Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kina uhakika wa kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kutokana na kukubalika kwa wananchi na mikakati yake thabiti ya kufanikisha azma hiyo. Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa, alisema hayo jana, alipofungua semina elekezi ya Makatibu wa CCM wa wilaya na Makatibu wa Siasa na Uenezi wa wilaya za Kibaha Vijijini, Kibaha Mjini, Bagamoyo, Rufiji, Mkuranga, Mafia na Kisarawe, zilizoko mkoa wa Pwani. Semina hiyo ya watendaji wa Chama iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mkuu wa Mkoa, ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais unaotarajia kufanyika Oktoba 31, mwaka huu. Msekwa aliitaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa, mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2005/2010, mipango ya upatikanaji wa fedha za kampeni, uteuzi wa wagombea wanaokubalika, uzoefu wa uchaguzi katika mfumo wa vyama vingi vya siasa tangu mwaka 1961 na utaratibu wa kubadilisha mgombea wa urais kila baada ya miaka 10. Alisema CCM imejiwekea utaratibu wa wazi wa kukusanya fedha za gharama za uchaguzi, ikiwemo ununuzi wa vifaa (yakiwemo magari) kwa kuwashirikisha wanachama na wapenzi kuchangia kwa kutumia simu za mkononi na kuandaa hafla za kuchangisha fedha katika ngazi mbalimbali. Kuhusu utekelezaji wa Ilani, Msekwa alisema wana-CCM hawana budi kwenda kifua mbele kwa kuwa imefanikiwa kuzisimamia serikali kuitekeleza na kwamba, hakuna Mtanzania asiyefahamu hilo. Kutokana na mafanikio hayo, alisema CCM imeweka mikakati ya kuandaa na kuinadi kwa wananchi Ilani itakayotekelezeka kwa kipindi cha mwaka 2010/2015. Msekwa akizungumzia uteuzi wa wagombea katika nafasi mbalimbali, alisema kupanuliwa kwa demokrasia ndani ya Chama kwa kuruhusu wanachama wote kupiga kura za maoni kuwachagua wagombea, CCM ina uhakika kuwa, watachaguliwa wanachama wenye sifa za uongozi na wanaokubalika katika maeneo husika. Hata hivyo, aliwakumbusha wanachama, wapenzi wa CCM na wananchi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa wale ambao bado wana fursa ya kufanya hivyo, ili waweze kuwapigia kura wagombea watakaoteuliwa na Chama. Wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Msekwa alipata fursa ya kukagua madaftari ya wapiga kura wa CCM ya matawi mbalimbali yaliyoko wilaya za Kibaha Mjini na Kibaha Vijijini. Alitoa wito kwa wanachama ambao hawajajiorodhesha kufanya hivyo haraka, ili waweze kushiriki kupiga kura za maoni. Msekwa alitumia fursa hiyo kutoa ufafanuzi kuhusu kata mpya zaidi ya 700 zilizoongezwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Alisema uongozi wa kata zilizogawanywa utaratibu uchaguzi katika kata hizo, kazi ambayo inatakiwa ikamilike kabla ya kura za maoni.
Ushindi wa kishindo CCM lazima -Msekwa