SoC01 USHAURI: Matumizi sahihi ya Fedha za Pensheni kwa Wastaafu

SoC01 USHAURI: Matumizi sahihi ya Fedha za Pensheni kwa Wastaafu

Stories of Change - 2021 Competition

DustBin

JF-Expert Member
Joined
Jun 3, 2021
Posts
609
Reaction score
604
Fedha za pensheni ni malipo anayopewa mwajiriwa (mfanyakazi) baada ya kustaafu kazi/ajira yake. Huwa ni fedha nyingi ukilinganisha na fedha ambazo huyo mfanyakazi/mwajiriwa aliwahi kumiliki hapo kabla.

Wastaafu wengi kutapeliwa

Hivi karibuni kumezuka matukio mbalimbali yakiwahusisha wastaafu mara baada ya kupata fedha zao za pensheni, kama vile kuibiwa (kutapeliwa), matumizi mabaya ya fedha, kufanya mambo yasiyo na murua katika jamii, na mara nyingine kusababisha hasara kwa taifa na hata kusababisha vifo. Na ndio maana baada ya kutafakari kwa kina serikali ya awamu ya tano iliyokuwa ikiongozwa na hayati John Pombe Magufuli ikaamua kuja na mpango wa kuwasaidia wastaafu hao kupokea fedha zao kwa awamu. Ingawa wengi hawakupendezwa na mpango huo lakini lengo lilikuwa kuwasaidia hawa wastaafu ambao wengi hupatwa na matukio yasiyo ya kawaida pindi wanapopewa fedha zao, jambo ambalo hupelekea kutodumu kwa fedha hizo na kama zikibahatika kudumu basi hukosa kufanyiwa cha maana.

Kupata kiasi kikubwa cha fedha ghafla huwachanganya wengi

Wastaafu wengi hasa walimu (ndio ambao uchunguzi wangu nimeufanya kwao) fedha zao za pensheni wanazolipwa huwa naweza kusema zinawazidi kiwango. Wengi wao huwa katika maisha yao hawajawahi kuhodhi kiasi kikubwa cha fedha kama hizo hivyo huwapelekea kuwa na kichaa cha fedha (kimuhemuhe) kiasi wakashindwa kuzidhibiti katika matumizi. Na wengine ambao huweza kuzidhibiti huzitumia fedha hizo katika kujenga nyumba, kununua magari, na kufanya starehe zingine binafsi. Na wengine masikini hutumia fedha zao za pensheni hata kabla hawajazikamata mkononi kutokana na madeni.

Inasikitisha sana kuona mfanyakazi aliyetumikia ajira yake takribani miaka ishirini au zaidi, mpaka anafika umri wa kustaafu anakuwa bado hajajenga nyumba ya maana ya kuishi yeye na familia yake angalau. Kwa kawaida fedha za pensheni ni fedha ambazo mfanyakazi aliyestaafu anatakiwa azitumie kwa kuendesha maisha yake kwa kujipatia mahitaji muhimu kwa kipindi chote atakachokaa bila ya mshahara mpaka hapo mauti yatakapomfika.

Kuingiza pesa za pensheni kwenye ujenzi au miradi mikubwa

Kutumia fedha hizo na kuziingiza kwenye matumizi makubwa kama kujenga nyumba, au kuziingiza kwenye miradi mikubwa ni kujichimbia shimo la kujiangamiza. Uzoefu unaonesha wastaafu wengi ambao hujenga baada ya kustaafu huwa hawamalizi ujenzi huo. Fedha huisha na huku ujenzi unahitajika uendelee, kwani wakati wanazitumia fedha hizo kwa ajili ya ujenzi bado sehemu ya fedha hizo hutumika katika matumizi mengine ya lazima.

Na hata wale ambao hutumia fedha za pensheni kuanzisha miradi kama vile kufungua duka, au kampuni au kiwanda hushindwa kuendesha miradi hiyo kwani hukosa weledi na uzoefu wa kuendesha miradi kimaslahi. Hivyo utaona mradi unadumu miaka miwili au mitatu kisha unakufa moja kwa moja huku mstaafu akirudi mtaani kuishi maisha ya kuhangaika asiwe na msimamo madhubuti katika maisha yake. Mwisho wa siku anapatwa na shinikizo la damu anakufa ghafla, waswahili husema anakufa kabla ya siku zake.

Andaa mazingira ya kustaafu mapema

Enyi wafanyakazi wenzangu, enyi waajiriwa wenzangu nisikilizeni kwa makini sana. Jitahidi katika kipindi chako cha kazi (ukiwa kazini) kujiandalia maisha yako ya baada ya kazi. Jitahidi ujenge nyumba ya kuishi wewe na familia yako ukiwa kazini, jitahidi na ikiwezekana pambana angalau ununue hata kigari kidogo cha kutembelea, siku hizi magari yanauzwa bei rahisi sana.

Jitahidi na upambane uwe na mradi unaokusaidia kupata mahitaji muhimu ya nyumbani ili mshahara wako ufanye mambo mengine ya kimaendeleo. Ni aibu kubwa tena kubwa sana kwa mtumishi uliyetumikia ajira yako miaka nenda rudi kisha mpaka unafika wakati wa kustaafu hauna nyumba ya kueleweka ya kuishi. Nunua mashamba wakati upo kazini ili utakapostaafu utumie sehemu ya hiyo fedha kuyaboresha mashamba yako ili uishi kwa raha mustarehe.

Zamani enzi za ujamaa hapa kwetu kabla hatujaingia kwenye soko huria hili la mfanyakazi kuwa na umiliki wa hivi nilivyovitaja kweli haikuwezekana. Lakini dunia ya sasa ni tofauti na ile ya zamani. Kuna ambao wanaona haiwezekani kwa mfanyakazi/mtumizi hasa mwalimu akajenga nyumba safi, akamiliki usafiri, akamiliki miradi binafsi kwao wao hili haliingi akilini, wamezoea maisha yale ya zamani. Eti mshahara hautoshi, nani alikuambia mshahara unatosha?

Mshahara haujawahi kuwa mwingi

Hakuna ambaye mshahara wake unamtosha, kinachotumika ni akili yako namna ya kuusimamia vizuri mshahara wako. Inawezekana tena bila hata kufanya ubadhilifu wa mali za uma au kujiingiza kwenye vitendo haramu kama vile rushwa. Kikubwa usiwe na matumizi ya kuzidi uwezo wako hapo utakwama na yatakukuta yanayowakuta wastaafu wengi leo hii hapo utakapostaafu. Kuna baadhi ya watumishi/wafanyakazi ili aonekane na yeye mwanae anasoma kwenye shule za kulipia anampleka bila kujali kipato chake hakiruhusu. Wakati iliwezekana mwanae asome kwenye shule za jumuiya na kile kiasi cha fedha angeweza kumpatia mwanae mahitaji yote ya shule akasoma bila matatizo na angeweza kuwa na uwezo wa kufanya mambo mengine ya maendeleo.

Wito wangu

Wito wangu kwa wafanyakazi, tujipange vyema kwa ajili ya maisha yetu ya baadae na tuwe na uthubutu, maisha ya bila mshahara. Na kingine cha msingi sana tujitahidi tuzae mapema, fedha za pensheni sio za kusomeshea watoto. Watoto wasome wakati upo kwenye kazi, ukishastaafu na wao muda wa kuwalipia masomo uwe umeisha na kama kuna watoto wengine walichelewa basi wale watoto wako wa mwanzo ndio watasimamia jukumu hilo wewe uwe kama unasaidia tu.

Fedha za pensheni ni za matumizi yako wewe kwa ajili ya mahitaji yako muhimu na starehe kidogo. Ukishafikia umri wa kustaafu sio muda wa kupata msongo wa mawazo wa hili na lile, huo ni muda wa kupumzisha akili na kuishi kwa saada huku ukisubiria siku yako ya kwenda kwa mola wako.

Kama hautojipanga mapema basi hapo baadae utakua mzee msumbufu sana, na utalaumu serikali mpaka utakufa, maana serikali ndio ya kwanza kulaumiwa kwa kila kitu. Ili uweze kujikimu ndio pale utapoanza na wewe kuanza kufanya kazi upya kazi za mkataba wakati kiakidi huo sio muda wa wewe kukimbizana na vijana kufanya kazi. Niwapongeze wastaafu ambao walijiandaa kabla ya muda wao wa kustaafu na sasa wanakula kuku kwa mrija, hayo ndio maisha bwana!


DustBin
 
Upvote 4
hivi hio lump sum wanaopewa wastaafu hawezi ikagawanywa wakawa wanapewa kwa instalments ??? mfano wakapewa kiwango kile walichokua wanapata kwa mwezi, ama wakitaka mara mbili yake,iwe choice yao mara ngapi??
 
hivi hio lump sum wanaopewa wastaafu hawezi ikagawanywa wakawa wanapewa kwa instalments ??? mfano wakapewa kiwango kile walichokua wanapata kwa mwezi, ama wakitaka mara mbili yake,iwe choice yao mara ngapi??
Inawezekana kabisa.., lakini lilipojaribiwa kuwekwa ili mtu apewe asilimia kadha kisha zinazobaki apewe kidogo kidogo watu walikuja juu na kulalamika kuwa serikali inafanya unyanyasaji. Lakini lilikua wazo zuri sana kwa upande wa maslahi ya mstaafu
 
Mods waliupambania sana uzi wangu huu ila majaji waka udust bin
 
Watumizi unayoita mabaya ww yanasaidia uchumi kukuta mfano akimlipia pango kimada na kuwalewesha marafiki mwezi mzima ni mzunguko mkubwa sana mstaafu anakuwa amechangia kwenye uchumi
 
Back
Top Bottom