Usijiue kwa sababu ya hasara ya pesa au kukimbiwa na mpenzi

Usijiue kwa sababu ya hasara ya pesa au kukimbiwa na mpenzi

Jumanne Mwita

JF-Expert Member
Joined
Nov 18, 2014
Posts
530
Reaction score
1,446

Usijiue kwa sababu ya hasara ya pesa au kukimbiwa na mpenzi

Maisha ni safari yenye milima na mabonde. Kila mmoja wetu hukutana na changamoto tofauti, lakini hakuna sababu yoyote inayostahili kuchukuliwa kama mwisho wa kila kitu. Kupoteza pesa, kazi, biashara, au hata mpenzi ni mambo yanayoumiza, lakini si sababu ya kukata tamaa wala kujidhuru.

Leo hii, kuna kijana mtaani ambaye amepoteza maisha kwa sababu kaibiwa milioni mbili! Dogo amejinyonga, sijui kwa nini alichukua maamuzi magumu hivi. Hela zinatafutwa, zingeweza kupatikana nyingine, lakini uhai hauwezi kurudi.

Nakubali kabisa – pesa ni ngumu, maisha yanabana, na mambo si rahisi. Lakini maisha yako ni ya thamani zaidi kuliko pesa au mahusiano. Uhai wako ni wa kipekee, na kila changamoto unayopitia inaweza kushughulikiwa ukiwa hai. Ukijitoa uhai, hakuna nafasi ya pili.

USHUHUDA WANGU

Mwaka 2017 hadi 2019, nilikuwa mwanzilishi na mkurugenzi wa kampuni X mkoa flani. Nilihangaika na kuwekeza muda na nguvu, lakini mambo yakavurugika hadi ikabidi nifunge kampuni. Nilijikuta nimerudi kuajiriwa, jambo ambalo sikuwahi kufikiria. Ila sikuruhusu mawazo mabaya yanitawale – sikuwahi kufikiria kujiua wala kuona kwamba maisha yamefika mwisho. Nilijua ninaweza kuanza Upya na mambo yakaenda sawa ila siyo kufikiria kujiua.

Nikaanza moja, nikaweka akiba kidogo kidogo, na leo hii, hata kama sijafanikisha kila kitu, ninafuraha kwa sababu nilithamini uhai wangu kuliko pesa. Nisingeweza kusimama tena kama ningekuwa mtu wa mawazo mabaya au visasi. Watu wengi wamenidhurumu na kunitapeli, lakini sikuweka chuki moyoni. Najua mwenye haki siku zote hupata chake, na hata asiye na haki hujuta baada ya muda.

UJUMBE KWA VIJANA

Ikiwa unapitia changamoto yoyote – iwe ni kufilisika, kuachwa na mpenzi, au kushindwa kimaisha – tafadhali kumbuka haya:
  • Pesa zinatafutwa, lakini uhai hauna mbadala.
  • Mpenzi anaweza kuondoka, lakini mapenzi hayajaisha duniani.
  • Changamoto yoyote ina suluhisho, ilimradi uko hai.
  • Hakuna mtu aliyefanikiwa bila kupitia magumu.
Jipe moyo. Anza upya. Omba msaada kwa marafiki au familia ikiwa unahisi umelemewa. Hakuna tatizo lisilo na suluhisho, ila kifo hakina marekebisho.

Thamini maisha yako – ndiyo mtaji mkubwa zaidi ulionao!
 
Back
Top Bottom