Babu yangu Mwanakijiji,katu usitingwe akilini
Watakuja wengi wajibuji,na majibu yaso kifani
Haihitaji kumpa mtu mji,ili upate jibu akilini
Embe lisilo na kokwa,si embe bali kimbembe
Embe lisilo na kokwa,kamwe haliwezi tokea
Hata ukienda Rukwa,lenye kokwa watakuelea
Embe lilo na kokwa,vizuri mtini labembea
Embe lisilo na kokwa,si embe bali kimbembe
Amani kweli umenena,kuhusu kokwa lilo laini
Kwa hakika umenikuna,kwa wako ubeti makini
Kokwa laini lililotuna,embe lake ni tamu jamani
Embe lisilo na kokwa,si embe bali kimbembe
Embe lililo na kokwa,kwa nafasi linanyonywa
Laliwa pasi kumenywa,na maganda lamengenywa
Hilo embe lisilo na kokwa,hata bure huwezi pewa
Embe lisilo na kokwa,si embe bali kimbembe