Utani; Rebmann na Wachagga mlimani Kilimanjaro

Utani; Rebmann na Wachagga mlimani Kilimanjaro

Wildlifer

JF-Expert Member
Joined
May 12, 2021
Posts
1,884
Reaction score
5,235
Paa la Afrika.
images (29).jpeg

Nilikuwa nimesikia mengi juu ya Kilimanjaro, mlima mrefu kuliko wote barani Afrika. Hali kadhalika, nilisoma mengi na kutazama picha nyingi zilizoonyesha mlima huo. Lakini katika yote hayo niliyosikia au kuona kwenye picha hakukuwepo lolote lililoniacha nisiweze kupigwa na butwaa huku nikiwa siyaamini macho yangu pale nilipoutia machoni mlima huu. Kwa kweli, ni mlima ambao lazima uuone, kusimuliwa pekee kulikuwa hakutoshi.

Ilikuwa ndio kwanza nashuka toka katika basi lililonileta mjini hapo, macho yangu yalipopokelewa na utukufu ule. Ujio wangu Kilimanjaro ukiwa umefanyika bila matarajio baada ya yale mapokezi ya kutisha niliyoyapata Singida. Mapokezi ya kulazwa chumba kimoja na fisi.

Ni mawazo hayo yaliyofanya Singida kama nuksi nyingine iliyokuwa ikinisubiri. Hali iliyopelekea baada ya siku mbili tatu za kuzurula mjini hapo nipande basi lililonileta Kilimanjaro, kwa matarajio ya kupata kazi au biashara yoyote ambayo ingeniwezesha kupata chochote ili nitimize azma yangu ya kurudi nyumbani. Azma ambayo umuhimu wake uliongezeka siku baada ya siku.
Mlima ulisimama pale kwa kiburi na fahari zote. Ulikuwa peke yake, ukiwa umechomoza hadi juu ya mawingu, kiasi cha kujionyesha vizuri popote uliposimama katika eneo la miji kama Moshi, arusha na vitongoji vyake. Ukiwa umepambwa kwa theluthi iliyokuwa ikimeremeta kileleni, Kilimanjaro ulisimama pale, peke yake, kama mfalme aliyevalia taji lake ambaye hakuwa na mpinzani. Hapana, alionekana zaidi kama malkia mwenye majivuno, aliyevalia mapambo yake yote, ambaye hakupenda kujichanganya na watu wengine.
Sijui ningeukodolea macho kwa muda gani mlima huo kama nisingehisi kushikwa bega huku sauti ya mtu mmoja ikisema, “Angalia, yasije yakakukuta yaliyomkuta Rebmen kwa kuushangaa mlima huo.”

Nikazinduka. Nikayaondoa macho yangu toka kileleni na kumtazama msemaji. Alikuwa mpita njia tu, mvulana aliyevaa mavazi ya shule, mfuko wa madaftari yake ukiwa kwapani. Alikuwa akitabasamu.
“Rebmen gani?” nilimuuliza.
John Rebmen. Yule Mjerumani aliyekuwa Mzungu wa kwanza kuutia machoni mlima huu,” alifafanua.
images (30).jpeg

Nikalikumbuka jina hilo. Nikakumbuka pia tarehe na mwaka ambao Rebmen aliuona mlima huo kwa mara ya kwanza. Ilikuwa Mei 11, 1848.
Rebmen alifanya nini?” niliuliza.
“Hukumbuki?” mwanafunzi huyo alinihoji. “Hukumbuki yaliyompata? Hukumbuki kuwa aliibiwa mfuko wake uliokuwa na fedha zake, nyaraka zake na kumbukumbu zote za safari yake? Ulivyokuwa umeduwaa pale wewe pia ungeweza kuporwa huo mfuko wako bila kujijua”
Nikacheka. Nilikumbuka kusoma tukio hilo kwenye kitabu cha mwandishi mmoja. Nadhani alikuwa Rebmen mwenyewe aliyeandika. Kwamba akiwa Kilimanjaro, maeneo ya kibosh, aliibiwa mfuko wake uliokuwa na fedha zake zote na nyaraka zake zote muhimu. Siku hizi watani wa Wachaga, hasa Wapare, hulitumia tukio hilo kuwadhihaki Wachaga kuwa kwa ajili ya tukio lile Rebmen aliyekuwa mmisionari aliwalaani hata wakawa watu wa kupenda na kuabudu sana pesa kuliko utu. ‘Mchaga mzuri ni aliyekufa tu,’ ni moja ya kauli zinazoendana na utani huo.

Ingawa sikumbuki kama kweli Rebmen aliibiwa wakati akiushangaa mlima lakini bado nisingeweza kumlaumu. Kwa mtu kama yeye, aliyetoka mbali sana na ambaye hakupata kusikia wala kuona picha ya mlima huo kama mimi, kuduwaa kiasi cha kuibiwa begi lake kamwe lisingekuwa jambo la ajabu.

Kitendo cha ardhi kuchomoza hadi meta 5894 juu usawa wa bahari, huku ukiwa umesimama peke yako siyo jambo la kawaida. Aidha, ile theluji kileleni na historia ya milipuko ya volkano katika vilele vyake vitatu vya Kibo, Mawenzi na Shira
Kilimanjaro_3D_view.jpg
ni sababu nyingine za kihistoria ambazo zitamfanya mtazamaji aukodolee macho hata kuweza kuporwa begi lake.

(Kiguu na Njia, Ben Mtobwa, Sura ya 5, Uk 243—)
images (28).jpeg
 
Back
Top Bottom