Upungufu wa vyoo shuleni wadau wataka Serikali kuchukua hatua

Upungufu wa vyoo shuleni wadau wataka Serikali kuchukua hatua

UTPC

Journalists' Union
Joined
Apr 17, 2026
Posts
51
Reaction score
38
Tatizo la upungufu wa matundu ya vyoo katika shule za Manispaa ya Shinyanga, limeendelea kuwa changamoto inayotishia afya na ustawi wa wanafunzi, huku baadhi yao wakilazimika kujisaidia vichakani kutokana na vyoo kujaa, kuchakaa na kutokidhi idadi ya wanafunzi.

Mbali na upungufu huo, baadhi ya shule hazina vyumba maalumu vya wanafunzi wa kike kujistiri wakati wa hedhi, hali inayowaweka katika mazingira yasiyo rafiki kiafya na kuathiri ustawi wao wanapokuwa shuleni.

Kutokana na hali hiyo, wadau mbalimbali wameishauri Serikali, kuanzisha kampeni maalumu ya kitaifa ya ujenzi na ukarabati wa vyoo shuleni, wakieleza kuwa msukumo wa aina hiyo unaweza kuwa njia ya haraka ya kupunguza na hatimaye kumaliza tatizo hilo ambalo limeendelea kwa miaka mingi.
Screenshot 2026-10-09 174359.png

Mwalimu wa Malezi, Afya na Mazingira wa Shule ya Msingi Bugimbagu, Cletisia Manda akionyesha vyoo vya shule hiyo, hivi karibuni, ambavyo ni pungufu na kupelekea wanafunzi kujiasaidia vichakani.
PICHA: MARCO MADUHU
​

Kwa mujibu wa wadau hao, suluhisho halipaswi kuishia katika kujenga vyoo vipya pekee, bali linapaswa kwenda sambamba na utekelezaji madhubuti wa Mwongozo wa Kitaifa wa Maji, Usafi wa Mazingira kwa Shule za Tanzania (SWASH) wa mwaka 2009, pamoja na kuweka bajeti maalumu na mfumo wa kufuatilia utekelezaji wake.

Diwani wa Kata ya Kizumbi Rubeni Kitinya, anasema kata hiyo ina shule tano za msingi za Serikali, lakini baadhi yake zinakabiliwa na hali mbaya ya miundombinu ya vyoo.

Anataja shule ya Msingi Buyambelele kuwa miongoni mwa shule zenye changamoto hiyo, akisema baadhi ya vyoo vimejaa na hivyo kuwalazimu wanafunzi kujisaidia vichakani.

Anasema tatizo hilo halipo Shinyanga pekee, bali linajitokeza katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo serikali inapaswa kuchukua hatua za makusudi kulitatua.

“Serikali kupitia Wizara ya Afya na TAMISEMI zishirikiane kuanzisha kampeni maalumu ya kupambana na upungufu wa vyoo shuleni, ambapo wakurugenzi wapewe agizo maalumu kwamba kila halmashauri ijenge idadi kadhaa ya matundu ya vyoo kila mwaka na utekelezaji wake ukaguliwe,” anasema Kitinya.
MWANAFUNZI NGW'IHANDO NA MWADISHI.JPG

Anazitaja kampeni za kitaifa ambazo zilizowahi kufanyika, ikiwamo ujenzi wa shule za sekondari kwa kila kata na vyumba vya madarasa, na kudhihirisha kwamba, serikali inapoweka msukumo maalumu kwenye miradi, inaweza kutekelezwa kwa kasi na kwa mafanikio makubwa.

Kwa mtazamo wake, mkakati kama huo ukitumika katika ujenzi wa vyoo, tatizo hilo linaweza kupungua kwa kiwango kikubwa na hatimaye kubaki kuwa historia.

Anashauri, pia katika miradi ya ujenzi wa vyumba madarasa inayoendelea, kwamba bajeti zake ziingizwe na matundu ya vyoo, ili tatizo la vyoo lianze kupungua sambamba na ujenzi wa vyumba hivyo.

Diwani wa Kata ya Kolandoto Moses Mshagatila, anataja suluhu nyingine ya utatuzi wa upungufu wa vyoo shuleni, ni kuhamasisha wananchi kuchangia nguvu kazi badala ya kusubiri bajeti ya serikali pekee.

Anasema mbinu hiyo tayari wameaza kutekelezwa katika Shule ya Msingi Kolandoto, ambako ujenzi wa matundu manne ya vyoo unaendelea.

Anasema kwa sasa bajeti ya kata imeelekezwa zaidi katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, kutokana na kuwepo pia kwa upungufu mkubwa wa miundombinu hiyo.

Hata hivyo, anashauri Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vyoo, kwa kuwa shule nyingi za msingi zina miundombinu iliyochakaa na haiendani na mahitaji ya wanafunzi.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya Msingi Ng’wihando Shabani Mantenga, anasema miundombinu ya vyoo katika shule hiyo, imechakaa huku baadhi ya matundu yakisitishwa kutumika kutokana kuwa mabovu.

“hali ni mbaya sana, hata chumba cha wanafunzi wa kike kujistiri na hedhi ambacho tulikitenga mwaka 2018 hakitumike tena sababu kiliharibika na tukakosa fedha ya ukarabati sh, 600,000, tunaomba serikali katika bajeti zake ziangalie zaidi shule zilizo na hali mbaya, amesema Matenga.

Mwanafunzi wa shule hiyo, Lucy Gabriel, anaiomba Serikali kuwajengea matundu ya vyoo pamoja na chumba maalumu cha kujistiri wakati wa hedhi ili kunusuru afya za wanafunzi.

Anasema kutokana na upungufu wa vyoo, baadhi ya wanafunzi hulazimika kujisaidia maeneo ya pembeni, huku baadhi ya vyoo vikiwa havina mfumo wa mabomba ya maji.

Naye mwanafunzi wa shule ya Msingi Old Shinyanga, Rehema Mwandu, anasema upungufu wa matundu ya vyoo husababisha wanafunzi kusubiri foleni ndefu kila wanapotaka kutumia choo wakati wa mapumziko.

Mwanafunzi wa shule ya sekondari Emiliana Mtei, anasema shule hiyo yenye wanafunzi wa kike 285 haina chumba maalumu cha kujistiri wakati wa hedhi, bali hutumia choo kimoja kilichotengwa kwa matumizi hayo.

Anaiomba serikali, kuweka kipaumbele katika bajeti zake kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vya kutosha na vyumba maalumu vya kujistiri wakati wa hedhi.

“Shule yetu ipo mjini kabisa, lakini tunasoma katika mazingira ambayo si rafiki kiafya, kutokana na upungufu wa matundu ya vyoo na kutokuwapo kwa chumba maalumu cha kujistiri wakati wa hedhi,” anasema Mtei.

Wakati suluhisho la muda mrefu likiwa ni kuongeza na kuboresha miundombinu, wataalamu wa afya wanashauri pia hatua za haraka zichukuliwe katika shule ambazo bado hazijapatiwa vyoo vya kutosha.

Daktari wa magonjwa ya dharura na mlipuko katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dk. Kambi Buteta, anasema moja ya hatua za haraka ni kuhakikisha shule zinakuwa na ndoo za kunawia mikono zenye maji safi na sabuni.

Anasema, hatua hiyo itasaidia wanafunzi kujisafisha baada ya kutumia vyoo na kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa mbalimbali, wakati serikali ikiendelea na mipango ya kujenga na kuboresha miundombinu ya vyoo.

Ofisa Takwimu wa Manispaa ya Shinyanga Bopali Mwakiluma, anasema bajeti ya serikali haiwezi kukidhi kwa wakati mmoja mahitaji yote ya kumaliza upungufu wa matundu ya vyoo na vyumba maalumu vya kujistiri wakati wa hedhi shuleni.

Kwa sababu hiyo, anawaomba wadau wa maendeleo kuendelea kuisaidia serikali katika kukabiliana na changamoto hiyo.

Anasema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, Manispaa ya shinyanga imetenga sh. milioni 118.8 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 54 ya vyoo pekee, wakati upungufu uliopo unafikia matundu 1,145.

Kwa mujibu wa Mwakiluma, anasema matundu hayo 54 yataelekeza katika shule ambazo miundombinu yake ya vyoo iko katika hali mbaya zaidi, huku serikali ikiendelea kutenga fedha kila mwaka ili kutatua tatizo hilo hatua kwa hatua.

Hata hivyo, hatua za kusaidia shule zimeanza pia kupitia wadau wengine, ambapo Aprili 19 mwaka huu Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Samweli Jackson, alifika katika shule ya Sekondari Town na kutoa sh. milioni 3.3 kupitia fedha za mfuko wa jimbo kwa ajili ya ukarabati wa vyoo vya shule hiyo vilivyokuwa katika hali mbaya.

Anasema katika mgawanyo wa fedha za mfuko wa Jimbo, kila kata huwasilisha mapendekezo ya miradi inayopaswa kupewa kipaumbele, na baadhi ya kata zimependekeza ukarabati wa miundombinu ya vyoo.

Mdau wa elimu Flaviana Matata, anasema taasisi yake imekuwa ikisaidia ujenzi wa vyumba maalumu vya kujistiri wakati wa hedhi shuleni katika Manispaa ya Shinyanga, pamoja na kusaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo.

Anasema vyoo vya wasichana vinapojengwa pamoja na maeneo ya kujistiri wakati wa hedhi, vinasaidia pia kupunguza msongamano wa matumizi ya vyoo katika shule.

Julai 23, 2026, Flaviana alikabidhi jengo la choo cha wasichana lenye vyumba vya kujistiri wakati wa hedhi katika Shule ya Sekondari Busulwa Manispaa ya Shinyanga.

Amesema Jengo hilo litahudumia wanafunzi wa kike 502, hatua inayolenga kuwaondolea adha ya ukosefu wa vyumba vya kujistiri na kulinda afya zao.

Mwananchi wa Manispaa ya Shinyanga Joseph Nkalango, anasema changamoto ya upungufu wa matundu ya vyoo na vyumba maalumu vya kujistiri wakati wa hedhi, haiwezi kuendelea kutazamwa kama tatizo la kawaida.

Anasisitiza, umuhimu wa kuwepo kwa kampeni maalumu ya kitaifa, pamoja na usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa mwongozo wa SWASH.

Kwa mantiki hiyo, suluhisho la tatizo hilo linahitaji hatua zaidi ya ujenzi wa matundu machache kila mwaka. linahitaji mpango wenye malengo yanayopimika, bajeti maalumu, ushirikishwaji wa wadau na ufuatiliaji wa utekelezaji katika kila halmashauri.

Iwapo kila halmashauri itawekewa malengo ya wazi ya kuongeza idadi ya matundu ya vyoo kila mwaka, huku miradi ya ujenzi wa madarasa ikiambatana na vyoo na wadau wa maendeleo wakishirikishwa, upungufu huo unaweza kupungua kwa kasi.

Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.
 
Back
Top Bottom