Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
TAMKO KUHUSU UKIUKWAJI WA KATIBA YA JAMUHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA ULIOFANYWA NA SPIKA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Ndugu Waandishi wa Habari,
Awali ya yote niwashukuru na kuwapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya hasa wakati huu ambapo dunia inaendelea kupambana na janga la virusi vya Corona (COVID 19). Sisi watetezi wa haki za binadamu tunapenda kuwatia moyo muendelee na kazi ya kutuhabarisha lakini bila kusahau kuchukua tahadhari za kutosha kujikinga na ugonjwa huu.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Shirika la Elimu ya Uraia na Msaada wa Sheria (CILAO) limesikitishwa na kitendo cha Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya maamuzi yanayokiuka misingi ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Itakumbukwa kwamba Bunge la Jamuhuri ya muungano wa Tanzania na Vyama vya siasa vinaongozwa kwa mujibu wa Katiba na sharia zingine za nchi. Ibara ya 71 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza wazi kuhusu ukomo wa mtu kuwa Mbunge. Kwa mujibu wa Ibara ya 71(1)(e) ya Katiba ni wazi kuwa Mbunge atapoteza nafasi yake ya ubunge ikiwa atapoteza uanachama wa chama chake kilichompatia ubunge wakati wa uchaguzi.
Mnamo tarehe 6 Mei 2020, Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Job Ndugai, aliruhusu, aliyekua mbunge wa Ndanda, Bwana Cecil Mwambe ambaye aliishajiuzulu nafasi yake ya ubunge aendelee na kazi hiyo. Bwana Mwambe aliishaonekana katika vyombo vya habari akitangaza kujivua uanachama wa CHADEMA na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Kwa kuwa Cecil Mwambe alitangaza kijiondoa CHADEMA basi tunaamini pasipo shaka kwamba alipoteza tayari sifa ya kuendelea kuwa Mbunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kitendo cha Spika kumruhusu kuendelea kuwa Mbunge ni ukiukwaji wa Katiba ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania na kwa kuwa Katiba inatamka wazi katika Ibara ya 26(1) kuwa kila RAIA ana wajibu wa kusimamia na kutetea Katiba na Sheria, sisi kama Taasisi kwa kushirikiana na wadau wengine tunakusudia haraka iwezekanavyo kufungua kesi Mahakama Kuu kuomba ufafanuzi wa Mahakama kuhusu kitendo hiki cha Spika.
Imetolewa leo tarehe 9 Mei 2020,
Na,
Odero Odero,
Mkurugenzi,
Civic and Legal Aid Organisation (CILAO)