Uraia Hai ni chachu ya mabadiliko chanya katika jamii

Uraia Hai ni chachu ya mabadiliko chanya katika jamii

The Sheriff

JF-Expert Member
Joined
Oct 10, 2019
Posts
747
Reaction score
2,112
RAIA HAI KATIKA JAMII.jpg


Uraia Hai (active citizenship) unamaanisha watu kujihusisha katika jamii zao na demokrasia katika ngazi zote na kuelewa kuwa sisi sote ni tofauti, lakini jukumu la kubadilisha jamii zetu ni sawa. Uraia hai unaweza kuanzia katika ngazi ndogo kama vile kampeni ya kusafisha mtaa wako au kubwa kama kuelimisha jamii kuhusu maadili ya kidemokrasia, ujuzi na ushiriki. Uraia hai ni mojawapo ya hatua muhimu zaidi katika kutengeneza jamii bora, hasa katika nchi za kidemokrasia kama Tanzania.

Katika jamii unayoishi unapata kujua watu na kusikia kuhusu maeneo ambayo yanahitaji maboresho na mabadiliko ya ziada. Kujifunza zaidi kuhusu eneo unaloishi (pamoja na maeneo yanayolizunguka kwa ujumla) kunaweza kukusaidia kuwa raia hai zaidi. Kuna njia nyingi za kujitolea wakati na nguvu zako kusaidia kufanya jamii yako kuwa mahali bora zaidi pa kuishi.

Yapo mambo mengi tu ambayo mtu anaweza kufanya ili kuwa raia hai.

Kwa mfano, ni vema ujihusishe au ujielimishe vyema kuhusu siasa za eneo lako. Huenda hujawahi kuwaza kugombea nafasi ya aina yoyote, lakini hapa ndipo mahali ambapo unaweza kuleta mabadiliko zaidi katika sera. Ni vema kuhudhuria mara kwa mara mikutano ya eneo lako na kufahamu masuala ambayo viongozi wako na wananchi wenzako wanajadili.

Si lazima kuwa kiongozi au kuwa na nia ya kushika uongozi ndiyo uwe raia hai katika eneo lako. Ushiriki hai unakupa fursa ya kukutana na watu wengi wanaoishi katika eneo lako ambao hujawahi kukutana nao, hivyo kujua changamoto na maendeleo ya eneo lako, pamoja na fursa ya kujua endapo msaada wako unahitajika kwa ajili ya maendeleo ya pamoja.

Raia hai anapaswa kuwa na taarifa za kutosha, anajua haki na wajibu wake, na anaweza kutoa maoni yake bila hofu. Anahusika katika maisha ya jamii yake na kushiriki katika kufanya maamuzi yanayohusu jamii yake. Kwa maneno mengine, raia hai wanachukua mambo mikononi mwao ili kubadilisha hali halisi inayowazunguka.

Kushiriki katika shughuli za kujitolea ni jambo jema pia. Hii inamaanisha kujitolea bila kutarajia malipo ya kifedha. Baadhi ya malipo hayawezi kubadilishwa kuwa pesa, kama vile tabasamu la mtu mwenye uhitaji na shukrani zao. Kuna fursa nyingi za kujitolea kwa sababu watu wengi wanahitaji msaada huo.

Pia, kujitolea kunaweza kuwa shughuli ya kupanda miti, kusaidia masikini au kufundisha jamii mbinu mbalimbali muhimu za maisha. Ili kupata fursa ya kujitolea inayokuvutia zaidi, unaweza kutafuta mashirika/taasisi zilizo karibu ambayo zinashughulika na suala ambalo una interest nalo au ni muhimu kwako.

Kumbuka tu kwamba hakuna suluhisho moja la changamoto za kijamii, hivyo raia hai anaweza kutafuta namna yoyote inayoweza kuleta mabadiliko chanya katika jamii yake.

Jamii zina uwezekano mkubwa wa kustawi kunapokuwa na raia hai ambaye anachangia vyema katika maisha ya kisiasa na ya umma kama mpiga kura, raia mwenye taarifa, mpenda maendeleo na mwenye moyo wa kujitoa kwa ajili ya jamii yake.
 
Back
Top Bottom