Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
UWANJA WA MNAZI MMOJA 1948
Nilipata kuandika katika moja ya mitandao ya kijamii kuwa takriban kila aliyesikika katika historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika yumo ndani ya Nyaraka za Sykes.
Baadhi ya wasomaji walinishambulia wakinishutumu kuwa nina mkakati wangu maalum wa kuharibu historia ya uhuru.
Kwa hakika mjadala ule ulikuwa mkali sana na sababu kubwa ni kuwa wale waliokuwa wananishambulia pengine walifanya hivyo kwa nia njema tu.
Wengi walikuwa kwanza wadogo kwa umri na pili ni wageni wa Dar es Salaam kwa hiyo baadhi ya majina ambayo wanakutanana nayo katika makala zangu na matukio ambayo wanayasoma yaliyofanywa na wazalendo niliokuwa nawataja wao hawajapata kuyasikia hata siku moja katika historia ya uhuru.
Elimu katika mtandaoni inabidi mwalimu afanya rejea ya kurudia somo analosomesha mara nyingi kwani ni mfano wa basi linalosimama katika vituo na abiria wapya wanapanda.
Makala iliyoandikwa na pengine kujadiliwa siku nyingi za nyuma msomaji mpya ataisoma leo na atakuja na maswali ambayo tayari yalishajibiwa.
Katika majuma haya ya karibuni nilifanya mahojiano na mtangazaji Hilda Foya wa Azam TV kuhusu Kariakoo.
Mada ilikuwa wazi na tulizungumza mengi kuhusu Kariakoo kuanzia soko lenyewe na yaliyopitika pale sokoni wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.
Huu ulikuwa wakati wa miaka ya mwanzoni 1950 Mwingereza Brian Hodges katoka katika nafasi ya Market Master na nafasi ile amechukua Abdul Sykes.
Haraka sana tukaingia katika historia ya Julius Nyerere, Shariff Abdallah Attas, Mshume Kiyate katika soko lile kama wazalendo ndani ya TANU wanapambana na Waingereza.
Siku zote kila ninapokuja na historia mfano wa hii hiki kizazi cha leo hupigwa na butwaa kubwa wakisema hiyo kwao ni historia mpya kabisa.
Wanasema hawajapata kusikia historia hii popote si shule ya msingi, sekondari, chuo kikuu wala hawajasoma katika kitabu chochote.
Mtangazaji Hilda alikuwa kaja na kadha akawa kapata na akaondoka na kadha wa kadha.
Akaniambia kipindi chake bado hakijakamilika sharti twende katika mitaa na sehemu nilizozitaja anihoji tukiwa katika sehemu hizo.
Jana tukalifanya hili.
Picha ya pili Hilda Foya na mpiga picha wake wako pembeni ya nyumba ya Bi. Mwamtoro Chuma na hapo walipo ni mpaka wa nyumba ya Bi. Mkubwa huyu na Ofisi ya TANU, Makao Makuu enzi za kupigania uhuru.
Angalia picha ya nyumba hizo.
Nikawaeleza historia ya nyumba hiyo ambayo yote iko Mtaa wa Kariakoo wakati nyumba ya TANU ilikuwa kwenye kona ya New Street na Kariakoo.
Mtoto mkubwa wa Bi. Mwamtoro Chuma alikuwa Haidar Mwinyimvua kati ya wanachama wa mbele na shupavu wa TANU na mtu aliyekuwa karibu sana na Julius Nyerere.
Ilikuwa TANU wakiwa na mikutano ya ndani kwa ufinyu wa nafasi Bi. Mwamtoro alikuwa anavunja ua wake wa makuti na kuangunisha nyumba yake na ua wa ofisi ya TANU ili papatikane nafasi ya watu kukaa.
Rais wa TANU Mwalimu Nyerere alikuwa akifanya mikutano mingi katika ua wa nyumba hii ya Bi. Mwamtoro.
Bi. Mwamtoro huyo hapo kwenye picha akipiga kura Uchaguzi Mkuu mwaka wa 1970 na picha inayofuatia ni mwanane Haidar Mwinyimvua.
Picha nyingine tuko Mnazi Mmoja sehemu ya pili upande Kidongo Chekundu tumesimama katikati ya uwanja ule.
Nimegundua kuwa kizazi cha leo kinajua Mnazi Mmoja ni ule uwanja nyuma ya Ukumbi wa Arnautoglu hawajui chochote kuhusu uwanja wenyewe khasa ambako ndipo ulilipokuwa huo mnazi mmoja wenyewe.
Hapa ndipo kwa mara ya kwanza katika mkutano wa hadhara wa TANU mwaka wa 1955 Nyerere aliwahutubia wananchi na kuwaambia kuwa kutawaliwa ni fedheha Watanganyia tunadai uhuru wa nchi yetu.
Nilimweleza mtangazaji Hilda Foya kuwa mimi nikiujua uwanja wa Mnazi Mmoja toka utoto wangu na nikamwambia afute katika akili yake hayo magorofa upande lilipo Jengo la Washirika na badala yake aweke nyumba za wenyeji zilizoezekwa kwa makuti na madebe; na aondoe hizo barabara mbili za Lumumba Avenue aweke barabara moja nyembamba ya vumbi New Street.
Nikamweleza kuwa hapo Mnazi Mmoja ni sehemu ya mchanga mtupu wazi hakuna ukuta wala hapajajengwa chochote ni uwanja tu ambao watoto wakicheza mpira jioni na Siku ya Iddi zikifungwa pembea na kujengwa vibanda kwa ajili ya kusheherekea sikukuu.
Hapa Mnazi Mmoja ndipo TANU ilipoanza kampeni yake dhidi ya ukoloni wa Mwingereza.
Picha ya mwisho ni Uwanja wa Mnazi Mmoja kama ulivyokuwa miaka hiyo.
Picha hii imepigwa na Mohamed Shebe.
Turejee mwanzo wa makala niliposema kuwa nilipata kuandika kuwa kila aliyehusika katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika utamkuta katika Nyaraka za Sykes.
Nilipokuwa natalii kutaka kujikumbusha historia ya uhuru niliingia katika kitabu cha Abdul Sykes kuutafuta uwanja wa Mnazi Mmoja.
Hayo hapo chini ndiyo niliyoyakuta:
''Abdul Sykes alikuja kupata habari kuwa mpinzani wake katika kile kinyanganyiro cha nafasi ya katibu wa Dar es Salaam Dockworker's Union na adui wa baba yake wa miaka mingi, Erika Fiah, alikuwa akiuchochea uongozi wa chama kumpindua akisema, ''Muondoeni yule mtoto wa Kleist Mzulu.''
Baadhi ya wale makuli walikuwa wanataka hasa Abdul Sykes ajiuzulu na ampishe Fiah achukue uongozi wa chama.
Jambo hili liligawa chama pande mbili.
Upande mmoja ulimtaka Abdul Sykes aendelee kukiongoza chama na mwingine ulimtaka ajiuzulu mara moja.
Fiah alitakiwa kwa sababu baadhi ya wanachama walidhani Abdul Sykes alikuwa na msimamo wa wastani mno akizuia makuli kufanya mgomo na wakaunga mkono mwelekeo mkali wa Fiah.
Mgogoro ulipoendelea bila ya dalili zozote za kutatulika, Abdul aliitikia wito wa baba yake na akajiuzulu cheo chake Julai 1948.
Abdul Sykes aliiongoza Dar es Salaam Dockworker's Union kwa miezi sita tu.
Lakini ilipodhihiri kuwa kweli Abdul sasa anajiuzulu na itawabidi wanachama wachague katibu mpya, kikundi cha wanachama kilimzuia na kumuomba abakie.
Abdul Sykes hakutaka kubadili uamuzi wake.
Alikuwa ana matatizo mengine nyumbani.
Baba yake alikuwa mgonjwa kitandani taabani kwa maradhi na alikuwa akikisisitiza kuwa Abdul lazima ajiuzulu nafasi yake mara moja.
Katika kuonyesha mshikamano makuli walimbeba kijana wao Abdul Sykes juu juu mabegani toka ofisi za Dockworker's Union Acacia Avenue (Samora Avenue) hadi viwanja vya Mnazi Mmoja mahali ambapo wanachama wa Dockworker's Union walikuwa wakifanya mikutano yao.''
Miaka saba baadae baada ya haya Abdul Sykes alikuwa akionekana Mnazi Mmoja katika mikutano ya TANU kasimama nyuma kabisa akiandika hotuba za Nyerere katika short hand (hati mkato) neno kwa neno.
Hotuba hizi inaaminika zipo katika shajara zake ambazo hadi leo wanafamilia hawajazifungua zisomwe.
Hii ni hazina kubwa ambayo thamani yake ni tabu kukadiria.
Mimi nimeziona shajara hizi kwa macho yangu nyumbani kwa mwanae, Kleist Sykes, Sea View miaka ya 1980.
Historia ya uhuru wa Tanganyika ina mengi.
Ukifika makaburi ya Kisutu kaburi la Abdul Sykes na Haidari Mwinyimvua yamekaribiana sana.
Hawa wote watu wa TANU ya New Street miaka ya 1950 ya mikutano ya ndani uani kwenye nyumba ya Bi. Mwamtoro bint Chuma.
Nililiona kaburi hili la Haidar Mwinyimvua siku ya maziko ya Kleist Sykes na aliyenionyesha ni Adam Haidar mtoto wake ambae yeye na Kleist katika utoto wao walisoma pamoja Shule ya Aga Khan katika miaka ya 1960.
Hakika historia ya TANU ina mengi.