Uwezo Tanzania yazindua Mradi wa Kijiji Changu awamu ya IV Njombe

Uwezo Tanzania yazindua Mradi wa Kijiji Changu awamu ya IV Njombe

Parabolic

JF-Expert Member
Joined
Dec 3, 2013
Posts
2,922
Reaction score
3,252
264A2685.jpg (1).jpeg

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa elimu baada ya kuzindua Mradi wa Kijiji Changu (My Village) Agosti 11, 2026.

NJOMBE, Agosti 11, 2026. Shirika la Uwezo Tanzania imezindua rasmi awamu ya nne ya Mradi wa Kijiji Changu (My Village), unaolenga kuboresha uwezo wa watoto katika kusoma, kuandika na kuhesabu katika shule na vijiji 120 vya Mkoa wa Njombe.

Uzinduzi wa mradi huo umefanyika chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka, na unahusisha halmashauri zote sita za mkoa huo.

Mradi huo unapanua matumizi ya Mbinu ya Jifunze, ambayo awali ilifanyiwa majaribio kupitia mpango wa ufadhili wa pamoja katika Wilaya ya Ludewa.

Kwa mujibu wa Uwezo Tanzania, upanuzi huo unalenga kuwafikia watoto katika shule na vijiji 120, ikiwa ni sehemu ya mpango mpana wa taasisi hiyo wa kuwasaidia watoto milioni moja kujifunza kusoma na kuhesabu ndani ya kipindi cha miaka mitano kupitia afua zinazoongozwa na jamii.

264A2666.jpg.jpeg

Uzinduzi huo umewakutanisha viongozi na maafisa wa elimu kutoka ngazi ya Mkoa na Wilaya, wakiwemo Katibu Tawala wa Mkoa, Ofisa Elimu wa Mkoa, Ofisa Taaluma wa Mkoa, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wenyeviti wa Halmashauri, Maofisa Elimu wa Wilaya, Maofisa Taaluma wa Wilaya na Wadhibiti Ubora wa Shule.

Jumla ya washiriki wapatao 70, wakiwemo timu ya mradi kutoka Uwezo Tanzania na wanahabari, wamehudhuria tukio hilo.

Katika uzinduzi huo, washiriki wamepatiwa maelezo kuhusu uzoefu wa mpango wa ufadhili wa pamoja uliotekelezwa Ludewa, pamoja na mfumo wa utekelezaji wa awamu ya nne, ratiba na majukumu ya wadau mbalimbali.

Baada ya tamko rasmi la uzinduzi na picha ya pamoja, kikao kiligawanyika katika vikao viwili. Kikao cha uongozi kilijadili na kuridhia muundo wa uratibu pamoja na shule zitakazoshiriki katika halmashauri sita, huku kikao cha utekelezaji kikijikita katika mfumo wa Jifunze na mipango ya utekelezaji.

Uwezo Tanzania imesema uzinduzi huo una malengo manne makuu, ambayo ni kuimarisha uratibu wa kimkakati na umiliki wa mradi kati ya Serikali za Mkoa na Wilaya na Uwezo Tanzania; kuwasilisha mfumo wa utekelezaji, ratiba na majukumu ya wadau; kupitia na kuridhia muundo wa uratibu na shule zinazoshiriki; na kuandaa maazimio ya pamoja ya utekelezaji pamoja na mifumo ya uwajibikaji.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, upanuzi wa Mradi wa Kijiji Changu unalenga kuimarisha matokeo ya elimu ya msingi kwa kuweka jamii na taasisi za Serikali katika nafasi kubwa ya kushiriki katika kuboresha ujifunzaji wa watoto.

Uwezo Tanzania imeeleza kuwa mradi huo ni sehemu ya juhudi zake za kuhakikisha watoto wanapata fursa sawa ya elimu bora ya msingi, huku ikisisitiza umuhimu wa afua zinazoongozwa na jamii katika kuboresha ujifunzaji.

Mradi wa Kijiji Changu awamu ya IV unatarajiwa kuwa hatua nyingine katika kupanua matumizi ya mbinu zinazolenga kuongeza ujuzi wa msingi wa watoto na kuimarisha ushiriki wa Serikali na jamii katika kuboresha elimu ya msingi nchini.
 
Back
Top Bottom