Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
=================
===================
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Mamlaka ya Udhibiti, Usafiri Ardhini (Latra) wamelaani vikali kitendo cha waandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) na dereva kushambuliwa wakati wanatekeleza majukumu yao.
Waandishi hao Fortune Francis na Sunday George pamoja na dereva wao Omary Mhando walivamiwa na kupigwa huku gari waliyokuwa nayo namba T707 DKW lililokuwa na nembo za kampuni kuharibiwa na kupasuliwa vioo, wakiwa wanatekeleza majukumu yao.
Mbali na kujeruhiwa kwa waandishi hao na dereva, pia wameibiwa simu za mkononi.
Tukio hilo lilitokea mchana wa jana Jumamosi, Julai 22, 2023 wakati waandishi na dereva walipofika kufuatilia maandalizi ya mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chadema unaofanyika leo Jumapili, Bulyaga, Temeke jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo limeripotiwa Kituo cha Polisi cha Chang’ombe.
Tukio hilo lilitokea wakati wanaangalia maandalizi ya mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao unafanyika leo Jumapili uwanjani hapo.
Leo Jumapili, THRDC na Latra wameungana na wadau mbalimbali kulaani tukio hilo. Mkuu wa idara ya huduma za utetezi kwa watetezi wa haki za binadamu kutoka THRDC, Wakili Paul Kisabo amesema kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 waandishi wa habari wana haki na uhuru wa kukusanya taarifa ikiwa ni pamoja na kuuhabarisha umma juu ya taarifa hizo.
“Hivyo kwa namna yoyote ile ni makosa na ni kinyume cha Katiba na Sheria za nchi kuwashambulia waandishi wa habari wakiwa wanatekeleza majukumu yao,” amesema
“Mtandao unatoa wito kwa wananchi kujiepusha na vitendo vya kuwashambulia waandishi wa habari ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kuuhabarisha umma na tunatoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la Polisi ili wale wote waliohusika kuwashambulia waandishi hao wajulikane na wakamatwe kwa mujibu wa Sheria,” amesema Kisabo.
Wakili Kisabo amesema mtandao unatoa wito kwa jeshi la Polisi kufanya upelelezi kwa kuzingatia Sheria na Amri Kuu za Jeshi la Polisi (PGO) ili kuhakikisha kwamba wale wote waliohusika wanakamatwa na kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.
“THRDC tunatoa wito kwa jeshi la Polisi nchini kuimarisha ulinzi na usalama kwa raia pamoja na mali zao ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu nchini ikiwa ni pamoja na kwenye mkutano unaofanyika leo katika viwanja hivyo,” amesema Kisabo.
Nayo Latra kupitia salamu zake za pole imesema, imesikitishwa na inalaani kitendo cha waandishi hao kushambuliwa wakiwa wanatekeleza wajibu wao.
"Latra inatoa pole kwa waandishi hao, Gazeti la Mwananchi kwa ujumla na kuwatakia waliojeruhiwa uponaji wa haraka. Tunaamini waliofanya uhalifu huo watatafutwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria," imeeleza taarifa ya LATRA iliyotolewa kwa umma.