Katika majadiliano kuhusu vilabu vya michezo, wasemaji wa vilabu hivi mara nyingi hujulikana kwa kujiamini na hata kujigamba.
Ligi maarufu za soka duniani zina vilabu ambavyo wasemaji wake wanapenda kunadi timu zao kupitia vyombo vya habari. Hivyo wanachofanya akina Kamwe, Ally, Ibwe, Masau, Ligalambwike nk si kitu kigeni, na binafsi sihisi kwamba kuna uchawa au siasa.
Kinachoonekana kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara sio jambo jipya katika tasnia ya soka.
Kwa baadhi yetu mashabiki, tunavutiwa na kipengele hiki cha "football and more." Hiyo 'more' ndiyo ipo kwa hawa wasemaji, wananogesha sana boli letu, na tunapenda kuwasikiliza wakitambiana.
Mimi binafsi napenda jinsi Masau Bwire na Thobias Kifaru 'Ligalambwike' wanavyotamba, pamoja na hawa vijana wa Simba na Yanga na Azam SCs.
Hebu tupunguze kuwa wakali na kuwa rasmi sana kwenye burudani kama mleta sledi unavyojaribu kuwa!!.
Burudani ya soka haihitaji urasmi kupita kiasi—ikiwa unataka kuleta uboss, bora ubaki ofisini upambane na mambo rasmi ya madodoso, madokezo nk, ukimaliza mafaili ya kazi zako nenda pale Kempiski au dubei kuinjoi au nenda jimkana kwa washua kacheze gofu.
Mifano ya Wasemaji wa Vilabu Mbali Mbali Duniani ambao wamechangamka "waongoza njia"
- Ligi Kuu ya Uingereza (EPL):
Vilabu kama Manchester United, Liverpool na Chelsea vina wasemaji ambao wana tambo kwelikweli na mara nyingi hujigamba kuhusu historia tajiri ya vilabu vyao, nguvu za kifedha na mafanikio uwanjani. Mbinu hizi zimesaidia Ligi Kuu ya Uingereza kupata umaarufu mkubwa hata huku kwetu Mwantombya ambako japo hatujawahi kufika huko UK, tunafuatilia ligi kwa shauku kubwa. Kazi kubwa ya publicity imefanya tukaijua na kuipenda EPL.
- La Liga (Hispania):
Real Madrid na Barcelona ni mifano bora ya vilabu vyenye mashabiki duniani kote. Wasemaji wa vilabu hivi mara kwa mara huzungumzia ubabe wao katika ligi ya ndani na mashindano ya kimataifa, huku wakijivunia wachezaji nyota waliopo kikosini.
- Serie A (Italia):
Juventus na AC Milan ni vilabu vinavyojivunia historia tajiri ya mafanikio na mikakati thabiti ya ushindi, ambayo wasemaji wao hupenda kuwasilisha masuala yao ya mafanikio kwa umahiri mkubwa kupitia vyombo vya habari.
- Bundesliga (Ujerumani):
Bayern Munich ni mfano bora wa vilabu vyenye wasemaji wanaozungumzia utawala wao katika ligi ya nyumbani na utendaji wao bora katika mashindano ya Ulaya.
- Ligue 1 (Ufaransa):
Paris Saint-Germain (PSG), pamoja na uwekezaji mkubwa wa kifedha na wachezaji nyota, ina wasemaji wanaosisitiza malengo ya klabu ya kutawala soka la Ufaransa na kuwa nguvu kuu katika soka la Ulaya.
Ligi hizi na wasemaji wa vilabu husika mara nyingi hutumia vyombo vya habari kuimarisha chapa ya vilabu vyao, kuhamasisha mashabiki, na wakati mwingine kufanikisha vita vya kisaikolojia dhidi ya wapinzani.
Dhima Kuu ya Wasemaji wa Vilabu:
Wasemaji hawa ni sehemu muhimu ya mbinu za kisaikolojia katika soka, maarufu kama
"mind games". Katika mpira wa miguu, mbinu hizi huchangia si tu morali ya wachezaji bali pia hutoa hamasa kwa mashabiki.
Binafsi nawapongeza vijana hawa wasemaji wanaojitahidi kuinua mchezo huu pendwa na wanatoa mfano mzuri kwa ukanda wa CECAFA. Si uliona hata Msemaji wa Vital’O ya Burundi, Arsene Bucuti, alivyopendezwa na kile wanachofanya? Na yeye akaiga japo walipokea kipondo kutoka kwa Klabu Kubwa Tanzania.
Penda mpira, furahia maisha. Acha kuchanganya siasa na soka!