Candid Scope
JF-Expert Member
- Nov 8, 2010
- 11,897
- 6,925
[h=1]‘Vijana msiwaze kuajiriwa, jiajirini'[/h]Vijana wameshauriwa kuacha kutegemea ajira za ofisini, badala yake watafakari namna ya kujiingiza katika ujasiriamali ili kuondokana na umaskini.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Kitivo cha Elimu ya Biashara na Uchumi cha Chuo Kikuu cha Iringa (IUCo), Enock Ugulumo kwenye maadhimisho ya wiki ya ujasiriamali iliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho mjini Iringa.
Maadhimisho hayo yalilenga kuwaongezea vijana na wanafunzi wa chuo hicho maarifa katika kujitegemea. Utafiti wa wataalamu mbalimbali duniani unaonyesha asilimia kubwa ya watu wanaotegemea ajira, hufa wakiwa maskini, tofauti na wale wanaojiajiri.
Alisema chuo hicho kimeanzisha mpango huo ili kuibua vipawa vya vijana na kuwawezesha wanafunzi kutumia elimu na ujuzi walionao kuibua ajira mpya, jambo ambalo litatoa fursa kwa jamii kupata nafuu ya upatikanaji wa kazi.
"Mfumo huu wa ujasiriamali ambao unaendana na mafunzo kwa vitendo, umelenga kuwafundisha wanafunzi namna ya kutengeneza bidhaa na kutoa huduma, kama sehemu ya kukabiliana na tatizo la ajira," alisema.
Mkurugenzi wa kitengo cha ujasiriamali wa chuo hicho, Dk Hosea Mpogole alisema mpango wa ujasiriamali kwa wanafunzi ulioanzishwa chuoni hapo utapunguza kero ya ajira nchini. "Vijana wakiwaza namna ya kujiajiri, Taifa litapaa kiuchumi," alisisitiza.