Asante, kwa kweli mimi hapa nimeshuhudia aina tofauti za uongozi Kenya, niliishi enzi ambazo hatukua na demokrasia, yaani kipindi kile kutaja jina la rais uliruhusiwa tu wakati unamsifia, hata kwenye klabu cha walevi pamoja na ulevi wote ilikua huwezi kutaja chochote cha kuhusu serikali, au rais.
Wakuu wa wilaya, machifu, viongozi wa mitaa na hata mapolisi walikua wanatunyanyasa, yaani nakumbuka kwetu kijijini ilikua kawaida kufikishiwa ujumbe kwako nyumbani eti chifu anashida nawe, ukamwone mara moja, na ukifika kwake anakuamrisha utoe kitita fulani cha hela maana serikali imekua ikifuata mienendo yako na wana taarifa kukuhusu na hurusiwi kuhoji ni taarifa zipi hizo maana serikali haihojiwi.
Rais akitangazwa kuja mjini kwetu, lazima tutoke wote mashuleni tukamlaki pembeni mwa barabara, maduka yote yalikua yanafungwa, biashara zinasimama, uchumi wa nchi ulikua umekwama, uzalishaji na ukuaji wa uchumi vilikua vitu vya kigeni kwetu. Ikulu ilikua inapiga simu na kuamrisha makampuni yachangie mamilioni ya hela, kamata kamata za mapolisi zilikua mambo ya kawaida, walikua wanazunguka kitaa na kukusananya vijana bila makosa yoyote, tunaswekwa kwenye kaladinga za polisi kiholela.
Haiwezekani hata kidogo nikawaza kurudi huko hata siku moja, tumepiga hatua, tumesonga, tupo mbali sana kila nikiangalia nyuma naona umbali wa tulikotoka, naweza nikaandika mengi sana ya tuliyopitia enzi hizo. Nilikua mmoja wa waliopokea vibano vya polisi ili tufikie hapa tulipo.
Nakiri hatujafika, safari bado mbali, hatua za kukamilisha bado ni nyingi lakini taratibu tunasonga, changamoto zipo, kuna viongozi ambao waliishi kwa mazoea ya zamani bado wanapitia hali ngumu ya kuzoea huu mfumo mpya. Damu bado inamwagika, mabomu ya machozi bado yanarindima mjini, makelele na mikimbio kila siku, lakini tutafika na nina uhakika watoto wetu ipo siku wataishi kwa raha sana, lakini kwa sasa tutapambana hadi kieleweke maana nimeona matunda ya katiba nzuri, niemonja hayo matunda na kama walivyosema wataalam wa maisha mchovya asali hachovi mara moja.