Utajiri wa rafiki yangu ulivyofanya nikamuamini Shetani - 14.
Mimi "Nishafika"
Warda "Umesimama wapi?"
Aliendelea "Ooh ok nishakuona"
Baaada ya nusu dakika alikuja mwanamke mmoja mwenye asili ya uarabuni akiwa amevaa hijab nyeusi ikiwa imempendeza sana kutokana na rangi ya ngozi yake.
Warda "Bila shaka wewe ndiye uliyetumwa na Ally"
Mimi "Yes ndiye mimi "
Warda "Unaitwa nani?"
Mimi "Naitwa Umughaka"
Warda "Mhh mbona Ally hakunitajia jina hilo!"
Mimi "Kaka Ally amezoea kuniita Master,Umughaka ndiyo jina langu halisi"
Warda "Ooh sawa nimekuelewa"
Aliendelea "Ngoja kwanza nimpigie simu halafu nikupe uongee nae"
Alichukua simu yake akaanza kumpigia simu Ally Mpemba na wakaanza kuongea,baada ya kuongea akanipatia na mimi simu ili niongee na Ally,baada ya kujiridhisha aliniambia nifuatane nae.Tulitembea kama hatua kumi kisha tukaingia kwenye nyumba moja ambayo ilikuwa ni ghorofa,ile ghorofa ilikuwa ni Apartment ya watu kuishi na haikuwa kwa ajili ya ofisi.
Baada ya kufika ndani tuliingia kwenye lift nikaona yule dada anabonyeza batani ambayo ilionyesha namba 4,ile lift iling'oa nanga na baada ya sekunde kadhaa tukawa tumefika kwenye floor namba 4,tulipofika tulitembea hatua 3 tukawa tumefika kwenye chumba ambacho baada ya kukifungua tuliingia ndani.
Warda "Nisubiri hapo "
Aliingia chumbani ambako hakutumia muda mwingi akawa ametoka na pochi kubwa ambayo ilikuwa imetuna.
Warda "Hizi ni pesa ambazo Ally amesema nikukabidhi sasa kabla ya kuondoka inapaswa uzihesabu ndipo uondoke"
Alizitoa zile hela kwenye ile pochi kubwa ya kike,kiukweli zilikuwa ni pesa nyingi sana.Nilianza kuzihesabu na kuzipanga ndipo nilipata jumla yake milioni 40.Wakati nazihesabu alikuwa amekaa akiniangalia huku akiendelea kuchezea simu yake.
Mimi "Tayari"
Warda "Umepata bei gani?"
Mimi "Milioni 40"
Warda "Ok uko makini"
Alichukua karatasi pamoja na wino akawa ameweka pale juu ya meza na kuniambia.
Warda "Shika hii"
Aliendelea "Utasaini hapa na hapo chini utaweka dole gumba "
Basi nikafanya kama alivyoniambia na nilipomaliza alichukua simu yake kisha akampigia simu Ally Mpemba.
Warda "Haya nishamkabidhi pesa yako,huyu hapa ongea nae"
Ally Mpemba "Master,huo mzigo nenda kaniwekee benki,nakutumia sasa hivi vielelezo"
Mimi "Sawa kaka"
Warda "Ngoja nikupatie kibegi kidogo,huo mkoba nina kazi nao"
Sasa baada ya kupewa kibegi kidogo,niliziweka zile hela kwenye kile kibegi huku akili yangu ikiwa imechanganyikiwa kabisa,nilipanga nitoroke na zile hela,baada ya kushuka ghorofani nilianza kutembea mdogo mdogo kuelekea mnazi mmoja.
Nilikuwa najisemea uenda ndiyo wakati ambao Mungu aliamua kunitoa kwenye umasikini kupitia zile hela za Ally Mpemba kwa maana hata kama ningeondoka zangu kurudi Mwanza asingepata kwasababu ni mtu tu ambaye nilikutana nae kkoo na halikuwa hanijui kiundani wala haifahamu familia yangu,kiukweli nilikuwa kwenye vita nzito kuhusu zile fedha lakini niliamua nizipelekea Benki ili kuendelea kuonyesha uaminifu wangu kwa Ally,nilisema kama ni umasikini niliandikiwa basi ningekufa masikini tu hata kama ningekimbia na zile hela,pengine ni heri kufa masikini kuliko kuiba cha mtu ambaye ufahamu kakipata vipi,Uaminifu kwangu hata kama usingenilipa lakini ungenijengea heshima kubwa miongoni mwa marafiki na watu wa karibu,hivyo niliamua kuwa muaminifu ingawa nilikuwa nahitaji sana fedha.
Nilitembea kwa haraka sana hadi katikati ya jiji mtaa wa Azikiwe ambapo kwa mujibu wa maelekezo ya Ally Mpemba ilipaswa niende hapo ilipo benki ya Crdb kuziweka hizo fedha.
Baada ya kumaliza kila kitu pale benki,niliondoka zangu kurudi kkoo,nilipofika kwakuwa muda nao ulikuwa umeenda sana,nilimwambia Aunt Farah anipatie kile kiasi ambacho aliambiwa na Ally anipatie ili niondoke zangu kununua mahitaji ya siku hiyo kisha niondoke nikaandae mapema.
Aunt Farah alinikabidhi laki tatu ambazo kwa mujibu wa maelekezo ya Ally Mpemba ni kwamba,laki mbili ningeitumia kwa mahitaji ya vitu kwa siku zilizokuwa zimebaki hadi yeye kurudi na ile laki moja ingekuwa kwa ajili ya matumizi yangu ya kawaida.
Kweli,ile kazi niliifanya kwa uaminifu mkubwa mno hadi siku ambayo alirudi Ally mpemba alikuwa akinishangaa namna nilivyokuwa muaminifu kiasi kile na sikuwahi kumwambia mtu yeyote siri ile.
Ally Mpemba "Kaka kati ya watu na wewe ni mtu!"
Mimi "Kwanini kaka?"
Ally Mpemba "Ndugu zangu si waaminifu kama wewe ulivyo muaminifu"
Aliendelea " Sielewi hata nitakulipa nini!"
Mimi "Usijali kaka haya ni maisha tu!"
Kiukweli nilikuwa najiuliza mle ndani kwa Ally kulikuwa na kitu gani lakini nilikuwa nakosa jibu kwasababu ndani ya siku zote hizo nimekuwa nikiwinda nipate kukiona lakini nilikuwa naishia kusikia sauti tu,mimi sikutaka kuonyesha kama nina wasiwasi,nilichofanya ni kwamba nikiwa nazungumza nae yeye aelewe mimi sifahamu chochote na nilikuwa napotezea mambo mengine ili asije kunoti kitu kutoka kwangu.
Niendelea kupiga kazi yangu ya usajili wa line za simu huku na ile kazi ya usimamizi wa Catering ikiendelea,kiukweli kama kuna muda ambao nilitengeneza pesa ilikuwa ni kipindi hicho,baada ya kupata pesa ya kutosha,nilimtafuta dalali akanitafutia uwanja maeneo ya Chanika Zingiziwa chenye ukubwa wa 25 x 20 nikawa nimenunua Milioni 3.
Nikawa nimepanga nipambane sana ili nikusanye fedha nyinngine nianze ujenzi mdogo mdogo ili nitoke kwenye nyumba za kupanga na mimi niamie kwangu.
Kuna siku tulipata tenda ya kuhudumia chakula maeneo ya Mikocheni,sasa Ally akawa ameniambia siku iliyokuwa inafuata nisiingie kazini ili niende kuwasimamia wale kina mama na vijana kama kawaida yangu maana ndiyo ilikuwa kazi yangu,kiukweli Ally alikuwa akiniamini sana na ilifika kipindi fedha zake zote mimi ndiye nilikuwa nikizipeleka benki,mkurya mimi nikajiona ni mtu mwenye bahati ya kuaminika na na mtu mwenye asili ya uarabu kuliko wakurya wote kutoka Tarime;kweli,siku iliyofuata sikwenda kazini kama kawaida na nilimpigia simu Team leader wangu nikampanga kabisa ili asije akaona baada ya kushika shika vihela nimeanza kuwa na kiburi.
Baada ya maandalizi mimi na timu yangu ya Catering,tukawa tumefika maeneo ya mikocheni kama kawaida,tuliendelea na maandalizi hadi kuhakikisha vitu vyote viko sawa,sasa tukiwa kwenye hiyo shughuli mida ya 2 usiku, Ally akanipigia simu akiwa na kiwewe kisichokuwa cha kawaida.
Ally Mpemba "Master hebu fanya haraka njoo hapa Sinza Mori"
Mimi "Kaka Sinza Mori sipafahamu"
Ally Mpemba "Hebu mpelekee Jabir simu niongee nae"
Baada ya kumpa Jabir simu na kuzungumza nae inaonekana alimwambia Jabir anitafutie muda ule Taxi na akamuelekeza eneo ambalo ningemkuta,sasa baada ya kupata Taxi,Jabir alimpatia maelekezo yule dereva kisha akaniambia niingie kwenye gari tuondoke.
Tulipofika hilo eneo ambalo ambalo Ally alikuwa amesema nimkute pale,nilimpigia simu akaniambia niingie ndani,ilikuwa ni hotel kubwa tu ambayo pia ilikuwa ni bar,nilipoingia ndani nilimkuta jamaa yupo na watu kadhaa wakiwemo mademu wenye asili kama yake wakila na kunywa.
Ally Mpemba "Kaka kanisaidie kufungua chumba,siunajua nimejisahau "
Aliendelea "Aiseee yaani hata sielewi nimejisahau vipi!"
Mimi "Sawa kaka ngoja sasa niwahi!"
Ally Mpemba "Ukishafungua utanirudishia hapa funguo utanikuta hapa hapa "
Mimi "Sawa kaka"
Niliondoka kuelekea kwenye Taxi tukaondoka zetu kuelekea Magomeni,nilipofika nilimwambia dereva Taxi anisubili nje ya geti.Nilifungua mlango kisha nikaingia ndani nikawasha taa,sasa nilipowasha taa sikuona kitambaa cheupe pale kwenye ile meza ya kioo ndipo nilielekea jikoni kwenye kabati nikakikuta ikabidi niende nikitandike kisha nikachukua kabeji na mboga mboga nikaziweka juu ya ile meza,baada ya kumaliza niliondoka zangu nikaenda kufungua ule mlango wa kile chumba.
Sasa nilipomaliza kuufungua ule mlango nikiwa nimegeuza mgongo naondoka ili nitoke ndani nifunge mlango niondoke,aisee nilisikia nimesukumwa na nguvu isiyokuwa ya kawaida,ile nataka kuanguka chini nilimuona kiumbe wa ajabu ananipita kwa kasi ya ajabu akiwa uchi kama alivyozaliwa akikimbilia sebuleni na kuanza kuyafakamia yale makabeji kwa spidi kali mno,nilipokuwa bado naendelea kushangaa na kuhamaki yeye hakuwa kabisa na muda na mimi.
Ndipo nilimshuhudia mwanamke aliyekuwa na asili ya kiarabu lakini akiwa na manywele mengi si kichwani tu hadi kwenye makwapa na sehemu za siri,alikuwa anatoa harufu kali sana ambayo haikuwa ya kawaida. Niliogopa sana na ikabidi nikimbilie nje na kufunga mlango kisha nikaelekea kwenye lile bomba la nje kunawa, baada ya kumaliza kunawa nikatoka nje nikafunga geti nikapanda Taxi kurudi Sinza kumrudishia jamaa funguo, kiukweli roho ilichafukwa sana na niliogopa sana na hata ujasiri niliokuwa nao wote uliyeyuka.
Huruma, majuto na masikitiko vyote kwa pamoja vilinisumbua sana kwa usiku ule; Sasa wakati nikiwa kwenye gari narudi Sinza, Ally Mpemba alinipigia simu akiwa kama mtu aliyepagawa.
Inaendelea:
Sehemu ya 15