SoC04 Usimamizi wa taka na usafi wa mazingira: Changamoto na suluhisho la kudumu

Tanzania Tuitakayo competition threads
Joined
Nov 23, 2022
Posts
57
Reaction score
64
Tarehe tano (5) mwezi juni kila mwaka, dunia huadhimisha siku ya mazingira ikiwa lengo lake ni kuleta pamoja mamilioni ya watu duniani kote na kuwashirikisha kwenye jitihada za kutunza na kuboresha Dunia kupitia mazingira yao. Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani huchukulia umuhimu siku hiyo kwa kuweka msisitizo kwa sekta za umma, mashirika na watu binafsi kushiriki katika utunzaji wa mazingira.

Licha ya jitihada zote, Tanzania bado inakabiliwa na changamoto za kiuchumi, kijamii na kimazingira zinazotokana na usimamizi duni wa taka na usafi wa mazingira. Hata hivyo, bado ipo nafasi ya kubwa ya kuleta mabadiliko chanya kwa kutekeleza mikakati Madhubuti katika usimamizi wa taka ili kujenga utamaduni wa usafi wa mazingira katika jamii ya Watanzania.

CHANGAMOTO.
Nchini Tanzania, suala la usimamizi wa taka na usafi wa mazingira limekuwa na changamoto kubwa, zifuatazo ni baadhi ya changamoto zitokanazo na usimamizi duni wa taka na ukosefu wa utamaduni wa usafi wa mazingira nchini Tanzania.

Kwanza kabisa, usimamizi duni wa taka katika maeneo ya masoko na makazi ya watu ni changamoto kubwa. Masoko mengi hayana miundombinu madhubuti ya kukusanya na kusafirisha taka, hivyo kusababisha taka kujaa mitaani na kuhatarisha afya ya umma. Kwa upande mwingine, ukosefu wa magari maalumu ya kuzolea taka unafanya ukusanyaji wa taka kuwa mgumu na wa kusuasua.


kielelezo 1; Usimamizi duni wa taka katika makazi ya watu​

Aidha, uwepo wa maeneo ya kutupa taka karibu na mazingira ya watu husababisha chafe wa mazingira na kuongeza hatari za magonjwa. Maeneo ya kutupa taka ni mazingira mazuri kwa kuzaliana kwa vimelea hatari kama vile bakteria, na virusi. Hii inaweza kuleta mlipuko wa magonjwa kama vile kipindupinu, pamoja na magonjwa mengine ya kuambukiza.


kielelezo 2; Uwepo wa maeneo ya kutupa taka karibu na makazi ya watu​

Pamoja na hayo, ukosefu wa elimu katika jamii pamoja na ushiriki duni wa jamii katika suala la usafi wa mazingira ni changamoto nyingine. Wananchi wengi hawana elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira safi na jinsi wanavyoweza kushiriki katika mchakato wa usimamizi wa taka.

SULUHISHO.
Ili kutatua changamoto hizi, suluhisho la kudumu linahitaji hatua mbalimbali kama ifuatavyo;

Kwanza, elimu kwa umma inapaswa kutiliwa mkazo, ambapo njia bora ni kuanzisha programu za elimu katika shule ili kuwaandaa watoto na wanafunzi waliopo shule za msingi na sekondari ili wawe mabalozi wazuri katika usimamizi wa taka na usafi wa mazingira. Programu hizi zianze kutekelezwa kuanzia mashuleni ili kujenga mtazamo chanya miongoni mwa wanafunzi kuhusu usafi wa mazingira. Hii itawaandaa kuwa mabalozi bora wa usafi mazingira katika jamii zao. Pia elimu ya usafi wa mazingira itolewe kupitia nyumba za ibada. Hii itawezesha kueneza ufahamu kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika kutunza mazingira.


kielelezo 3; Picha katika shule ya msingi Mazimbu A mkoani Morogoro ikionesha kampeni ya utunzaji wa mazingira mashuleni.​

Pili, ni muhimu kuweka vatu vya kuhifadhi taka mbali na makazi ya watu ili kuzuia uchafuzi wa mazingira na kuhatarisha afya ya umma.

Tatu, serikali inapaswa kutunga sera madhubuti za usimamizi wa taka na kuzitekeleza kikamilifu ili kupunguza athari za taka kwa mazingira na afya ya umma. Serikali itunge kanuni kali za kudhibiti uchafuzi wa mazingira na utupaji wa taka ovyo ikiwa ni pamoja na kuweka adhabu kwa kila anayekiuka kanuni hizo. Mfano, kwa upande wa vijijini kila kaya iwe na eneo maalumu la kutupa taka. Kwa upande wa mijini, kila mwenye biashara atenge vifaa maalumu vya kuhifadhia taka zinazozalishwa katika shughuli zao.

Kwa upande mwingine, matumizi ya mwenge wa uhuru kwa muda wa miaka mitano ijayo yanaweza kuwa na manufaa kwa kuanzisha kampeni maalumu ya kuhimiza usafi wa mazingira, ikiwa na kaulimbiu maalumu itakayowahamasisha wananchi kuchukua hatua za kudumisha usafi na utunzaji wa mazingira. Kila mwaka katika mbio za mwenge iwepo kaulimbiu maalumu yenye ujumbe unaohamasisha jamii kuchukua hatua za usafi na utunzaji wa mazingira. Sambamba na hilo, mwenge wa uhuru unaweza kutumika kutoa elimu kwa umma kuhusu sera na kanuni za kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kuhimiza hatua za kuchukua katika usafi wa mazingira kwa faida ya vizazi vijavyo.

Aidha, serikali iandae wiki ya mazingira kitaifa ambayo kilele chake itakuwa ni juni 5 ya kila mwaka (siku ya mazingira duniani). Wiki hii ya mazingira kitaifa inaweza kujumuisha shughuli mbalimbali ikiwemo elimu kwa umma kuhusu usimamizi wa taka na ushiriki wa jamii katika usafi wa mazingira. Katika wiki hii, wadau mbalimbali wa mazingira watoe semina maalumu za usafi wa mazingira ikiwa ni pamoja na maonesho kupitia maeneo ya umma na vyombo vya habari. Hii itasaidia kujenga utamaduni wa usafi wa mazingira kwa watazania.

Serikali iweke utaratibu maalumu wa kuwawezesha wanaokusanya taka za plastiki mtaani kama vile kuweka miundombinu ya uchakataji wa taka za plastiki ili kutengeneza bidhaa mpya. Hii ijumuishe ujenzi wa mimea ya kisasa ya uchakataji wa taka za plastiki angalau moja kwa kila kanda. Hatua hii itasaidia kuongeza motisha ya usimamizi wa taka katika makazi ya watu na hivyo kuimarisha usafi wa mazingira.

kielelezo 4; Mchango wa watu wanaokusanya taka za plastiki mtaani.​

HITIMISHO
Katika kujenga jamii endelevu inayothamini usafi wa mazingira, jitihada za pamoja kati ya serikali, mashirika na wadau binafsi zinahitajika katika utoaji wa elimu kwa umma ili kujenga utamaduni wa kudumu kwa watanzania kuhusu usimamizi wa taka. Kwa kuzingatia suluhisho hizi, Tanzania inaweza kufanikiwa katika kuboresha usimamizi wa taka na usafi wa mazingira, na hivyo kujenga mazingira bora kwa maisha endelevu ya siku za usoni. Ni muhimu kwa serikali, sekta binafsi, na jamii kwa ujumla kufanya kazi kwa pamoja katika kutekeleza suluhisho hizi ili kufikia malengo ya usafi na afya bora kwa wote. Mwisho, ni muhimu Watanzania waelewe kuwa suala la usimamizio wa taka na usafi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja. Hivyo ni wajibu wetu sote kujenga utamaduni wa usafi wa mazingira ili kuandaa jamii bora kwa manufaa ya baadae.
 
Upvote 4
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…