CHUKUA msimamo wa Ligi Kuu England msimu huu, Arsenal ipo kwenye nafasi ya sita huko na pointi zake 57, pointi 33 nyuma ya vinara na mabingwa Manchester City. Ni aibu.
Pointi hizo za Arsenal zimeizidi West Brom inayoburuza mkia msimu huu kwa pointi 32. Kwa maana hiyo, Arsenal ipo karibu na timu inayoshuka daraja kuliko mabingwa wa msimu huu.
Pengine hilo ndilo lililowafanya mabosi wa Arsenal kufikiria kufanya mabadiliko ya benchi lao la ufundi kwa kumwaambia kocha wao, Arsene Wenger akampumzike tu. Wenger atakusanya mikoba yake na kuachana na Arsenal mwishoni mwa msimu huu baada ya kudumu kwenye kikosi hicho kwa karibu miaka 22, maana alitua kwenye timu hiyo Oktoba 1996.
Hata hivyo, aibu hiyo ni kwa msimu huu tu, lakini ukichukua rekodi za jumla ya mechi zote za Ligi Kuu England zilizochezwa tangu Wenger alipotua kwenye ligi hiyo, Man City hata kwenye Top Six haipo.