Nisikuchoshe na usinichoshe, tusichoshane!.
Kwanza kabisa nipende kuwashukuru wote ambao mmeendelea kuwa na mimi bega kwa bega tangia mwanzo wakati naanza kusimulia visa vya maisha yangu ambayo nimeyaishi na kuyapitia kama mwanadamu.
Simulizi yangu ya kwanza kabisa hapa JF imefahamika kama "TULICHOMFANYA YULE MCHAWI HATOKUJA KUSAHAU KAMWE" hii inapatikana kwenye jukwaa hili la Entertainment, simulizi hii iliangazia namna tulivyopata shuruba ya ushirikina wakati ambao nilienda kumsalimia baba yangu mdogo aliyekuwa mwalimu katika shule moja ya sekondari huko mkoani Tabora, kiukweli ni mkasa ambao sitokuja kuusahau kamwe kwasababu ndipo niliamini wachawi wapo na uchawi upo!
Simulizi ya pili ilikuwa ni muendelezo baada ya hiyo ya kwanza, simulizi hii ya pili niliona nianze kusimulia baada ya mimi kwenda shule ya upili(Advance)na wakati nilipomaliza matokeo yangu hayakuwa mazuri hivyo nikatimuliwa na Mzee(Baba)yangu nyumbani nikaingia mtaani kupambana, simulizi hii inafahamika kama "
NILIVYONUSURIKA KIFO BAADA YA MZEE KUNITIMUA NYUMBANI" na inapatikana kwenye jukwaa la Habari na Hoja Mchanganyiko.
Sasa leo nimeona niwaletee na niendelee na masimulizi ya maisha yangu ili kuwapa hamasa vijana wenzangu kuweza kupambana na kutokata tamaa mapema! Dhumuni la masimulizi yangu ni kutoa funzo kwa watu na sipo hapa ili kujipatia fedha kwa njia ya ulagahai, mimi binafsi ninajiweza kwasababu ni mpambanaji na sihitaji hata mia mbovu ya walalahoi wenzangu!.
Mimi binafsi ni mfanyabiashara, nimejiajiri kwa kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria almaarufu kama Bodaboda, shughuli zangu huwa nazifanyia hapa Bunju, ingawa ki makazi naishi Mbezi Inn ila kikazi nafanyia Bunju. Sasa kama mtakumbuka kwenye simulizi ya mwisho nilisema ya kwamba, baada ya kuwa tumeuza lile duka la vipodozi ambalo tulikuwa tumefungua na rafiki yangu kipenzi Mtatiro (Kwa sasa anaishi nchini Uganda), tuliamua kugawana fedha kila mtu afe na chake, mimi niliamua kurudi zangu Tarime-Sirari, baada ya kukaa kule kuna ndugu yangu(Mtoto wa Baba yangu mkubwa) tuliwasiliana naye akaniambia nije Dar es salaam ili tufanye biashara ya uuzaji wa vyombo vya ndani kwasababu kwa wakati huo ilikuwa na pesa(Kwa maelezo yake).
Niliianza safari ya kuja Dar es salaam, sasa nilipofika Dar es Salaam pale Ubungo(Kipindi stendi bado haijahamia Mbezi), ile nimefika mida ya saa 5 usiku nikampigia simu mwenyeji wangu lakini majibu toka kwenye simu ni kwamba "Namba unayopiga kwasasa haipatikani, jaribu tena baadae", niliendelea kuipiga ile simu lakini majibu yalikuwa ni hayo hayo!.
Kwakuwa nilikuwa nimechoka, niliamua kumsikiliza moja ya watu ambao walikuwa wakinisumbua ili wabebe mzigo wa begi langu ili niwalipe posho, mpaka wakati huo nilikuwa makini sana kujilinda mimi binafsi pamoja na mzigo wangu, kilichofanya nikawa makini kupita kiasi ni stori ambazo mara zote nimekuwa nikizisikia kuhusu Jiji la Dar es Salaam na vioja vyake.
Mimi " Mwanangu vipi!?"
Jamaa " Poa bro"
Mimi "Mbona mnavurugu, shida ni nini?"
Jamaa " Si huyu msenge, nimemwambia wewe ni wakwangu lakini hataki kusikia"
Mimi "Ok mnasemaje"
Jamaa "Bro we nipe begi mi nikubebee, achana na huyu muhuni atakuibia"
Mimi " Sasa wote mnang'ang'ania mzigo, nimpe nani na nimwache nani?"
Mimi "Sa sikia, begi langu nitalibeba mwenyewe, achaneni na mimi"
Baada ya kusikia lafudhi yangu na namna nilivyochukia nadhani waliamua kutii sheria bila shuruti, waliondoka wakiwa wananiangalia kwa uchungu na maumivu makali ya kukosa posho! Kiukweli muda huo nilichokiongea ndicho nilichokuwa nikikimaanisha, kutokana na sifa mbaya za mkoa wa Dar es Salaam nilikuwa nimesema yeyote ambaye angejitia kimbelembele kunikaba au kuniibia, basi siku hiyo ndiyo ingekuwa mwisho wa maisha yake! Jeuri na kiburi cha kikurya vilinitia morali maradufu na niliwaona wale vijana wa pale stendi ni kama wanawake tu wasiokuwa na uwezo wa kunifanya chochote!.
Niliamua kujisogeza mpaka kwenye geti la kutoka nje, nilipotoka nje nilikuwa nikiendelea kushangaa pilika pilika namna zilivyokuwa za kutosha pale stendi, kiukweli sikuwahi kuona mji uliokuwa na pilika nyingi kama Dar es Salaam.
Mwanza nimekaa lakini hakukuwa na harakati za kutosha kama Dar es salaam. Nilichukua simu yangu nikawa nampigia tena mwenyeji wangu lakini simu yake ikawa haipatikani. Nilichukia sana kwasababu nakumbuka nilivyofika Singida alinipigia simu nikamwambia ya kwamba nimefika Singida na akawa amesema ikifika mida ya saa 2 usiku angekuwa amekuja pale stendi ili anisubiri nikifika tuondoke wote.
Kuna jamaa mmoja alikuwa kando ya geti la kutokea nje ya stendi pale Ubungo nilimsogelea nikawa namuuliza kuhusu Guest House yeyote iliyokuwa karibu ili niende nikalale na ikiwezekana asubuhi niendelee kumtafuta jamaa.
Jamaa "Sasa tutafanyaje ndugu!"
Aliendelea "Mwenyeji wako hajatokea?".
Mimi "Nimempigia simu lakini hapatikani!"
Jamaa "Duuuu mbona ni hatari!"
Aliendelea "Sasa sikia, wewe nyooka na hii barabara, unaona kwenye ile njia?"
Mimi "Ndiyo"
Jamaa "Hebu subiri"
Jamaa " Hassaniiiiiii"
Baada ya ya kuita hilo jina muhusika alifika
Jamaa "Hassani hebu nenda kampeleke huyu jamaa pale kwa Asteria, ukifika mwambie jamaa anataka chumba"
Aliendelea "Kaka nenda na jamaa atakupeleka kwenye Lodge ambayo kuna usalama na vyumba vipo vya kutosha, ila utamlipa maana kuna umbali"
Mimi "Hakuna tatizo"
Basi yule jamaa aliyeitwa Hassan akanichukua akanivusha barabara tukaikamata njia ya Ubungo Maziwa kuelekea kwenye hiyo lodge ambayo nimeambiwa kuna usalama na vyumba vya kutosha. Wakati tunakwenda na Bwana Hassan tulikuwa tunapiga stori za hapa na pale huku mikono yangu ikiwa bize imeng'ang'ania begi kwasababu ndilo lililokuwa na hela pamoja na nguo za kubadilisha, kiukweli nilikuwa nimesema endapo yeyote angejipendekeza kunikaba angejuta kuzaliwa.
Baada ya mwendo mrefu kidogo hatimaye tukawa tumefika kwenye Bar moja iliyokuwa inapiga mziki kwa sauti kubwa huku kukiwa na watu wengi.
Hassan " Nisubiri hapa nakuja"
Nilimsubiri Hassan pale nje baada ya kufika kwenye hiyo Bar na baada ya dakika 15 akawa amekuja kunichukua na kuongozana nae kuingia ndani. Tulipofika ndani ambako kulikuwa na kaunta, Hassan alinichukua tena kuelekea Uani ambako nilikuta kuna vyumba vingi ambavyo vilikuwa havipungui 10.
Sasa baada ya kufika pale Uani alikuja mwanamke mmoja mweusi mnene na ndiye aliyekuwa akiitwa Asteria, alimuita Hassan Pembeni wakawa wanaongea, sikufahamu kitu walichokuwa wanazungumza kwa wakati huo. Baada ya yale mazungumzo Hassan alirudi kwangu.
Hassan "Sasa bro,mimi nadhani nikuache wewe upumzike, niangalizie basi ustaarabu"
Mimi "Chumba changu cha kulala ni kipi?"
Hassan "Atakuonyesha Asteria, wala usijali kaka hapa ni nyumbani"
Baada ya maneno ya kutia moyo ya Hassan nikachomoa shilingi elfu 5 nikawa nimempatia kama posho ya kunipeleka hapo Guest.
Hassan "Aaah kaka hela gani hii?"
Mimi "Hela gani kivipi?"
Hasaan "Aaaah Kaka yaani nikutoe kule stendi na nimeacha shughuli zangu halafu unanipatia buku tano? Hebu ongeza ongeza kaka angalau kesho niamkie supu"
Sikutaka mambo mengi na yule Jamaa ikabidi nizame tena mfukoni nikatoa elfu 5 nyingine nikampatia, hivyo kufanya jumla kuwa elfu 10.
Baada ya jamaa kuondoka lile eneo nikamfuata yule demu aliyeitwa Asteria ili aje anionyeshe chumba niingie kulala kwasababu nilikuwa nimechoka.
Asteria "Kaka ina maana Hujaambiwa huu si muda wa kulala?"
Mimi "Si muda wa kulala?"
Mimi "Si muda wa kulala kivipi?"
Asteria "Kaka hapa huwa hatulazi watu ila tunakodisha!"
Aliendelea "Hivi vyumba vinakodishwa kwa dakika na masaa, labda usubiri mpaka saa 9 wateja wakipungua ndipo tutakukodishia ulale"
Kiukweli baada ya ile kauli niliishiwa nguvu ghafla, sasa baada ya kuniambia maneno yale yeye aliondoka akaenda kuendelea na shughuli zake akaniacha pale Uani nikiwa sijui cha kufanya, sasa ndipo nilikuja kugundua ya kwamba, vile vyumba vilikuwa vinatumika kwenye biashara ya short time(Biashara ya Ngono),sasa kumbe ile Bar niliyopelekwa, pale nje kulikuwa na wanawake wanaouza miili yao(Dada Poa) na vile vyumba vilitumika kwa shughuli ya short time.
Itaendelea.
Muendelezo soma
Utajiri wa rafiki yangu ulivyofanya nikamuamini Shetani
SEHEMU YA 1
SEHEMU YA 2
SEHEMU YA 3
SEHEMU YA 4
SEHEMU YA 5
SEHEMU YA 6
SEHEMU YA 7
SEHEMU YA 8
SEHEMU YA 9
SEHEMU YA 10
SEHEMU YA 11
SEHEMU YA 12
SEHEMU YA 13
SEHEMU YA 14
SEHEMU YA 15
SEHEMU YA 16
SEHEMU YA 17
SEHEMU YA 18
SEHEMU YA 19
SEHEMU YA 20
SEHEMU YA 21
SEHEMU YA 22
SEHEMU YA 23
SEHEMU YA 24
SEHEMU YA 25