Maumivu haya zaidi uhusisha moyo na yanapomtokea mtu huchukua muda mfupi na huisha, aina hii ya maumivu kwa lugha nyingine ya kitaalamu huitwa Kilio cha moyo ambapo misuli ya moyo inayowezesha moyo usukume damu inakosa hewa ya oksijeni hivyo inachoka na kufanya kazi kwa kujilazimisha ndiyo maana hali ikizidi kuwa mbaya utajikunja inakulazimu upumzike au ukae chini.
Chanzo cha tatizo
Maumivu haya ya kifua kama tulivyoona hutokana na misuli ya moyo kufanya kazi huku ikikosa hewa ya oksijeni. Kwenye misuli ya moyo kuna mishipa ya damu inayosambaza damu katika misuli hiyo.
Mishipa hiyo inayoitwa Coronary Artery. Mishipa hii ni midogo kwa hiyo huwa inaziba kutokana na mafuta mengi kuzunguka kwenye damu au ‘Cholesterol’ au kwa Kiswahili ‘lehemu.’ Mafuta haya huganda ndani ya mishipa ya damu hivyo hupunguza kipenyo cha mshipa wa damu au bomba la kupitisha damu na mwishowe kuziba kabisa. Mishipa hii ikiziba katika upande mmoja wa moyo husababisha upande huo kitofanya kazi vizuri.
Mahitaji ya mzunguko wa oksijeni katika misuli ya moyo huwa makubwa pale unapojishughulisha kwa mazoezi, aidha kukimbia, kutembea harakaharaka au kupanda ngazi au mlima, hapo utajisikia pumzi inapungua na kifua kinauma.
Maumivu ya kifua zaidi huwa upande wa kushoto na wakati mwingine yakielekea mgongoni upande huohuo.
Jinsi tatizo linavyotokea
Kama tulivyoelezea jinsi maumivu yanavyotokea, mgonjwa atagundua kwamba anatatizo hili la Angina endapo siku zote anaishi vizuri tu, hana presha ya kupanda wala kushuka lakini si mtu wa kufanya mazoezi lakini akijishughulisha kwa mazoezi au kupanda ngazi anapata shida hasa kupanda mlima.