Utajiri wa rafiki yangu ulivyofanya nikamuamini Shetani - 22
Aliendelea "Nakuuliza wewe,mbona upo kimya!?"
Mimi "Kaka kwani kuna nini?"
Ally Mpemba "Hujui ulichokifanya?"
Mimi "Kaka nipe nusu saa tuongee maana sipo salama kuzungumza!"
Baada ya kumwambia vile akawa amekata simu kwa jazba na kufyonza,nilitaka angalau nitoke nje niende hata kwenye gari nikazungumze na kaka Ally kwakuwa hadi muda huo sikuwa nimelielewa kosa langu hasa lilikuwa ni nini!.Niliamka nikaelekea kuoga kisha nikawa nimevaa vizuri nijiandae kutoka lakini Rehema nae akawa amesema nimsubiri akaoge kisha nimsindikize aondoke.Baada ya Rehema kumaliza kuoga alivaa nguo yake nzuri ya kitenge kisha tukawa tumetoka nje na kuondoka,sasa tulipofika kwenye gari,Rehema alishika kitasa cha mlango wa Mbele akawa amejiandaa kuufungua na kuingia ndani nilikumbuka maneno ya Ally Mpemba na nikamuwahi haraka nikawa nimemwambia asikae kiti cha mbele kwakuwa ni kibovu lakini ni kama hakunielewa na alidhani uenda ninamkataza kukaa mbele kwakuwa sitaki wanawake zangu wamuone.
Rehema "Wewe sema tu hutaki wanawake zako wanaione huna lolote"
Mimi "Kweli baby hicho kiti cha mbele huwa ni kibovu"
Rehema "Nshakwambia wewe sema hutaki wanawake zako wanione tu basi inatosha,mbona jana hukuniambia hivyo na tumekuja wote nikiwa nimekaa mbele! au kwasababu ilikuwa usiku ?"
Baada ya kuniambia jana usiku alikaa mbele ndipo nilizidi kuchanganyikiwa kabisa,sikutaka kumuonyesha nimeshituka ili asije kunishangaa,kiukweli hakuna siku niliyo ichukia pombe kama siku hiyo,kumbe baada ya kunywa bia kadhaa pale Tabata ukichanganya na kuchanganyikiwa kwa penzi jipya nikawa nimejisahau kabisa kwamba Ally Mpemba aliwahi kuniambia asije akatokea mtu yeyote akakaa kwenye siti ya mbele ya ile gari isipokuwa ndugu zake,sasa baada ya Rehema kuwa ameniambia vile ikabidi nimruhusu tu aendelee kukikalia kile kiti ili apunguze wivu kwakuwa kama ni kosa lilikuwa lishatokea.
Mimi "Basi baby kaa ili usinifikirie vibaya"
Rehema "Akuu wewe twende mi nitakaa nyuma nisije kukuletea shida kwa wanawake zako"
Mimi "Hapana baby kaa mbele twende maana ushanzaa nifikiria vibaya"
Baada ya kumbembeleza kidogo Rehema alifungua mlango wa mbele na kuingia ndani,niliwasha gari na kuondoka kuelekea Ubungo kumrudisha Rehema kwao;wakati tukiwa njiani nilikuwa nikimwambia kile kiti anakisikiaje ili kuendelea kutetea pointi yangu ya ubovu wa kiti asiendelee kunifikiria vibaya.
Mimi "Hausikii hicho kiti kama kinacheza?"
Rehema "Hapana,mbona mimi sisikiii?"
Mimi "Duuuu!..,nikishika kwa mfano breki mi naona kabisa kinaenda mbele na nikiachia kinakuwa kama kinarudi nyuma,wewe huwezi kuona "
Mimi "Nadhani baadae itanibidi niipeleke gereji warekebishe"
Maneno yote hayo ilikuwa ni kumfariji Rehema tu ili asinifikirie vibaya kuhusu maneno yangu yale ya uongo.Baada ya kumfikisha Rehema pale Ubungo nilimuachia na hela kiasi kwa ajili ya matumizi yake ya kawaida kisha nikaondoka zangu kuelekea Magomeni kwa Ally Mpemba.Nipofika nilifungua geti na kuiingiza ile gari ndani,nilishukaka nikaelekea kuufungua mlango na kuingia ndani ya nyumba.
Vile vyakula vya Maya vilikuwa pale sebuleni kama kawaida kwakuwa usiku ule hakuwa amekula na mimi sikutaka kabisa kuvitoa nikawa nimeacha palepale,nilikaa kwenye sofa pale sebuleni nikawa ninatafakari kwa kina jambo ambalo nilikuwa nimelifanya na kiukweli nilijuta sana na niliona kabisa naweza kukosana na Ally Mpemba hivi hivi!.Nijitahidi sana kuilazimisha furaha lakini moyoni mwangu tayari kulikuwa na majonzi makubwa mno.Baada ya masaa mawili kupita nikiwa naendelea kutafakari yaliyotokea,Ally Mpemba akanipigia simu tena na bado alionekana kukasirishwa na kukerwa kwa kile kitendo,kiukweli jamaa sikuwahi kumuona akiwa mkali kiasi kile.
Ally Mpemba "Nikwambia tangu mwanzo uwe makini lakini naona unataka kunitia kwenye umasikini,mimi siwezi kukubali kaka hiyo itakugharimu sana"
Mimi "Nisamehe sana kaka najuta kwa nilichokifanya"
Ally Mpemba "Mimi nikusamehe kama nani?,uliyemkosea yupo na ndiye mwenye mali unapaswa kumuomba msamaha"
Aliendelea "Umenikwaza sana Master pamoja na kukuamini lakini kumbe wataka kunirudisha kwenye umasikinik,aiseee wewe ni mtu mbaya sana"
Mimi "Kaka nilipitiwa tu nisamehe"
Ally Mpemba "Hebu kamuombe msamaha haraka kaka usije niletea matatizo!"
Kwakuwa nilifahamu kabisa kile kitendo nilichokuwa nimekifanya kilikuwa kimemkwaza Maya,moja kwa moja baada ya kuzungumza na Ally,nilichukua fungua nikausogelea mlango wa chumba cha Maya kisha nikaufungua na kuingia ndani,nilipoingia ndani sikutaka kabisa kuufunga ule mlango kwani niliogopa na nikaona ishu ikiwa ngumu basi mimi ni kutoka nduki!.
Nilipofika ndani nilianza kuongea kwa sauti ya upole na majuto ili kuonyesha nimefanya kosa na nalijutia.
Mimi "Nimekuja mbele yako Maya nakuomba unisamehe sitorudia tena!"
Mimi "Maya nakuomba unisikie na unisamehe kwa kitendo nilichokifanya na sitorudia tena"
Wakati naongea hivyo lile kabati ambalo ni kama mlango wa kuingilia kwenye lile shimo alimokuwa anakaa Maya lilikuwa limefungwa na ndipo nikaanza kusikia sauti za kilio cha kwikwi,kile kilio kilianza taratibu lakini kadiri dakika zilivyosogea ndipo nacho kilikuwa kikiongezeka.Mimi sikukata tamaa hata kidogo,niliendelea kumuomba msamaha lakini bado sikuona majibu.
Baada ya muda niliona ule mlango wa kabati ukifunguliwa na Maya akawa ametoka,kiukweli alikuwa amekasirika sana tofauti na mwanzo nilivyowahi kumuona,sikuwahi kumuona akiwa amejaa sumu kiasi kile huku machozi yakiwa yanamtoka,alisimama akawa ananiangalia huku akitetemeka kwa nguvu na kutoa sauti kama Nguruwe.Kile kitendo kiliniogopesha sana na nikaona naweza kupoteza maisha kimzaha mzaha,niliondoka kwenye kile chumba nikawa nimekimbilia sebuleni kwenye mlango wa kutokea nje,nilisimama pale mlangoni nikiendelea kuangalia hali itakuwaje na kama hali ingekuwa mbaya zaidi nilipanga kutoka nduki kuelekea nje.
Nikiwa nimesimama pale mlangoni Ally Mpemba akanipigia simu tena.
Ally Mpemba "Ushamuomba msamaha?"
Mimi "Ndiyo kaka nishamuomba msamaha lakini naona hajibu yupo kimya?"
Ally Mpemba "Yupoje?"
Mimi "Yupo vile vile tu kaka uchi"
Ally Mpemba "Nachotaka kufahamu yeye yupoje?,analia au anacheka?"
Mimi "Analia tu kaka na kutetemeka!"
Ally Mpemba "Hebu funga hiyo nyumba na uondoke haraka kuelekea Unguja,naomba ufanye haraka vinginevyo sitokuwa na huruma na wewe!"
Mimi "Kaka Unguja au Chumbe?"
Ally Mpemba "Usiendelee kupoteza muda hapo nimekwambia funga nyumba uondoke kwenda Unguja kwa Sheikh"
Mimi "Sawa kaka naondoka"
Ally Mpemba akawa amekata simu kwa jazba sana,Kiukweli jamaa alikuwa amechukia sana na ndipo sasa niliiona sura halisi ya Ally Mpemba akiwa amechukia namna anavyozungumza kwa ukali,mara zote nilikuwa nikimchukulia poa kumbe haikuwa kama nilivyodhani,niliondoka nikawa nimeenda kupanda daladala zilizokuwa zinaelekea posta maeneo ya bandari ili niwahi kuelekea Unguja kama alivyokuwa ameniambia Ally.Nilifanikiwa kuondoka mida ya saa 9 alasiri kuelekea Unguja ambapo baada ya kufikia kuna jamaa nilikuta ananisubiri na ndiye aliyeniepeleka hadi Chumbe kwa mzee yule ambaye nimewahi kwenda kwake nikiwa na Ally Mpemba.
Baada ya kufika pale hatukumkuta na jamaa yeye akawa ameniacha akaondoka,kuna mwanamke ambaye alikuwa mke wa mzee akawa amesema ametoka na hivyo ikabidi nimsubiri hadi arejee.Yule mzee alirejea saa 1 usiku na baada ya kufika tu swali lake la kwanza ilikuwa ni kwanini niko pale bila uwepo wa Ally Mpemba.
Mimi "kaka Ally ndiye kaniambia nije kwako"
Mzee "Mambo ni matamu ila mnashindwa kufanya utamu kuendelea kuuzuia utamu"
Aliendelea "watu wa bara mwatumia nguvu sana mahali isipohitajika!"
Mimi niliendelea kukaa kimya huku nikimsikiliza mzee akininanga kwa maneno ya kiswahili yasiyokuwa na chembe ya huruma.
Mzee "Mwenzio kajitahidi kutafuta mambo matamu nawe wataka mtia shubiri!"
Aliendelea "Haya wataka mie nikusaidie nini!"
Mimi "Kuna jambo limetokea mzee wangu ndipo baada ya kuwasiliana na Ally akaniambia nije kwako"
Mzee "Mie naelewa kila kitu weye ulichofanya,sasa hapa kwangu kuna mambo mawili,nsikize kwa makini,moja ni damu na mbili ni ufe wewe!"
Mimi "Sijakuelewa mzee tafadhali nieleweshe"
Mzee "Tangu lini watu wa bara mkaelewa!"
Aliendelea "Kuna mambo mawili weye uchague,moja utoe damu na mbili ufe weye!"
Mimi "Kufa hapana kwakweli,nitoe damu mzee wangu"
Mzee "Hupendi kufa na weye wafanya ujinga!"
Aliendelea "Haya nsikize kwa makini,huyo aliyesababisha haya inapaswa afe kwa kumwaga damu,sasa kuna dawa nitakupatia na nguo hivyo ukifika bara hakikisha unafanya kama nitakavyokueleza"
Mimi "Sawa mzee"
Usiku ule mzee alinichukua akawa amenipeleka kwenye nyumba moja ambayo hakukuwa na mtu ndani yake,tulivyofika hapo alichukua nguo ya ndani ya mwanamke (Chupi)ambayo ilikjwa mpya kabisa na ilikuwa ya rangi nyekundu,kisha akachukua kopo moja ambalo kulikuwa na unga fulani ambao sikuuelewa kisha akaniambia kwakuwa Mwanamke niliyekuwa naye usiku ndiye chanzo cha matazizo ni lazima yeye afe ili mimi nisalimike kwakuwa kosa lile halikuwa na mzaha hata kidogo,kimuonekano waweza kudhani kosa la kukaa siti ya mbele lilikuwa la kawaida kumbe haikuwa kama nilivyokuwa nimedhani.
Mzee "Shika hii!"
Niliichukua ile chupi nikawa nimeishika kama alivyokuwa amenitaka kufanya.
Mzee "Hii dawa utaipaka hivi,na ukishamaliza kuipaka utampelekea huyo mwanaizaya huu mzigo na uhakikishe anaupokea kwa mikono yake miwili usije mpa mtu mwingine kuipokea badala yake,ukifanya hivyo usije kunilaumu!"
Mimi "Sawa mzee"
Mzee "Hii chupi ataivaa na akishaivaa utanipa majibu"
Mimi "Sasa hawezi kuikataa?"
Mzee "Hawezi!,ukifika bara ingia duka lolote mnunulie chupi nyingine kama zawadi na umpelekee kwa pamoja ikiwemo na hii"
Mimi "Itamtosha kweli?"
Mzee "Hiki ndicho kipimo chake na hakikisha utakazonunua zilingane saizi na hii"
Mimi "Sawa ,nimekuelewa mzee"
Baada ya maelekezo yale mzee alinitaka niwe makini tena siku nyingine kwenye harakati kwasababu mambo huwa si mepesi kama nilivyodhani,nililala pale kwake na Asubuhi mida ya saa 2 niliodnoka kuelekea bandarini kwa ajili ya kuianza safari ya kuelekea Dar es salaam.
Nilipofika Dae es salaam nilielekea mitaa ya Kkoo kununua chupi nyingine kama zuga ili nije nimpelekee Rehema kama zawadi,chupi nilizonunua zilikuwa za rangi tofauti na zilikuwa jumla tano na hakukuwa na ugumu kwasababu nilipoingia kwenye lile duka nilimuonyesha ile chupi nyekundu na nikawa namwambia ni size ya mpenzi wangu hivyo anipatie size kama hiyo.
Inaendelea:
Sehemu ya 23