Hii nayo ni huruma ya NSSF au kuturudisha kwenye vijiji vya ujamaa?.Baadhi ya wanaolazimishwa kuchangia NSSF wala hawana haja na nyumba zenye michoro ya NSSF zilizopangwa kama kota au za Kibutz.
..............................................................................
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) inatarajia kuwekeza katika ujenzi wa hoteli ya kitalii na nyumba za kuishi, jijini Mwanza ambazo wanatarajia kuziuza kwa wanachama wao na kwa wananchi.
Katika mradi huo zaidi ya nyumba 687 zinatarajiwa kujengwa katika maeneo ya Bugarika pamoja na Kiseke ikiwa ni njia moja wapo ya kuwapunguzia wanachama gharama za ujenzi.Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mipango na Uwekezaji, Yacoub Kidula alisema mpaka sasa wameishalipa fidia kwa watu wote ambao walitakiwa kuhama kwenye maeneo hayo na asilimia 40 ya fedha kwa halmashauri ya jiji ili kutengeneza miundombinu ya barabara katika maeneo hayo.
Michoro yote ya ujenzi wa nyumba pamoja na hoteli imekamilika, muda siyo mrefu tunatarajia kunza ujenzi ambao utachukua mwaka mmoja kukamilika,alisema.Alisema wanaharakisha ujenzi wa nyumba hizo ili kushindana na mfumuko wa bei na kuzifanya nyumba hizo kuwa za gharama nafuu ili kila mmoja amudu gharama za kununua.
Kwa upande wa ujenzi wa hoteli alisema wameamua kuwekeza katika mradi huo kwa kuwa mji wa Mwanza unakua kwa kasi.Alisema katika awamu ya pili ya mradi huo watajenga shule pamoja na vituo vya afya katika maeneo hayo mawili ambayo watakuwa wamejenga nyumba za kuuza ili kusogeza huduma karibu wa wateja wao.
Mchakato wa kuomba viwanja kwa ajili ya huduma muhimu unaendelea na halmashauri ya jiji imetuhakikishia kutupatia viwanja hivyo,alisema Kidula.Waziri wa wa Kazi na Vijana Gaudensia Kabaka alisema Serikali inatakiwa kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wa ndani ili kuongeza thamani ya ardhi.
Ujenzi wa nyumba hizo ni wagharama kubwa na serikali haiwezi kujenga, ninaomba kusiwapo na vikwanzo vyovyote ili kuharakisha ujenzi wa nyumba hizo pamoja na hoteli hiyo ya kitalii,alisema Waziri Kabaka.
MWANANCHI