Nasema itakuwa ni ushujaa na kutanguliza maslahi ya taifa, itakuwa ni njia pekee sahihi na muafaka ya kuonesha kutokubaliana na uchaguzi huu batili uliojaa hila, fitina na nia ovu.
Kama tume itakataa kuwarudisha wagombea ubunge zaidi ya 150 wa upinzani hususani ACT na CHADEMA waliowaengua kwa sababu moja ama nyingine basi upinzani ukubali tu kuwa kujitoa kushiriki uchaguzi ndiyo njia pekee sahihi na muafaka.
Mpaka sasa kwa mujibu wa Zitto Kabwe wagombea ubunge wa chama hicho zaidi ya majimbo 45 Tanzania bara na Zanzibar wameenguliwa. CHADEMA mpaka sasa ni karibia majimbo 25 kwa Tanzania Bara sijajua huko Zanzibar na bado uenguaji unaendelea. Na hapo kuna wagombea pia wa CUF, NCCR wameenguliwa, ukijumlisha unapata idadi ya wagombea wasiopungua 150 kwa vyama vyote vya upinzani nchi hii.
Hapo bado sijazungumzia udiwani, majimbo ambayo wagombea ubunge wa upinzani wameondolewa kuna wagombea udiwani at least wasiopungua 10 wanaondolewa. Sasa idadi ya madiwani ni makumi kwa mamia wanaondolewa.
Je upinzani bado unaamini una haja ya kuendelea kushiriki uchaguzi huu? Je upinzani utaendelea kujilisha upepo mpaka lini?
Upinzani kuendelea kushiriki uchaguzi huu ni kujiaibisha wenyewe. Sisi sote ni watu wazima na wenye uelewa. Hatutakiwi kujidanganya, kujipa matumaini hewa na kujilisha upepo. Kusema eti watanzania watakubali kuandamana kupinga udhalimu huu ni uongo, watanzania ni waoga sana, hivyo mwitikio mdogo wa hayo maandamano utapelekea hao wachache watakaoitikia kuumia na hiyo itawavunja moyo na kuendelea kuwaogopesha wengi.
NI ATHARI ZA KUENDELEA KUSHIRIKI HUU UCHAGUZI?
Ni kuwasindikiza CCM, kuendelea kubariki uhuni wanaoufanya, kuendelea kushiriki dhuluma yao na najisi kwa umma.
Kushiriki huu uchaguzi na wakati unajua mwenzako ana majimbo 25 Zanzibar na 30 bara ambayo amejitwalia mezani. Halafu unaenda kugombania majimbo 200 ambayo pia uhakika wa kutangazwa hauna ni kujidanganya big time.
Ishu isiwe Lissu tu, hapo ndipo tunapodanganywa tunang'ang'ana na Lissu huku wenzetu wanajizolea ubunge na udiwani wa dezo mpaka ikifika siku ya uchaguzi na huyo Lissu naye wanamuibia kura tunabaki na kitu gani?
Tujitoe mapema sana kabla hatujafika hata mwisho mwa kampeni. Najua watasema tunamwachia fisi bucha ni heri tuonekane tulimwachia fisi bucha kuliko tukaonekana tulishiriki pamoja na fisi kula nyama buchani kumbe tuliambulia mifupa michache tu.
Magufuli anataka kuthibitisha ile kauli yake kwamba ameufuta upinzani na hapo anajiona mjanja sana maana aliteua wana ccm kwenye ukurugenzi makusudi na matokeo yake yanaonekana sasa hivi. Sasa sisi tusiwe sehemu ya kumsindikiza Magufuli kwenye hiyo project yake.
Narudia tena utakuwa uzalendo na ushujaa kususia uchaguzi huu kuliko kujidanganya na kujilisha upepo kuwa tutashinda pamoja na mwenendo mzima unavyoonekana katika hizi hatua za mwanzo.