19th May 2009
CCM yaonya italipuka kama Mbagala
Yaasa wananchi kuhudhuria mikutano
Nguzo za umeme zasambazwa jimboni
Chama tawala sasa wabadili mbinu
Mgombea wa kiti cha Ubunge jimbo la Busanga kupitia Chama cha Mapinduzi, Lolesia Bukwimba akiwainamia wanakijiji cha Nyachiluluma kilichopo wilaya ya Geita.
Wananchi wakimsikiliza mgombea wa CHADEMA katika kampeni za kugombea kiti cha Ubunge wa jimbo la Busada.
Habari zilizozagaa katika jimbo la Busanda kwamba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kitaanza kampeni zake wiki hii kwa kutumia helikopta, zimeongeza homa ya uchaguzi na wapinzani wao wamezua jambo kuhusu usafiri huo.
Chadema ambayo imekuwa na utaratibu wa kutumia helkopta katika kampeni zake, inadaiwa kwamba itatumia usafiri huo katika wiki hii ya lala salama kabla ya kupigwa kura Jumapili ijayo katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni humo.
Kutokana na taarifa za helikopta kusambaa Busanda, makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wametahadharisha wananchi kuhudhuria mikutano yenye helkopta hiyo kwa madai kwamba litalipuka.
Gari la matanzo la CCM juzi na jana lilikuwa likiranda katika mitaa jimboni humo likiwaonywa wananchi kutokuhudhuria mikutano ya helikopta, kwani wanaweza kulipukiwa kama mabomu ya Mbagala.
Magari ya CCM yaliyofungwa spika yamekuwa yakitoa matangazo kwamba helikopta hiyo inaweza kulipuka kama mabomu ya Mbagala jijini Dar es Salaam ajali iliyotokea Aprili 29, 2009 na kuua watu 26 na kujeruhi kadhaa.
"Mkihudhuria mikutano ya Chopa (helikopta) linaweza kulipuka kama mabomu mnayoyasikia huko Mbagala," alitangaza mkereketwa mmoja katika gari ya matangazo.
Hata hivyo tofauti na vishawishi hivyo, wananchi wengi wanaonekana kuwa na shauku ya ujio wa Chopa.
Jana Chadema walitangaza kwamba helikopta wanatakayotumia itawasili leo jimboni humo kwa lengo la kumnadi mgombea wao, Finias Magesa.
Akitumia helkopta hiyo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, anatarajia kufanya mikutano mitano kwa siku.
Nguzo za umeme zasambazwa Busanda
Wakati hayo yakitokea watu waliojitambulisha kama wafanyakazi wa Tanesco, wamemwaga nguzo za umeme katika maeneo ya Bukondo na kuwaeleza watu kwamba kuna mpango wa kuwapelekea umeme.
Hatua hiyo imelalamikiwa na vyama vya upinzani jimboni hapa, kwa vile ina lengo la kuwaghilibu wananchi.
Mgombea wa ubunge kwa tiketi ya Chadema Mhandisi Finias Magesa, alisema watu hao sio wafanyakazi wa Tanesco, bali ni makada wa CCM.
Akihutubia wananchi wa Kata ya Lwamgasa Magesa alisema hatua hiyo ya CCM ni utapeli, kwa vile hakuna umeme unaoweza kufikishwa sehemu, bila kwanza eneo husika kupimwa.
"Sasa kama wanaleta umeme kwa nini nguzo zianze kumwagwa Bokondo, badala ya kuanzia kule Geita umeme unapotoka, huu ni utapeli wa CCM na wala sio Tanesco," alisema.
Katika hatua nyingine Tanzania Labour Party (TLP) kimetangaza kumuunga mkono mgombea wa CUF, Oscar Ndalahwa.
Uamuzi huo ulitangazwa mjini hapa na Katibu wa Chama hicho wilayani Geita Emanuel Silas.
"Sisi TLP tumeamua kukipigia debe chama cha CUF katika uchaguzi wa Busanda," alisema Katibu huyo.
Polisi: Hatujapokea malalamiko ya Chadema
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi nchini limesema halijapokea malalamiko kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) dhidi ya Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Geita, Shaban Kimea kwa madai ya kuisaidia CCM, katika kampeni zake za kuwania kiti cha ubunge jimbo la Busanda.
Msemaji wa Jeshi hilo, Juma Ally, alisema jana kuwa ofisi yake haijapokea malalamiko kutoka kwa mtu binafsi, taasisi au chama chochote kuhusu madai kwamba OCD Kimea amekuwa akikisaidia CCM katika kampeni zake.
"Inawezekana labda malalamiko yao wamepeleka kwa Tume ya Uchaguzi, lakini ofisi yetu haijapokea malalamiko dhidi ya OCD wa Geita," alisema na kuongeza:
"Malalamiko hayo yametolewa na nani na lini…ofisi yangu haijapokea malalamiko yoyote kuhusu OCD huyo. Unajua Jeshi la Polisi ni kubwa na lina utaratibu wake wa kupokea malalamiko, pengine inawezekana malalamiko hayo yamewasilishwa kwanza kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, lakini hapa ofisini kwangu hayajafika."
Wiki iliyopita, Chadema kilitoa malalamiko katika mikutano ya hadhara ya kampeni za uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge katika jimbo la Busanda, kikimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekata Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema, kumhamisha OCD wa Wilaya ya Geita kwa kile walichodai kuwa anakiuka taratibu za kampeni za uchaguzi kwa kukisaidia chama tawala kiweze kushinda katika uchaguzi huo mdogo.
Inadaiwa kuwa polisi wilayani humo wamekuwa wakiwatawanya wanachama wa Chadema pale wanapokusanyika katika ofisi zao kwa mikutano ya ndani na wakati mwingine kuwakamata wanachama wake kwa madai ya kuleta vurugu.
Vipigo vyaendelea kutolewa
Katika hatua nyingine vipigo vimeendelea kutawala mikutano ya hadhara ikiendeshwa na walinzi wa mikutano ya CCM.
Katika mkutano wa CCM uliofanyika jana saa 4:30 asubuhi kijiji cha Nyachiluluma wilayani humo kumnadi mgombea wake Lolesia Bukwimba, wafuasi wanaodhaniwa kuwa ni wa Chadema walipata kipigo kutoka kwa walinzi hao wa CCM.
Wakati mkutano huo ukiendelea, walipita vijana watatu wakiwa na pikipiki huku wakipeperusha bendela ya Chadema karibu na eneo hilo, lakini waliporejea walinzi hao wa CCM wanaojiita Green Guard, walimkamata mmoja wao na pikipiki yake na kuanza kumpiga kisha kumpeleka katika gari lao.
Wakati tukio hilo linatokea, hapakuwepo na askari yeyote kama wanavyoonekana katika mikutano inayofanyika mijini ambako mara zote Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wametanda wakiwa na silaha za moto na mabomu ya machozi.
Katika mkutano huo, Mbunge wa Same Mashariki na Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC), Anne Kilango Malecela, aliwaambia wananchi wa kijiji hicho kuwa wasisikilize maneno ya wapinzani kuwa CCM ni mafisadi.
Kilango alisema hakuna serikari yoyote duniani ambayo haina viongozi ambao siyo waadilifu: "Nakiri katika chama changu kuna mtu mmoja mmoja ambao wanafanya mambo ya ufisadi. Ila sisi wenyewe katika chama huwa tunasemana na ndio maana nipo hapa kumuunga mkono mwanamke mwenzangu muchagueni kwani yeye sio fisadi."
Naye Mbunge wa Ilemela na Mjumbe wa NEC, Anthony Dialo, aliwataka wanakijiji hao kutowachagua watu wanaotaka kura kwa kutoa chumvi na fedha.
Mgombea huyo, Bukwimba, akijinadi huku amechuchuma akiomba kura, alioambia wanachi hao wamchague ili aendeleze mambo mazuri aliyoacha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu Faustine Rwilomba Kabuzi.
Alisema ataendeleza sekta ya elimu, kilimo na kwa wafanyabiashara ndogo ndogo kwa kuwatafutia mikopo ili kukuza biashara zao.
CCM wabadili mbinu
Katika hatua nyingine, CCM jana kiliahirisha mkutano wake uliopangwa ufanyike eneo la CCM Centre na sasa wanaendesha vikao vya ndani.
Wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Bara, George Mkuchika, waliamua kufanya mkutano wa ndani, uliowajumuisha baadhi ya wazee na vijana wafanyabiashara.
Katika mkutano huo, habari zinasema kwamba Mjumbe wa kudumu wa Kamati kuu ya CCM, John Malecela, alishindwa kuwazoa wafanyabiashara 50 wa Soko la Katoro, ambao alikutana nao katika mkutano wa ndani.
Malecela alifika eneo hilo jioni akiwa na gari namba T 509 AFZ aina ya Toyota Land Cruiser, akiwa amefuatana na baadhi ya wapiga debe wa CCM.
Katika mkutano huo Malecela alisema ameamua kuwaita wafanyabiashara hao na kufanya nao mkutano wa ndani kwa lengo la kuwashawishi wakisaidie CCM.
Aliwaahidi wafanyabiashara hao wakichague CCM kwa vile kwa kutumia kofia yake ya chama tawala, itahakikisha inaboresha soko hilo na kuondoa kero zote zilizopo.
Hata hivyo mkutano huo wa ndani ulifichuka na kuwa kama wa hadhara baada ya wafanyabiashara hao kupiga makelele ya kusema wamechoka na CCM.
Mmoja wa vijana hao, Marando Malya, alimuuliza kama wao vigogo wamefikwa maji ya shingo, wakiingia vijana si watazama kabisa.
"Mheshimiwa sasa kama ninyi mpo maji ya shingo tukiingia sisi wadogo si tutazama kabisa?"alihoji Malya hali iliyozua ashangiliwe kwa nguvu.
Kutokana na ugumu huo, kikao hicho kiliahirishwa.
Imeandikwa na Simon Mhina, na Edwin Mjwahuzi (Busanda) na John Ngunge (Dar).
CHANZO: NIPASHE