SoC02 Ushirikishwaji, fursa za kilimo ni biashara

SoC02 Ushirikishwaji, fursa za kilimo ni biashara

Stories of Change - 2022 Competition

Mt09

Member
Joined
Sep 24, 2021
Posts
26
Reaction score
68
Mafanikio ya binadamu yeyote yanategemea namna anavyotumia maarifa katika kuyaendea yale anayoyaamini. Wakati maarifa yanaambatana na teknolojia iliyopo, Imani ni maono ya fikra za dini, falsafa ama itikadi. Kwa kuwa binadamu haishi pekee, bali ndani ya makundi yenye mamlaka na dhamana ya kumtawala kama vile serikali, basi mabadiliko yake yanatawaliwa na kanuni za kimfumo.

Kulingana na kanuni ya mabadiliko ya jamii, yapo mambo manne ya msingi yanayozingatiwa.

Sera, kuwepo kwa tamko la kimamlaka linaloainisha aina, kiwango, walengwa, mipango, rasilimali na muda kufikia mabadiliko kulingana na mahitaji ya jamii husika na ya wakati husika.

Hamasa kwa walengwa na wadau wa mabadiliko Ili kuwajengea Imani kuelekea mabadiliko na kuleta utayari wa kushiriki.

Uwezeshaji wa kimfumo na taasisi za kuelekeza teknolojia na fedha kutekeleza yale yaliyoaminiwa na jamii.
Pia kujenga mifumo mizuri ya kushirikisha walengwa Ili waweze kufikia na kushiriki fursa za mambo wanayoyaamini.

Ndio kusema mabadiliko chanya ya binadamu yanategemea na jinsi anavyowezeshwa kimfumo, kisheria na kiteknolojia kuyaendea yale anayoyaamini.

Tanzania kama jamii kitaifa, ilipitia mabadiliko ya kiuchumi miaka ya 80 na 90. Mabadiliko ambayo yalituwezesha kuachana na sera za kijamaa zilizodumu kuanzia mwaka (1967 - 1985) kutokana na Azimio la Arusha chini ya mwasisi wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kufuata sera za soko huria. Hali hiyo ilitokana na kushindwa kwa falsafa za kijamaa duniani na kushamiri kwa utandawazi.

Katika kufufua uchumi uliodorora, shirima la fedha la kimataifa IMF liliweka sera mpya ya mikopo ikiwemo mkopaji kubinafsisha shughuli za kiuchumi na kibiashara. Hivyo katika kuweka mazingira wezeshi ya kibiashara, serikali ya awamu ya pili (1985 -1995) ililegeza masharti ya biashara maarufu Kama "Ruksa". Miongoni mwa madiliko hayo ilikuwa kufungua mipaka Ili kuruhusu bidhaa kuingia nchini.

Jingine lilihusu misamaha ya Kodi na ushuru kwa muda wa miaka mitano kwa wawekezaji wakubwa wanaoanza kuwekeza nchini. Hii baadae ilifuatiwa na Azimio la Zanzibar la mwaka 1992 lililoruhusu watumishi viongozi wa umma kuwa na hisa katika makampuni binafsi hali iliyopigilia msumari sera ya ubinafsishaji.

Ukitazama hali hiyo utaona walengwa walikuwa wafanyabiashara wakubwa waliokuwa na mitaji na teknolojia mpya hususani kutoka nje ya nchi. Hata hivyo mabadiliko hayo yalisababisha vijana wengi kubadili shughuli za kiuchumi kutoka kilimo na kufanya biashara ndogondogo maarufu Kama machinga. Kwa kuwa hawakuwa maarifa ya biashara wengi waliishia kufanya utapeli maarufu Kama kanyaboya. Mifumo na teknolojia dhaifu ya kukusanya kodi, iliruhusu ukwepaji Kodi kiasi taasisi za fedha za kimataifa kupoteza Imani na serikali ya Tanzania.

Mfano mwingine wa mabadiliko ni pale serikali ya awamu ya tatu (1995 - 2005), ilipofanya maboresho ya kiuchumi. Uuzwaji wa mashirika ya umma kwa wawekezaji wakubwa kutoka nje kulisaidia kuingia kwa teknolojia mpya pamoja na mitaji kwa mashirika hayo. Maboresho hayo yalileta tija na ufanisi katika utoaji wa huduma Bora na za uhakika, mfano huduma za mashine za kutolea fedha ATM mitaani.

Pia maboresho katika mfumo wa makusanyo ya kodi ambapo mamlaka ya mapato Tanzania yaliyoanzishwa ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa misamaha ya Kodi. Sambamba na hayo ni mfumo mpya wa Kodi kupitia ongezeko la bei ya bidhaa yaani VAT kwa sheria ya bunge ya mwaka 1997. Mafanikio katika ukusanyaji mapato kutokana na mabadiliko hayo kulisaidia kurejesha Mahusiano yaliyofifia baina ya serikali na IMF kiasi cha kusamehewa kiwango kikubwa cha deni letu la nje.

Hata hivyo hapakuwa na mkakati wa kuweka mfumo wa kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wadogo kiuchumi zaidi ya kuambiwa kuwa "Mtaji wa Masikini ni Nguvu Zake Mwenyewe".

Katika awamu ya nne ya uongozi (2005 - 2015), mikakati ya MKUKUTA na MKURABITA iliyolenga kuinua uchumi na hali za wananchi ilifanya mabadiliko makubwa. Kwa mfano mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji mapato kupitia mashine za EFD kuliimarisha makusanyo ya serikali. Takwimu za TRA zinasema mapato yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 177 kwa mwezi mwaka 2005/2006 hadi kufikia shilingi bilioni 390 kwa mwezi mwaka 2009/2010.

Hii ilijenga uwezo wa serikali kutekeleza miradi ya kimkakati kama ujenzi wa barabara, shule,mingine ya kusaidia kuinua uchumi.

Kupitia MKURABITA, serikali ya awamu ya nne (2005 - 2015) ililenga rasmi kuwainua kiuchumi wafanyabiashara wa kati na wadogo wadogo kwa Kurasmisha kisheria rasilimali na biashara zao. Kupitia taasisi za BRELA na COSOTA, usajili wa makampuni na biashara pamoja na umiliki wa bunifu mbalimbali zilipewa hati za kisheria.

Hati hizi ziliwawezesha kufanya mikataba mbalimbali ya biashara kama vile upatikanaji mitaji, teknolojia na masoko na kukua kiuchumi. Mfano kupitia mitandao ya kijamii, wabunifu na wasanii wa tasnia za filamu, muziki na matangazo wameweza kupata na wanaendelea kunufaika na soko la mtandaoni.

Katika awamu ya tano (2015 - 2021), mabadiliko katika usimamizi wa fedha za serikali kupitia mfumo wa kielektroniki wa kufuatilia mwenendo wa miamala ya serikali ELPICA, kulisaidia kuzuia matumizi holela yasyokuwa na tija. Kutokana na udhibiti huo serikali iliweza kujenga uwezo wa kuanzisha miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere.

Katika awamu ya tano pia umefanyika urasmishaji sekta ya machinga kwa njia ya vitambulisho vya mlipa kodi. Kupitia mfumo huo ambao ni utekelezaji wa MKURABITA wamachinga wameanza kushirikishwa fursa zinazotolewa na serikali ikiwemo kupatiwa maeneo rasmi ya kibiashara. Huo ni mfumo wa ushirikishwaji fursa za kibiashara kwa machinga unaotekelezwa na awamu hii ya sita ya uongozi wa nchi.

Pamoja na ushirikishaji huo kwa machinga, serikali ya awamu ya sita pia imebuni mfumo wa kiteknolojia wa kukusanya nguvu za wananchi katika kuchangia shughuli za maendeleo ya jamii. Mfumo huo ujulikanao kama "tozo ya uzalendo" inalenga kuongeza tija katika miradi ya jamii.

Kufuatia mafanikio makubwa yaliyotokea kwenye sekta ya fedha na sekta ya biashara, serikali imeamua kuelekeza nguvu katika sekta ya kilimo. Kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023, serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 900 kutoka shilingi bilioni 294.1 zilizotengwa mwaka 2021/2022. Lengo ni kuibadilisha kilimo toka shughuli ya kubahatisha kuwa shughuli ya kibiashara kwa kuongeza matumizi ya sayansi na teknolojia pamoja na kujenga mifumo mizuri ya kibiashara. Ajenda hii ya 1030 yenye kaulimbiu ya "kilimo ni biashara" inakusudia pamoja na mambo mengine, Kutengeneza fursa mpya za ajira kwa vijana ambao ni nguvu kazi muhimu kwa uchumi.


USHAURI KWA SERIKALI
Kwa kuwa ajenda hii ni ya kitaifa, mfumo wa ushirikishwaji fursa hii uzingatie uwazi na usawa kwa wote. Mfumo uwe na tovuti yenye maelezo kuhusu mambo yote ya kimkataba ikiwa na dirisha la kujisajili. Lengo ni kuwezesha watu wote kuwa na uwezo wa kufikia fursa hii moja kwa moja bila usumbufu ama kudanganywa na matapeli, lakini vilevile kuzuia rushwa na upendeleo.

Pia serikali ijenge uwezo wa vijiji kisheria, kiteknolojia na kifedha katika kuanzisha miradi hii ya kilimo ni biashara. Kupitia makusanyo ya "kodi ya uzalendo" vijiji viwezeshwe kuandaa miundombinu husika na mazingira wezeshi. Lengo ni kupanua wigo wa fursa hii Ili watanzania wengi hususani vijana wasio na ajira na mitaji waweze kushiriki.​
 
Upvote 0
Back
Top Bottom