Utajiri wa rafiki yangu ulivyofanya nikamuamini Shetani - 24.
Mimi "Alinionyesha album ya picha "
Farah "Kitendo cha Ally kukuonyesha Album ya picha ya familia yake anakuamini sana kama mimi nilivyokuamini tangu mwanzo "
Aliendelea "wewe ni mtu mwema sana master kama hujui Ally anakuamini sana"
Kadiri Farah alipozidi kuongea kiukweli ndiyo nilizidi kuchanganyikiwa kwasababu ni kama sikumuelewa,mwanzo alianza vema sana kuzungumza lakini kadiri muda ulivyozidi niliona mabadiriko.
Farah "Unataka kuniona?"
Mimi "Ndiyo dada Farah nahitaji kukuona uenda kuna kitu utanisaidia!"
Farah "Huwa naonwa na mume wangu tu,sasa nikiondoa Nicab tambua wewe ni mume wangu!"
Mimi "Ndiyo maana nimekuomba dada"
Farah "Siwezi kukutolea hapa hadharani Nicab watu wote wanitazame"
Aliendelea "Kuna lingine?"
Mimi "Hapana Dada"
Niliondoka kuelekea nje kuendelea na kazi zangu lakini kiukweli siku hiyo hata kazi haikwenda vizuri,niliamua kuondoka zangu kuelekea nyumbani kupumzika tu.
Sasa nakumbuka Ally Mpemba akawa amerudi na alipokuwa akinikuta pale Kkoo pembeni ya duka lake nilikuwa nikimsalimia anaitikia kama hataki,ile hali kiukweli ilikuwa ikinipatia taabu sana,niliona nimtafute angalau nimuombe msamaha.Nijaribu kumwambia dada Farah aniombe msamaha kwa Ally lakini pia akasema ndugu yake hataki kunielewa.
Ile kazi ya Catering nayo ni kama iliota mbawa kwangu kwasababu sikuwahi kuambiwa tena wala kupewa ratiba ya kitu gani kilichokuwa kinaendelea,kitu nilichokuwa nakitegemea ni ile bangiri tu ambayo kila mwisho wa mwezi ilikuwa ikinipatia fedha,sasa nakumbuka hata mwisho wa mwezi huo ni kama hali ikaanza kuwa mbaya sana,ile bangiri ilibana kama kawaida na nikatoa damu nyingi sana lakini cha ajabu sikupata fedha hata tone.Kiukweli ile hali ilinitisha sana na kibaya nilipojaribu kuivua ilikuwa haitoki,nilidhani uenda ikawa inanibana nikachukua sabuni na kupaka kulainisha mkono lakini wapi!,sikuishia hapo tu bali nilichukua na mafuta ya kupikia nikajipaka mkononi kulainisha lakini nilipoitoa haikutoka.
Sikutaka kabisa kupoteza muda,nilijaribu kumpigia Ally Mpemba simu angalau ajaribu kuongea na Mzee wa Chumbe lakini jamaa simu zangu alikuwa hashiki kabisa na kuna muda alikuwa akizima.Ile hali ilibaki kama siri yangu lakini niliona nitafute mtaalamu anisaidie vinginevyo ningeendelea kukaa kimya hali ingekuwa mbaya sana.Nilimtafuta yule mshikaji wangu ambaye nilikuwa nikifanya nae kazi kule Dege aliyeitwa Mwakisaka angalau nimueleze hali niliyokuwa naipitia kama mwanaume mwenzangu,ingawaje sikumwambia ukweli lakini jamaa hakuwa na neno.
Mwakisaka "Kimya sana kaka"
Mimi "Mapambano tu ndugu yangu"
Mwakisaka "Nilikutafuta mara kadhaa ukawa hupatikani!"
Mimi "Sasa hivi natumia namba hii kaka ya Tigo"
Mwakisaka "Wapi sikuhizi "
Mimi "Bado nipo palepale Gongo la Mboto kaka"
Mwakisaka "Mwanangu mi niko Dodoma napambana"
Mimi "Mambo mazuri huko nini kaka!"
Mwakisaka "Mwanangu huku kuna hela,siunajua tena watu wanajenga sana huku"
Mimi "Sawa kaka,sasa kuna ishu naomba nikushirikishe kaka"
Mwakisaka "Niambie mwanangu"
Mimi "Mwanangu hivi kuna mtaalamu yeyote ambaye ni mzuri unaweza kuwa unamfahamu?"
Mwakisaka "Mtaalamu wa...?"
Mimi "Mganga kaka"
Mwakisaka "Vp ulikuwa na shida nini!"
Mimi "Yeah kuna ishu nilikuwa nataka kuziweka sawa kaka,siunajua mjini hapa!"
Mwakisaka "Nakuelewa sana kaka!"
Aliendelea "Ishu yako kubwa ni nini "
Mimi "Nilitaka tu wa kuniangalizia mambo yangu kaka"
Mwakisaka "Kama ni kuangalia mambo mbona wapo kibwena!"
Mimi "Ndo unisaidie sasa kaka"
Mwakisaka "Kwasasa nipo kibaruani,nipe muda hata jioni au kesho nitakupa jibu kaka!"
Mimi "Sawa kaka"
Baada ya mazungumzo na Mwakisaka niliamucha jamaa apambane na kazi yake na nikaendelea kuvuta subra kama alivyokuwa ameniahidi.Kazi kwa upande wangu ikawa ngumu sana kiasi kwamba hata nikienda pale Kariakoo kwa ajili ya usajili wa line za simu nilikuwa napata wateja 2 hadi 3 kwa siku kitu ambacho haikuwa kawaida,zamani nilikuwa nikiweka meza tu ile nimefungua unakuta wateja ni wengi sana kiasi kwamba mpaka nilikuwa nafurahi.
Nilimtafuta Mwakisaka baada ya siku mbili maana niliona jamaa uenda akawa ametingwa na mambo lukuki.Sasa nilipojaribu kumtafuta jamaa akawa ameniambia atanipigia baada ya dakika kumi na kweli baada ya dakika hizo akawa amenipigia.
Mimi "Kaka niambie basi ndugu yangu"
Mwakisaka "Kaka kuna mtaalamu mmoja yupo pale Namanyere,unapafahamu?"
Mimi "Namanyere sipafahamu kaka ila napasikia"
Mwakisaka "Sasa jamaa anapatikana kule na ni mtaalamu kweli kweli kaka naamini kwa shida yako ya kuangalia mambo yako basi atakusaidia"
Mimi "Nipatie lokesheni kaka namna ya kufika kwake"
Mwakisaka alinielekeza namna nzuri ya kufika kwa huyo mtaalamu na akawa amenipatia namba yake ya simu ili niwasiliane nae kabla ya kuondoka.Sasa nakumbuka nilipowasiliana na jamaa ilipofika usiku Ally Mpemba alinipigia simu.
Ally Mpemba "Acha kuangaika wewe unachokitafuta utakipata!"
Mimi "Kaka nahangaika kwa kitu gani?"
Ally Mpemba "Mimi nakuonya tu,usije sema sikukwambia "
Aliendelea "Haya mambo umeharibu mwenyewe ila sasa hivi unataka kuwatafuta watu ubaya,shauri yako!"
Mimi "Kaka nisamehe ndugu yangu,najua nilifanya makosa makubwa sana naomba unisamehe!"
Ally Mpemba "wewe fanya ulichokuwa unataka kufanya kaka ila ukijaribu utakiona cha moto!"
Aliendelea "Kuna muda unanisababishia matatizo lakini kwasababu dhamira yangu ni kuukimbia umasikini hivyo nakupuuza tu!"
Baada ya jamaa kuniambia kwa jazba alikata simu.Nilijaribu kumpigia tena lakini akawa hapokei tena.Rehema kuna muda aliniambia alikuwa anahitaji kama nina uwezo nimpeleke chuo akasomee ualimu,yeye hakufahamu kama kwa kipindi hicho nilikuwa ninapitia hali ngumu ya kimaisha na ukosefu wa fedha;Kwakuwa nilimpenda na nilikuwa nina ndoto nae,niliona lile pagale langu la kule Chanika niliweke sokoni ili niweze kumpeleka chuo Rehema.Namshukuru Mungu lile pagale niliweza kuliuza kupitia madalali na hivyo nilipata kiasi cha fedha ambacho kilitosha kabisa kumpeleka Rehema chuo cha ualimu na fedha nyingine ikabaki nikawa nimeihifadhi,Rehema nilimpeleka chuo cha ualimu Mhonda.
Maisha yalivyozidi kwenda Kombo kuna siku ilibidi nimfuate Ally Mpemba pale Aggrey nikajaribu kuonana nae na akanisikiliza ila akaniambia nijitahidi siku itakayofuata niende kwake nikaonane nae.
Kesho yake kweli nilikwenda hadi kwake na jamaa akanipatia kazi nyingine ya kufanya.
Ally Mpemba "Kwakuwa umetambua kosa lako na mimi kusema ukweli nililipa gaharama za uharibifu wako kwangu"
Aliendelea " Ila kama umeona nafaa tena kuwa na wewe nitakutazama na ikishindikana nadhani utapotea,huo ndio ukweli na wala nisikufiche"
Mimi "Kaka sasa hivi siwezi kufanya ujinga tena nimejifunza"
Ally Mpemba "Mimi hivi karibuni nafungua mgahawa ila naomba wafanyakazi unitafutie wewe na nitakupa kazi maalumu"
Mimi "Sawa kaka hakuna tatizo!"
Jamaa aliniambia kwenye mgahawa wake huo anao ufungua mimi ndiye niwe msimamizi na atanielekeza namna ya kuwa nawatoa kafara wafanyakazi kila baada ya miezi 6 hadi mwaka ili tuendelee kupiga pesa,ule mgahawa hadi leo ninapoandika hapa upo na unapiga kazi kama kawaida na wafanyakazi kila mwaka ni lazima afe mmoja,hiyo niliasisi mimi.
Ally Mpemba "Utakuwa tayari tufanye kazi?"
Mimi "Nipo tayari kaka"
Ally Mpemba "Ok wewe kaendelee na shughuli zako na utakapokuwa tayari kukamilika nitakujulisha"
Mimi "Kaka lakini hali yangu si nzuri kiuchumi"
Ally Mpemba "Uliharibu wewe kaka,utajiri hauko kama unavyodhani,nilazima uulinde kwa wivu mkubwa sana"
Aliendelea " Subiri nakuja"
Jamaa aliingia ndani akawa ametoka na hela kadhaa,sasa baada ya kuhesabu kiasi kile ilikuwa ni shilingi laki 5.
Ally Mpemba "Chukua hizo zikusogeze angalau kidogo"
Inaendelea: Sehemu ya 25