, amekatwa mapanga kichwani na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana.
Tukio hilo linadaiwa kutokea juzi, majira ya usiku wakati mgombea huyo akitoka kuzungumza na mawakala wake waliopangwa na chama chake cha CCM kusimamia kura katika mtaa huo, wenye upinzani mkali.
Katika tukio la kulazimishwa kutoa vitambulisho vya makazi, lililotokea kwenye kituo cha Mirongo, inadaiwa wapiga kura walipokuwa wakifika kwa ajili ya kupiga kura, walikuwa wakielezwa kuonyesha kitambulisho hicho, vinginevyo walikuwa wakifukuzwa na kukatazwa kupiga kura.
Tanzania Daima lililokuwa katika mizunguko ya kuangalia mwenendo wa zoezi zima la upigaji kura katika Jiji la Mwanza, lilielezwa kituoni hapo na baadhi ya wapiga kura kwamba, wananchi wengi wameshindwa kupiga kura kutokana na usumbufu huo.
Mmoja wa wapiga kura aliyezungumza na Tanzania Daima kituoni hapo, aliyejitambulisha kwa jina moja la Said alisema, hali hiyo ni mipango ya kutaka kuiba kura na kupunguza idadi ya kura za upande mmoja, hususani wa upinzani.
Alisema, wakati wa zoezi la kujiandikisha, walikuwa hawaombwi vitambulisho kama ilivyokuwa jana na kwamba wanashangazwa na kitendo hicho.
Kuhusu tukio la kucharangwa mapanga kichwani mgombea wa CCM, limechukuliwa na wananchi kama hatua ya uhasama wa kisiasa uliopo baina ya CCM na kambi ya upinzani katika maeneo mengi ya jiji hilo ukiwemo mtaa huo wa Mabatini Kusini.
Akizungumzia kukatwa kwake mapanga, mgombea huyo alisema, anaamini watu waliohusika katika tukio hilo, ni wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), kwa kile alichosema walikuwa wakipitapita maeneo hayo nyakati za usiku.
Hata hivyo, wasimamizi wa uchaguzi katika vituo hivyo hawakupatikana kuzungumzia matukio hayo mawili ya kuombwa vitambulisho vya makazi na kukatwa mapanga kwa mgombea huyo.
Mbali na kasoro hizo, baadhi ya vituo vya kupigia kura, wananchi wengi walikosa majina yao, huku wengine majina yao yakiwa yamebandikwa nje, lakini ndani hayaonekani.
Kutoka Tanga, katika Kijiji cha Kwadiboma, Kitongoji cha Kwa Mkongoye, wilayani Kilindi, makomandoo wa CCM walidaiwa kupora masanduku ya kura na kuyachoma moto baada ya kubaini wagombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wameshinda.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu kutoka Kilindi jana, Mwenyekiti wa CHADEMA wa wilaya hiyo, Salimu Ramadhan, alidai hali hiyo imeleta vurugu kubwa hali iliyosababisha polisi kuingilia kati.
Mwenyekiti huyo alidai juzi usiku wafuasi wa CCM wakiongozwa na mbunge wao walikwenda katika Kijiji cha Mzinga Gezaulole na kuwahonga wagombea wa chama chake baiskeli, mabati 20 na simu za mkononi, ili kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho.
Pia alidai wafuasi hao wa CCM walikwenda katika Kijiji cha Kibilashi na kuwahonga wagombea wa CHADEMA fedha taslim sh 50,000 huku wakitishiwa kuwa kama hawatajitoa usalama wa maisha yao utakuwa hatarini.
"Huku Kilindi hakuna uchaguzi, ni vurugu tupu, wagombea wetu wamehongwa na watu wa CCM na katika kijiji ambacho wamebaini tumeshinda, makomandoo wa CCM wamepora masunduku ya kura na kwenda kuyachoma moto," alisema mwenyekiti huyo.
.