Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Dodoma, Abdulhabib Mwanyemba amesema baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani ambao wamekuwa wakijinasibu na kudai ‘No Reform, No Election’ ni waongo, akidai kuwa hufanya vikao vya siri vya kuwaandaa watu kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Mwanyemba ameyasema hayo mkoani Dodoma katika ziara yake na Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Mkoa na Wilaya ya Mpwapwa walipotembelea Shule ya Msingi Kingiti kuzindua shina tawi katika Kijiji cha Iyenge na Lukole.
Aidha, amesema wanayoyaongea viongozi hao yanakinzana na uhalisia kutokana na wao kukosa msimamo, “Wanasema kwamba ‘hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi’, si kweli, tulikuwa na tume ya uchaguzi lakini sasa tuna tume huru ya uchaguzi na waliyokuwa wanataka yafanyiwe marekebisho yamefanyiwa”.
Katika ziara, Mwenyekiti Mwanyemba ameongozana na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu hamasa na chipukizi mkoa wa Dodoma Wenslaus Mazanda, wajumbe wa kamati ya utekelezaji wa UVCCM mkoa huo, Charles Nyembela, Mahmoud Omary Yusuph na viongozi wa umoja huo wa Wilaya ya Mpwapwa.