SIRI ZA MAISHA
JULAI 12, 2018.
SEHEMU YA PILI
SOMO: UNAVYOJIONA NDIVYO WATU WATAKAVYOKUONA!
"...TUKAJIONA NAFSI ZETU KUWA KAMA MAPANZI; NAO NDIVYO WALIVYOTUONA SISI"
(HESABU 13:33).
Nimejifunza kwenye maisha haya, kizuizi kikubwa cha mafanikio ya mtu ni mtu mwenyewe.
Kufanikiwa au kushindwa kwa mtu kunaamriwa na mtu mwenyewe hata kabla ya upinzani wa watu nje ya nafsi yake!
Chochote ambacho mtu ataona anakiweza, baada ya muda na kuendelea kukifanya bila kujali miluzi na makelele ya watu, baada ya muda watu wale wale wataanza kumsifu na kumpigia makofi.
Ni majuzi kwenye Kombe la dunia la Mpira wa miguu, mchezaji Christiano Ronaldo alifunga goli la tatu na la kuisawazishia timu yake ya taifa ya Ureno dhidi ya Hispania kwa MPIRA WA ADHABU (FREE KICK) ambao watu wengi walibaki kujadili kuhusu ubora wa goli lile na ubora wa mchezaji huyo kwa wiki kadhaa!
Lakini ni wachache wanajua kuwa ile ilikuwa FREE KICK YA 45 ANAIPIGA katika michezo kadhaa iliyopita na HAKUWA AMEFUNGA GOLI LOLOTE!
Unaweza kuelewa kuwa watu walishasema mengi kwenye MAPIGO 44 ALIYOJARIBU BILA GOLI LOLOTE. Najua kuna waliosema AMEZEEKA HANA UWEZO TENA. Naamini kuna walioshika vichwa wakisema KAMA NI HUYO ANAPIGA, REKODI YAKE NI MBAYA ATAKOSA TU!
Lakini, kijana huyu wa kireno alifaulu jambo moja ambalo wengi katika Kristo (kanisa) tunafeli. Yeye ALIAMINI ANAWEZA KUPIGA NA KUFUNGA. Yeye aliamini AMEJIFUNZA KUTOKANA NA MAPIGO 44 YALIYOPITA. Yeye aliamini ANA UWEZO WA KUPIGA NA KUFUNGA. Yeye aliamini na ALIJIONA MFUNGAJI KABLA WATAZAMAJI HAWAJAONA WAVU WA GOLI UKITIKISIKA!
NINACHOTAKA UJUE NI HIKI;
1) Watu watakuona utakavyojiona!
Ukijiona huwezi, ubora wako utapotea, uwezo wako utapungua, na mambo yataharibika nje, na kila mmoja ATAKUONA MSHINDWA!
Ukijiona unaweza, itazalisha akili ya kufanya, ubora na uwezo wa kuchukua hatua ambao hata kama watakucheka, kukupuuza, hautakata tamaa bali utaendelea kufanya na kufanya na kufanya tena kwa vile NAFSINI MWAKO NDIVYO ULIVYO, NA NDIVYO UJIONAVYO na hatimaye UTAANZA KUPATA MATOKEO na watu wale wale WATASEMA HAKIKA TULIJUA UTAFIKA JUU KWENYE KILELE CHA MAFANIKIO!
Kahaba anaitwa kahaba kwa vile anajiona na kujiweka kikahaba.
Mwalimu anaitwa mwalimu kwa vile anajiona na kujiweka kama mwalimu.
Ndivyo ilivyo kwa daktari, nesi na hata askari, wako hivyo ndani na wanajiweka hivyo na jamii inalazimika kuwaona na kuwaita hivyo.
2) Watu nje yetu si tatizo bali sisi wenyewe na mitazamo yetu ni tatizo!
Kwa mujibu wa andiko letu la msingi hapo juu, utagundua, "WATU WATATUONA VILE TULIVYOJIONA NAFSINI (NDANI) MWETU"
Hii ni kwa sababu zifuatazo;
-Chochote tutakachofanya nje watu wakakiona, kinaanza ndani ya nafsi zetu!
-Chochote kisichokua na nafasi kwenye nafsi zetu, hakiwezi kuwa nje kwenye maisha yetu!
-Watu wataona nje kile tu kilichoujaza moyo wako (Mathayo 12:35).
3) Ukitaka chochote nje (public) kizalishe kwanza nafsini mwako, halafu kitakuwa halisi machoni pa watu wote!
Huwezi kuwa tajiri wa mali, fedha nje (kwenye uhalisi) bila kuona cha kufanya kwanza ndani kitachogeuka fedha au mali au kitakachoingiza fedha na mali!
Huwezi kuheshimika nje, bila kujijengea heshima ndani yako kwanza!
Huwezi kupata chochote nje yako (kwenye mazingira) bila kukitengeneza ndani yako kwanza!
Nafasi yako ni kiwanda cha kuzaa yasiyoonekana nje lakini yanayoweza kuonekana, ukitaka chochote nje, kaa chini kizalishe nafsini mwako kwanza!
4) Jenga ubora wa nafsi yako ili upate heshima kwa dunia yako!
Nafsi yako inaweza kujengwa au kubomolewa.
Baadhi ya mambo yanayobomoa ubora wa nafsi yako;
i) Dhambi ya uzinzi (Mithali 6:32-34)
ii) Kutotambua na kuheshimu nafasi ya Mungu (Warumi 1:21-22,28).
iii) Ushirika na marafiki/ watu wasiofaa (1Wakorintho 15:33, Zaburi 1:1)
Baadhi ya mambo yanayoweza kuijenga nafsi yako;
i) Usomaji wa vitabu vya watu wenye matokeo (Danieli 9:2)
ii) Kusikiliza maneno na jumbe za watumishi wa Mungu wenye matokeo (2Timotheo 2:7)
Zaweza kuwa video zao, audio, semina, makongamano nakadhalika!
iii) Kuambatana na watu sahihi wenye matokeo (Mithali 13:20)
BIBLIA SI KITABU CHA HADITHI, NI KITABU CHA SIRI ZA MAISHA!
Mchungaji kiongozi,
Assembly Of Believers Church (ABC),
Mwalimu Dickson Cornel Kabigumila.