Mahakama ya hakimu mkazi Arusha imeahirisha kwa mara nyingine shauri la uhujumu Uchumi linalomkabili aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Lengai ole Sabaya na wenzake sita baada ya mshitakiwa Sabaya kuendelea kuwa mgonjwa.
Jana Novemba 3 mwaka huu mahakama hiyo iliahirisha shauri hilo baada ya kuarifiwa kuwa mshtakiwa namba moja (Sabaya)anaumwa na hakuweza kufika mahakamani na kupanga kesi hiyo kuendelea Leo (jana), ambapo shahidi wa saba wa jamhuri ambaye ni Ofisa wa Tehama wa Benki ya CRDB Kanda ya Kaskazini, Jofrey Nnko angeendelea kutoa ushahidi wake.
Akizungumza mahakamani hapo, Wakili wa utetezi Mosses Mahuna aliieleza mahakama kuwa mtuhumiwa huyo wa kwanza bado ni mgonjwa na kuwa ametoa ruhusa kesi hiyo iendelee kusikilizwa bila yeye kuwepo.