masai wa kilosa
New Member
- Aug 30, 2022
- 1
- 0
UTAWALA BORA
Ni vizuri tukaanza kwa kuangazia maana ya utawala bora, japo sio kwa tafsiri rasmi. Utawala bora ni dhana inayohusisha ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi yanagusa maisha au maslahi yao kwa namna moja au nyingine. Maamuzi hayo yanaweza kuwa yanagusa nyanja za kisiasa, kijamii au hata kiuchumi. Hivyo basi, ni wazi kwamba utawala bora ni moja kati kati ya dhana muhimu ambayo inagusa maisha ya kila siku ya mwananchi.
MISINGI.
Dhana ya utawala bora inajengwa katika misingi mbalimbali, lakini katika makala hii nitazungumzia demokrasia na utawala wa sheria. Demokrasia ni pale ambapo watu au wananchi wanashiriki katika kuamua mambo yao na hayo maamuzi kuheshimiwa. Kwa nchi yetu, moja kati ya njia za wananchi kushirikishwa katika maamuzi yao ni pale ambapo wananchi hupata haki ya kuchagua au kuchaguliwa kuwa viongozi kupitia mifumo ya kisiasa. Utawala wa sheria hujidhihirisha pale ambapo watu wote wanakuwa sawa mbele ya sheria na kuongozwa na sheria sawa. Utawala wa sheria pia hulenga kuondoa maamuzi binafsi yanatokana na mihemko bila kuzingatia sheria zilizopo.
Sheria hutungwa na bunge kwa mujibu wa sheria zetu kama inavyoelezwa kupitia ibara ya 64 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977. Japokuwa bunge linaweza kukasimisha jukumu hilo kwa mamlaka zingine. Ni wazi kuwa siasa ni maisha, hakuna namna ambayo maamuzi ya kisiasa yataacha kuathiri maisha yako iwe moja kwa moja au la. Tuchukulie tu mfano mwepesi kabisa, kupitia sheria maisha ya mwananchi huongozwa. Inaweza kukushangaza lakini ni uhalisia kuwa sheria zinaanza kukuongoza hata kabla hujazaliwa, mfano kupitia kifungu cha 219 cha Sheria ya Kanuni ya adhabu sura ya 16 inatoa adhabu kwa kosa la kuharibu mtoto ambaye hajazaliwa. Huo ni mfano tu mmoja wapo, lakini je ni mara ngapi tumesikia makaburi yakiamishwa kwa maamuzi ya serikali (kupitia viongozi)? Kumbe hata ukifa, bado sheria zinaamua na kukugusa. Na unapokuwa hai, hapo ndipo unaguswa moja kwa moja kupitia sheria mbalimbali ikiwemo sheria za kodi na nyinginezo. Hivyo basi ni wazi kuwa uwe mfungwa, mtu huru, mkulima, mfanyabiashara, mfanyakazi au sehemu yoyote ile, huwezi kukwepa kuguswa na maamuzi ambayo ni matokeo ya siasa.
JE, NI MUHIMU KUJIHUSISHA NA SIASA?
Kabla hatujajadili kuhusu umuhimu wa kushiriki katika siasa, ni vizuri tukakumbuka na tukaangazia uhusiano uliopo kati ya siasa na maisha ya kila siku. Maamuzi ya kila siku ni matokeo ya maamuzi ambayo hufanywa na watu au viongozi wanaotokana na mchakato wa kisiasa. Ni wazi na ni muhimu tukakubaliana kwamba wanadamu tumeumbwa kwa uwezo tofauti na vipawa tofauti, wapo ambao wana uwezo mkubwa sana wa kufikiri na kutenda jambo, wale wenye uwezo wa kawaida na wale wenye uwezo wa chini. Wanasiasa ni watu wanaotokana na jamii yetu, hivyo tusitegemee kuwa wanaweza kuwa na tabia za tofauti kabisa na jamii. Kama ambavyo tuna watu kwenye jamii ambao ni wabinafsi, wapo wachapakazi, wapo wenye fikra chanya na misimamo thabiti, wapo wasaka fursa wanaojipendekeza na kuwa wanafiki na tabia nyinginezo ambazo pia zipo kwenye jamii zetu. Sio vema kutaja majina kwa mifano, ila ukifuatilia na kufanya uchambuzi wa kina, utaweza kuwagundua na kuwapanga wanasiasa katika tabia mbalimbali ambazo pia ni tabia za baadhi ya watu katika jamii zetu.
Hivyo basi kama ambavyo tuna watu waadilifu, wazalendo, wenye maono, wapenda haki na usawa ni wazi kuwa tunaweza kuwa na viongozi wenye tabia hizi pia. Hili litafikiwa kwa ushiriki mkamilifu wa jamii katika siasa. Sehemu kubwa ya viongozi katika taifa letu ni matokeo ya michakato ya kisiasa. Tujiulize tu, kama siasa itaachiwa watu ambao sio waadilifu, wasiopenda haki na usawa, wasio na maono ya mbali yaliyo chanya kwa taifa, wanafiki na wanaojipendekeza tutapata viongozi wa aina gani? Na tukikumbuka kuwa viongozi wengi ni matokeo ya michakato ya kisiasa.
Nitoe rai tu kwa kila mwananchi, kutambua kuwa siasa ni jambo muhimu sana, siasa inaamua hatma ya kila mmoja bila kujali kuwa ulishiriki au hukushiriki katika kuchagua viongozi. Viongozi wakichaguliwa, wanakuwa viongozi wa wote bila kujali kama ulishiriki au hukushiriki kuwachagua. Je, ni busara kuacha kushiriki siasa kwa sababu tu kuwa “ siasa ni mchezo mchafu ‘’? je mchezo mchafu unaoamua hatma ya maisha yako huwezi kuufanya ukawa mchezo msafi? Je, uchafu huo ni matokeo ya kanuni za mchezo au aina ya wachezaji? Je, hatuwezi kubadili kanuni au wachezaji ili usiwe mchezo mchafu? Shiriki siasa ndugu yangu, siasa ni Maisha. Siasa ndiyo huamua kodi utakayolipa, sheria zitakazokuongoza, matumizi ya fedha na rasilimali za nchi yako na mambo mengine mengi. Je, upo tayari kufanya kazi, kufanya biashara, kukatwa kodi na tozo mbalimbali kisha kuwaachia viongozi ambao hujashiriki kuwachagua waamue hatma ya jasho lako?
Utawala bora unahusisha ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi ambayo yanagusa Maisha au maslahi yao kwa namna moja au nyingine. Na moja kati ya namna ambazo wananchi wanashirikishwa katika maamuzi ni kupitia siasa. Tanzania kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, hairuhusu mgombea binafsi. Tutumie mfano wa nafasi ya urais na ubunge kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya ibara ya 39 (1) (c) na ibara ya 67 (1) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1997 ili mtu aweze kugombea au kuchaguliwa kuwa Rais au mmbunge ni lazima awe amependekezwa na Chama Cha Siasa.
Hivyo basi, ili kuboresha utawala bora ni vizuri na muhimu pia kuhakikisha ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi katika siasa.
Upvote
0