Usikose vifaa hivi nyumbani kwako!

Usikose vifaa hivi nyumbani kwako!

Samahani

JF-Expert Member
Joined
Oct 29, 2018
Posts
221
Reaction score
335
Siku za karibuni, nikiwa likizo, nilimtembelea ndugu yangu mmoja ambaye aliugua kwa muda mrefu na sikuwa nimepata nafasi ya kumtembelea. Wakati tunazungumza, kuna jirani yake alikuja na kuomba kuazimwa jembe ili akaoteshe mche wa mti aliokuwa ameununua huko alikotoka.

Cha kushangaza, hata huyu ndugu yangu naye hakuwa na jembe. Jirani yule akaendelea nyumba za mbele zaidi kulisaka jembe. Hii iliniwazisha jambo fulani.Pamoja na ukweli kuwa tunapoishi mitaani tunashirikiana na kuazimana vifaa mbalimbali, naamini kuwa kila familia, au hata mtu binafsi, kuna baadhi ya vifaa na vitendeakazi ni muhimu sana kwenye matumizi ya kila siku.

Vitendeakazi hivi, kimsingi, vinasaidia katika kurahisisha kazi mbalimbali tunazozikabili kila siku, na kipekee pia, zinatuwezesha kupunguza baadhi ya gharama zisizo za lazima tunapokabiliana na kazi hizi. Vifaa hivi vinarashisisha kazi mbalimbali kama vile marekebisho mbalimbali nyumbani, ulinzi na usalama, kilimo na nyinginezo.Hivi ni pamoja na;

1. Panga na Msumeno

Panga linasaidia sana katika shughuli mbalimbali za kukata, kucharanga, kupasua na hata kujihami na hatari mbalimbali. Msumeno ni wa muhimu kwa shughuli mbalimbali kama vile kukata mbao, vipande vya bomba na vinginevyo.

2. Jembe

Kazi za jembe ni nyingi sana kila siku na zinafahamika. Hakika sio sahihi kwa nyumba kukosa kifaa hiki muhimu

3. Reki/ Rato

Usafi wa mazingira, uzoaji wa taka ngumu na hata shughuli za bustani zinafanyika kwa wepesi sana ikiwa unakuwa na vifaa hivi.

4. Nyundo
Marekebisho mbalimbali yanayohusu kugongelea au kung’oa misumari yanahitaji uwepo wa nyundo, na hakika sio vema kuikosa nyumbani.

5. Tochi
Miaka ya hivi karibuni, wengi sana tumeacha kabisa kumiliki kifaa hiki, pengine kwa kuwa simu zetu siku hizi zina tochi pia. Lakini naamini kuwa, tochi ni kifaa muhimu mno kuwa nacho nyumbani na hata tunapoenda safarini. Zipo tochi ndogo na zenye nguvu kubwa tunaweza hata kutembea nazo nyakati za usiku

6. Bisibisi/ Screw Driver/ Tester
Hiki ni kifaa kingine muhimu sana. Kuna wakati tunahitaji kufungua baadhi ya vitu kwaajili ya marekebisho, na sio lazima kuwatafuta mafundi au wataalamu wakubwa ili kufanikisha hili. Kwa mfano, kama ‘screw’ ya kitasa imelegea, unaweza tu kuikaza ukiwa na mojawapo kati ya kifaa hiki.

7. Balbu za akiba
Inapotokea balbu imeungua, ni vema kuwa na balbu ya akiba ili kubadilisha. Sio busara hata kidogo kuanza kumtafuta fundi wa umeme ili akubadilishie balbu ya hadi chumbani kwako!!! Ni jambo ambalo ni rahisi tu kujifunza na kulifanya mwenyewe.

8. Koleo/ Beleshi
Hili nalo linasaidia wakati wa ujenzi na marekebisho madogomadogo, usafi wa mazingira na hata shughuli za ufugaji

9. Viatu vigumu (Gumboots) & Gloves
Hizi nazo zina umuhimu mkubwa sana ukiwa nyumbani ili kujikinga na hatari mbalimbali katika miguu na mikono hasa katika shughuli za usafi, kilimo au ufugaji

10. Ngazi
Tunaihitaji ngazi katika kupanda na kushika katika vimo na vina tusivyoweza kufika kirahisi. Hata pale tunapowaleta mafundi majumbani kwetu kwaajili ya ujenzi au marekebisho, kuna wakati wanahitaji ngazi. Ngazi sio kitu cha kukosa nyumbani kwako, na gharama zake sio kubwa.

11. Pipa la taka (Dustbin)
Ingawa wengi tumezoea kuwa na mashimo ya taka, lakini kwa mazingira ambayo tunaishi siku hizi, hasa katika nyumba za kupanga katika miji na majiji makubwa, ni busara kuwa na pipa maalumu la taka, ili kuepuka kuzagaa ovyo kwa taka.

12. Pasi

Unadhifu wa mavazi ni muhimu kwa kila mtu. Ni vizuri kuwa na pasi, tena inapobidi, uwe na zaidi ya pasi inayotumia nishati moja. Mathalani, siku hizi wengi tumezisahau kabisa pasi za mkaa. Lakini kwa kuwa umeme wetu sio wa uhakika, ni busara kuwa na hata pasi ya mkaa ili inapotokea uhaba wa umeme, bado tubaki na umaridadi wetu.

13. Fimbo
Kwa watu wa mijini, sio rahisi sana kukuta mtu akiwa anamiliki bakora ndani. Lakini ni wazi kuwa, fimbo nzuri na ngumu ni muhimu kuwa nayo nyumbani. Tunapovamiwa na maadui au wadudu wa hatari kama nyoka, bila uwepo wa fimbo tunaweza kujikuta katika wakati mgumu zaidi kujilinda na kujiokoa

Si rahisi kwakweli kuvitaja vitu vyote muhimu kwa maisha ya kila siku. Bado orodha ni ndefu MNO. Hapa sijazungumzia Kinu pamoja na mtwangio, Kamba ya manila au kudu, waya mgumu, vipande vya mbao, tindo, sururu, shoka, fagio gumu, ndoo tupu za dharura na vingine vingi.

Ingawa kwa wengi, huwa tunavipuuza, lakini matokeo yake ni kuwa, kila siku tunajikuta tukikwama katika shughuli zetu za muhimu, au tukilazimika kuzurura ovyo kuvitafuta au kuviazima kwa majirani.

Unapoona kifaa unakiazima mara kwa mara kwa matumizi yako, na kipo ndani ya uwezo wako kukimiliki, kimiliki ili usiendelee kukwama zaidi.

Wasalaam,

SAMAHANI

+255 763 305 605
 
Inategemea unaishi wapi,

Na mazingira yapi,mpangaji wa chumba kimoja hawezi miliki hata jembe ndani,

Majirani wengine wakiazima kifaa wakimaliza kazi hawarudishi na mwisho kupotza,



NB, ninapo lala chini ya uvungu wa kitanda nimeweka upanga, umeelewa
 
Hiyo simu kwa ajili ya nini mkuu?

Au kuna ka msaada cha pesa ya kununua vifaa tajwa?
Simu ipi tena mkuu? Lengo ni kuainisha vifaa ambavyo kiuzoefu, ukiwa navyo kuna baadhi ya shughuli zinakuwa rahisi
 
Inategemea unaishi wapi,

Na mazingira yapi,mpangaji wa chumba kimoja hawezi miliki hata jembe ndani,

Majirani wengine wakiazima kifaa wakimaliza kazi hawarudishi na mwisho kupotza,



NB, ninapo lala chini ya uvungu wa kitanda nimeweka upanga, umeelewa
Nzuri sana hii... Hata mkijichanga wapangaji mkanunua kwa pamoja baadhi ya hivi pia ni nzuri
 
Back
Top Bottom