SoC01 Utashi wa kuku na mustakabali wetu wa uongozi

SoC01 Utashi wa kuku na mustakabali wetu wa uongozi

Stories of Change - 2021 Competition

John Eddy

New Member
Joined
Jul 13, 2021
Posts
0
Reaction score
0
Kuku ni kiumbe chenye utashi wa ajabu kama walivyo viumbe wengine ambao ni tofauti na binadamu. Mtu anapotaka kumtega kuku aliyepo katika kundi la kuku wengi hurusha punje za mahindi, mchele au mabaki mengine ya chakula. Kundi la kuku litaanza kumfuata taratibu mpaka ndani, kisha anafunga mlango na kumkamata kuku anayemhitaji na kumchinja. Kuku wengine wataachiwa na kuondoka. Mchinjaji anaweza kurudia mchakato uleule wa awali baada hata ya dakika tano na kumkamata kuku amtakaye na kumchinja. Kuku watategeka tena, wamesahau kwamba mwenzao aliadhiriwa dakika tano zilizopita, maisha yanasonga, wanazaliwa wanachinjwa.

Kwetu sisi wanadamu tutawananga kuku hawa kwa utashi wao huo wa kutochanganua mambo, inafika wakati hata tunawabeza. Lakini tunayoyafanya leo au yanayotukumba leo tukiwa na utashi wetu kamili kama jinsi ambavyo tunajipambanua kwamba sisi ni tofauti na viumbe wengine kwa sababu tuna utashi mkubwa sana wa kung,amua mambo (Rational being), tuna tofauti gani na kuku? Kwa mfano, bara la Afrika lilipitia katika kipindi cha Ukoloni.

Wakoloni walitumia mbinu mbalimbali za kuingiza utawala wao wa kidhalimu, kinyonyaji na kikandamizaji. Walitumia punje (Mbinu) maridhawa zilizowatega watawala wa mababu zetu kuingia machinjoni, ziliwalevya wachache wao hata wakaamini kwamba himaya zao zitakua imara na madhubuti chini ya wakoloni katika sekta za kiuchumi, kiutawala, kijeshi na hata kijamii. Watawala kama Chifu Mangungo wa Msovero, Kabaka wa Buganda ambaye aliingia makubaliano na Waingereza mwaka 1900 na kuzaliwa kinachoitwa makubaliano ya Buganda (Buganda Agreement of 1900). Ili kujikwamua na madhila haya, wazee wetu waliungana na kufanikiwa kumwangusha dhalimu.

Looh! Baada ya muda mchinjaji akarudi na mbinu mpya za kututega tena (Ukoloni mamboleo), tukaingia mtegoni tena na kusahau dakika tano zilizopita wenzetu waliingizwa mtegoni na kuchinjwa. Ukoloni huu unawatumia tena watawala wetu kwa kuwahadaa na zawadi nono, kuwafanya mawakala wao wa kibiashara kupitia makampuni yao ya kibeberu na hata kuwawekea miongozo ya namna ya kuongoza nchi. Utashi wa kuku!

Tuache hayo, naomba niende moja kwa moja kwenye mada yangu ya leo nikiangazia Tanzania yetu. Kama Nchi nyingine zinazojipambanua kidemokrsia, nchi yetu imekuwa ikiingia kwenye majaribio kadhaa ya ukomavu wa kidemokrasia (Democratic maturity). Kila baada ya miaka mitano kumekuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, tukiwa tunahesabu uchaguzi wa sita tangu siasa za nchi zilipoingia kwenye mfumo wa ushindani wa vyama vingi (Multiparty system). Kabla ya kujikita kwenye mada, tujadili dhana ya Uchaguzi na umuhimu wa Uchaguzi.


Malengo ya uchaguzi nini?

Uchaguzi ni mchakato muhimu sana katika ushiriki wa kidemokrasia kwa sababu hutoa fursa ya kupata wawakilishi na pia ni njia ya kuwawajibisha viongozi legelege. Uchaguzi huwa na umuhimu ufuatao katika mchakato wa kidemokrasia;

Kuwapatia wananchi na viongozi watarajiwa fursa ya kutafakari na kujadiliana kuhusu changamoto za maisha ya watu na namna bora ya kukabiliana nazo. Hasa chaguzi ni fursa kwa wananchi kuwaambia wagombea na fursa kwa wagombea kuwaambia wananchi.

Kutoa fursa kwa wananchi ya kuchagua kiongozi na pia nafasi ya kubadilisha kiongozi, kwa maneno mengine uchaguzi ni moja ya fursa za kuwawajibisha viongozi.

Kuwakumbusha wananchi kwa wao ndio wenye mamlaka na kwamba viongozi ni watumishi wao.

Kuwakumbusha wananchi na wagombea kuwa kura ni mkataba baina ya wananchi na mgombea na mgombea akishinda uongozi anapaswa kuwajibika kwa watu.

Kwa nini ni muhimu kushiriki uchaguzi?

Ibara ya nane (8) ya Katiba ya JMT (1977) inatamka wazi kuwa hii ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii. Moja ya misingi ya Demokrasia ni “Uhuru wa maoni”, “Ushiriki”na pia “Kupiga kura na kupigiwa kura”. Lakini pia moja ya haki za kijamii ni afya, maji, kilimo, hifadhi ya jamii na elimu. Hivyo yapo mahusiano makubwa baina ya ushiriki katika chaguzi huru na upatikanaji wa huduma za jamii.

Ibara ya 8 (1) inasisitiza kwamba;

Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa katiba hii;

Lengo la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi;

Serikali itawajibika kwa wananchi;

Wananchi watashiriki katika shughuli za serikali yao kwa mujibu wa masharti ya katiba hii.


Vipengele hivi vinne hasa (a) na (c) vinachochea nguvu ya “kura” ya mwananchi/raia. Vipengele hivi vinawakumbusha viongozi watarajiwa kuwa wananchi ndiyo WAAJIRI wao na wanapaswa kuwajibika kwao.

Hivyo uchaguzi ni mchakato wa kudai haki na wajibu; ni mchakato wa kuweka mkataba baina ya mpiga kura na mpigiwa kura.

Kila raia anapaswa kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, hili ni hitaji la kikatiba kama linavyotajwa katika ibara ya 21 (1):

“…Kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria”

21 (2): Kila raia anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomhusu yeye, maisha yake au yanayolihusu Taifa.


Hivyo ni wazi kuwa haki za kijamii ni suala linalomhusu kila Mtanzania na pia uchaguzi ni suala linalomhusu kila raia hasa kwa kuwa lina mahusiano makubwa na upatikanaji wa haki za jamii.

UCHAGUZI UNATUHUSU!

Ni kipindi ambacho watanzania wanapata nafasi ya kuwapima wagombea katika ngazi mbalimbali kwa kutimiza haki yao ya kidemokrasia. Naamini chaguzi hizi mbili zinawafanya watanzania wafanye maamuzi ya busara na yenye kuleta tija katika mustakabali wa Taifa kiuongozi. Waache kuhadaika na mitego ya wasaka tonge hawa kwa sababu itawapa raha ya muda mfupi na kuwasababishia madhila ya kipindi kirefu cha miaka mitano.

Kila mpiga kura ana utashi wake, ni vigumu kumwamuru mtu kumpigia kura mtu Fulani. Sababu ya mpiga kura A ni tofauti na sababu ya mpiga kura B. Kuna kundi la wapiga kura wanaoongozwa na hisia (Emotions) katika kumhalalisha mtu kuwa kiongozi wake. Kwa mfano wengine huvutwa na mwonekano wa nje wa mgombea, kwa kuangalia namna alivyovaa, sura yake, anavyopangilia maneno yake, vijembe vyake dhidi ya wapinzani wake, bendi za muziki alizoambatana nazo, wengine huzingatia ukongwe wa chama hata kama ufanisi wa watu wake umepungua, ushawishi wa marafiki au wazazi, kwa mfano, kama baba ni mkereketwa (Zealot) wa chama Fulani basi atawashawishi watoto au mama kupigia kura chama hicho

Wachache wao hufanya hivyo kwa kusudi la kulinda biashara zao kwa kuwaunga mkono wagombea kadhaa kwa lengo tu la kulinda maslahi yao. Kundi jingine huongozwa na sababu zenye mantiki (Rationality) katika kufanya maamuzi sahihi kwenye sanduku la kura. Wadau wa kundi hili huchambua kwa kina umahiri (Competency) wa mgombea, itikadi, ilani na falsafa ya chama chake katika kuleta mabadiliko. Binafsi naamini katika kundi hili.

Kwetu sisi Tanzania, wapiga kura walio wengi tumekuwa tukiwapapatikia wagombea wa nafasi mbalimbali bila kuwachambua kwa kina. Wanatupa punje za mchele kwetu kwa kuandaa sherehe kubwa kubwa kwa kupitishwa na vyama vyao vya siasa na hata kushinda chaguzi mbalimbali. Tunafurahi nao lakini mwishowe wanatupotea. Baada ya muda wanarudi mikono nyuma na punje tamu zaidi, bila kuwachuja vema tunaingia mkumbo na kusahau walichotufanya dakika chache zilizopita. Utashi wa kuku!

Ningependa kuangazia taasisi ya urais (Presidential wing), eneo hili la uongozi huwa na kurupushani nyingi sana. Kwa bahati nzuri sana watanzania tuna bahati kubwa sana ya kuwachuja wanaotaka kiti hiki kitakatatifu. Wenye nia huanza kujionesha mapema hata kabla ya michakato ya uteuzi ndani ya vyama vya siasa (Intra-party nomination process). Hata vyama hivi vya siasa vinapowapitisha wagombea urais, bado tunakuwa na muda mrefu kuwachambua. Tumejifunza kupitia makosa yaliyopita kwa sababu ya utashi wetu, tuliongozwa zaidi na hisia katika kufanya maamuzi sahihi kwenye sanduku la kura. Chaguzi hizi mbili ziwe chachu ya kufanya mabadiliko sahihi katika mfumo wa uongozi wetu.

Tuwachambue sana watu ambao wameonesha nia ya kuutaka urais kabla ya kuwashabikia kwa kujiuliza maswali kadhaa juu yao. Wachache wao walishawahi kuhudumu katika serikali wanayotaka kuiongoza na wengine bado wanahudumu. Tunapaswa tupime ufanisi na uimara wao kupitia uchambuzi wa UMAFUTI (Uwezo, Mapungufu, Fursa na Tishio) au NUFUVI (Nguvu, Udhaifu, Fursa na Vikwazo), yaani (SWOT Analysis). Tuwaweke kwenye mizani mmoja mmoja kwa kuangalia matokeo chanya waliyoleta walipokuwa wa kihudumu katika sehemu ya mfumo, nikiwa na maana kwamba baadhi walishakuwa mawaziri na wengine ni mawaziri.

Je, walikuwa na mbinu gani mbadala kuondoa kero zinazowakabili wananchi?

Kama waziri wa mifugo, aligundua mbinu gani mbadala za kurekebisha au kutilia mkazo hatua zilizoandaliwa kuondoa kasoro zilizoko kwenye mfumo zinazosababisha wakulima na wafugaji kumwagana damu kila kukicha? Kama waziri wa mahusiano au mambo ya ndani alikuwa na njia gani mbadala za kurejesha au kuimarisha mahusiano kati ya wananchi na vyombo vya dola au serikali?

Tukijiuliza maswali haya na mengineyo kabla ya kufanya maamuzi sahihi kwenye sanduku la kura tutakuwa na uongozi unaowajibika madhubuti ambao utafanya kazi kwa shinikizo la kwamba wananchi hawaishii kupiga kura tu, bali wana utashi mkubwa wa kuhoji mienendo ya sera na viongozi wetu hata kabla ya kufikia uchaguzi mwingine.

Tuna nafasi kubwa ya kuwachambua watu hawa kuliko kuwapapatikia na kuamini katika propaganda zinatufanya tutishike kisaikolojia na kushindwa kufanya maamuzi sahihi kwa sababu ya hofu. Ifike mahali hata kwenye kampeni zao wakiongea hoja za kuwashambulia watu tuwaambie wazi, kwamba, tunataka utuambie utatusaidiaje na sio kumnanga mtu jukwaani, MPIGA KURA WEWE NI MWAJIRI, AJIRI MTUMISHI ATAKAYEKUONGOZA KUFIKA UNAPOPATAMANI NA SIO MLAMBA NYAYO MWENYE HESHIMA ZA KINAFKI.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom