Usimamizi wa Rasilimali za Misitu Tanganyika: Nani Anawajibika?

Usimamizi wa Rasilimali za Misitu Tanganyika: Nani Anawajibika?

UTPC

Journalists' Union
Joined
Apr 17, 2026
Posts
51
Reaction score
38
WhatsApp Image 2026-05-22 at 14.10.14.jpeg
Katika makala iliyopita, uchunguzi huu uliibua hatari inayolikabili eneo la Tanganyika mkoani Katavi, ukataji wa miti ovyo unaotishia si mazingira pekee, bali pia mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 29 yatokanayo na biashara ya kaboni.

Lakini nyuma ya miti inayokatwa na mashamba yanayopanuka ndani ya misitu, kuna swali la msingi zaidi, nani anawajibika kulinda rasilimali hizi, na kwa kiwango gani?

Je, tatizo ni wananchi pekee, au kuna udhaifu ndani ya mfumo wa usimamizi?

Mfumo wa kisheria
Kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002, vijiji vina mamlaka ya kuanzisha na kusimamia misitu ya vijiji kupitia Kamati za Maliasili. Kamati hizi zinapaswa kusimamia matumizi ya ardhi, kuzuia uvamizi na kuratibu doria.

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 inaongeza wajibu wa ngazi ya kata na wilaya kuhakikisha sera za uhifadhi zinatekelezwa. Katika ngazi ya wilaya, Afisa Misitu na Afisa Mazingira wanawajibika kusimamia utekelezaji huo, huku Baraza la Madiwani likiwa chombo cha maamuzi na ufuatiliaji wa sera.

Kwenye makaratasi, mfumo unaonekana thabiti, lakini je, unafanya kazi kama ulivyokusudiwa?

Kamati za maliasili
Katika baadhi ya vijiji vilivyotembelewa, wananchi walisema Kamati za Maliasili zipo, lakini hazifanyi kazi kikamilifu.

Charles Maembe, Mwenyekiti wa Kijiji cha Bujombe, anasema changamoto ipo kwenye muundo wa kamati na maslahi yanayogongana. “Ili kuondoa mgongano wa maslahi binafsi inabidi tuhuishe upya hizi kamati za maliasili kwani hawa vijana wetu wamekuwa na marafiki huko msituni wanaovamia, wanapeleka ng’ombe, wanalima kwa sababu ya kuwa wenyeji. Tukihuisha hizi kamati kila baada ya muda fulani hata kwa miezi mitatu mitatu itasaidia kupunguza tatizo hili kwa kiasi kikubwa,” alisema.

Kauli hiyo inaonesha kuwa changamoto si ukosefu wa sheria, bali ni utekelezaji na nidhamu ya ndani.

Ngazi ya kata na wilaya
Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Joseph Bisura, anasema halmashauri imekuwa ikiendesha doria na kutoa elimu kwa jamii, lakini eneo la wilaya ni kubwa na rasilimali ni chache.

“Tunafanya doria mara kwa mara, lakini wakati mwingine maeneo ni makubwa na yanafikika kwa ugumu,” alisema.

Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kuwa baadhi ya wananchi wanaona doria hizo hazitoshi au hazifiki katika maeneo ya ndani zaidi ambako uvamizi hufanyika.

Kwa mujibu wa taarifa za halmashauri, mwaka 2025 pekee maonyo kadhaa yalitolewa kwa watendaji wa kata kutokana na udhaifu wa usimamizi wa mazingira. Hii inaashiria kuwa hata ndani ya mfumo wa serikali, uwajibikaji bado ni changamoto.
photo_2026-07-21_14-48-53.jpg

photo_2026-07-21_14-48-51.jpg
Biashara ya Mkaa chanzo kikuu cha uharibifu
Moja ya sababu kubwa zinazochochea ukataji wa miti ovyo ni biashara ya mkaa. Katika baadhi vijiji vya Tanganyika, mkaa umegeuka kuwa chanzo kikuu cha kipato kwa wananchi wasiokuwa na ajira rasmi.

Uchunguzi unaonyesha kuwa mkaa unaozalishwa Tanganyika husafirishwa kwenda mikoa mbalimbali kama Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Dar Es Salaam. Hii imeifanya misitu ya wilaya hii kuwa kama mgodi unaochimbwa bila mpango.

Kwa mujibu wa Afisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Wilaya ya Tanganyika, Bruno Mwaisaka, biashara ya mkaa ni miongoni mwa shughuli zinazoharibu misitu kwa kasi kubwa.

“Ukataji wa miti ovyo unasukumwa zaidi na biashara ya mkaa na uhitaji wa ardhi ya kilimo. Tuna maeneo makubwa ya misitu lakini rasilimali za usimamizi ni ndogo,” alisema Mwaisaka.

Anabainisha kuwa idara yake ina upungufu mkubwa wa wataalamu wa sekta za uhifadhi, ambapo wana wataalamu 20 pekee kati ya 50 wanaohitajika, hali inayofanya usimamizi wa maeneo makubwa ya misitu kuwa mgumu.

Kutokana na upungufu huo wamekuwa wakishirikiana na vyombo vingine vya serikali kama Jeshi na Polisi,Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Wilaya ya Tanganyika na askari wa Hifadhi ya Taifa (TANAPA) Mkoa wa Katavi, katika doria mbalimbali, kwa lengo la kudhibiti uvamizi kwenye maeneo ya misitu ya hifadhi.

Kilimo: Upanuzi bila mipango
Sababu nyingine kubwa ni upanuzi wa shughuli za kilimo bila kuzingatia mbinu bora za kilimo, kadri idadi ya watu inavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya chakula na kipato yanavyoongezeka.

Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Philemon Mwita, anaeleza kuwa ardhi nyingi inayolimwa kwa muda mrefu imepoteza rutuba.

“Wakulima wengi wanalazimika kufungua mashamba mapya kwa kukata misitu kwa sababu ardhi imechoka na elimu ya kilimo endelevu bado haijawafikia wote,” alisema Mwita.

Uchunguzi unaonyesha kuwa uchache wa maafisa ugani ukilinganishwa na ongezeko kubwa la wakazi umechangia wakulima kuendelea kutumia mbinu za zamani zinazoharibu ardhi na kulazimisha uvamizi wa misitu.

‘‘Kama halmashauri tunajitahidi kutoa elimu ya matumizi bora ya ardhi kwa kulima mazao ambayo yanaendana na eneo husika kwa kuchanganya mazao, kwa mfano unaweza kuchanganya maharage au mikunde kwenye mazao mbalimbali kwa ajili ya kurutubisha ardhi.’’ aliongeza

Ufugaji: Faida kubwa, adhabu ndogo
Kwa upande wa wafugaji, misitu imekuwa eneo muhimu la malisho, hasa wakati wa kiangazi. Hata hivyo, shughuli hizi zimekuwa zikifanyika hata ndani ya maeneo ya hifadhi.

Bruno Mwaisaka anaeleza kuwa baadhi ya wafugaji hawaogopi faini wanazotozwa.

“Wafugaji pindi tunapowakamata kwa kuingiza mifugo yao maeneo ya hifadhi na kuwatoza faini wanaamini wanapata faida zaidi kuliko faini wanayotoa. Mfugaji mwenye ng’ombe 2000 anaona faida anayoipata ni kubwa kuliko anacholipa kama adhabu,” alisema.

Hali hii inaonyesha kuwa adhabu zilizopo hazisababishi maumivu kwa mkosaji, hivyo kushindwa kuwa kikwazo cha uvamizi wa misitu.

Shinikizo la kiuchumi na uwajibikaji wa pamoja
Mwaisaka, anasema ni vigumu kuzungumzia uwajibikaji bila kuangalia hali ya uchumi wa wananchi.

“Ukipata mkulima anayevuna gunia tatu au nne kwa nusu heka, atafikiria kuongeza eneo badala ya kuongeza tija, hapo ndipo misitu inaingia hatarini,” alisema.

Kwa mantiki hiyo, uwajibikaji hauwezi kuwa wa viongozi pekee, ni mnyororo unaohusisha Kamati za Maliasili za Vijiji, Watendaji wa Kata, Maafisa wa Wilaya, Baraza la Madiwani na wananchi wenyewe. Udhaifu katika kiungo kimoja tu unaweza kuvuruga mfumo mzima.

Utekelezaji wa sheria ni changamoto kubwa
Kwa mujibu wa Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Tanganyika, Joseph Bisura, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 ipo wazi kuhusu wajibu wa kulinda mazingira, lakini changamoto iko kwenye utekelezaji.

“Uelewa mdogo wa wananchi kuhusu mabadiliko ya tabianchi na wakati mwingine ushirikiano hafifu kutoka ngazi za chini hufanya udhibiti wa ukataji wa miti kuwa mgumu,” alisema Bisura.

Anabainisha kuwa katika bajeti ya mwaka 2025/26, Halmashauri imetumia zaidi ya shilingi milioni 572 kwa ajili ya shughuli za uhifadhi wa mazingira, ikiwemo doria, elimu kwa wananchi na miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, alisema wanaendelea na kutoa elimu za mara kwa mara juu ya usafi na utunzaji wa mazingira katika kila mikutano ya vitongoji,vijiji na hata kata ili elimu hiyo iweze kuwafikia wananchi wote akisisitiza kuwa bila ushiriki wa jamii, juhudi za serikali pekee haziwezi kumaliza tatizo hilo.

Uvamizi wa maeneo tengefu na maslahi binafsi
Uchunguzi unaonyesha kuwa baadhi ya maeneo nyeti kama vyanzo vya maji na misitu ya hifadhi yameendelea kuvamiwa kwa shughuli haramu, zikiwemo uchimbaji mdogo wa madini na kilimo cha bangi.

Bisura anatoa mfano wa Kijiji cha Katuma, “Kwenye kingo za mto Katuma ambazo ni hifadhi ya msitu wa kijiji, lakini mara kwa mara tunakamata watu wakichimba madini, hata tukiwakamata, wanarudi tena,” alisema.

Hali hii inaashiria kuwepo kwa maslahi binafsi, ukaidi wa sheria na wakati mwingine ushawishi unaokwamisha utekelezaji wa maamuzi.

Je, Mfumo unahitaji marekebisho?
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tanganyika, Hamad Mapengo, anasema Baraza la Madiwani limepitisha maazimio kadhaa ya kuimarisha uhifadhi, lakini amesema kuwa usimamizi wa ngazi za chini bado unahitaji kuimarishwa. “Sheria zipo, lakini utekelezaji wake ndio changamoto,” alisema.

Uchunguzi huu unaonyesha kuwa pengo lililopo si kati ya sheria na wananchi pekee, bali pia kati ya maamuzi ya juu na utekelezaji wa chini.

Hitimisho
Tanganyika ina mifumo ya kisheria, taasisi za usimamizi na miradi ya kimataifa ya uhifadhi, lakini ufanisi wake unategemea uwajibikaji wa kila ngazi. Bila uwazi, ufuatiliaji na nidhamu ya pamoja, hata miradi yenye kuingiza mabilioni inaweza kuyeyuka.

ANDIKO LA: Swaum Katambo – Tanganyika
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.
 
Back
Top Bottom