Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

KOCHA Unai Emery amesema alichotaka ni kushinda mechi yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu England na baada ya hilo kukamilika, amefurahi kwa sababu mambo matamu zaidi yanakuja.

Kocha huyo wa Arsenal ambaye alipigwa kwenye mechi mbili za kwanza dhidi ya vigogo Manchester City na Chelsea kwenye Ligi Kuu England, alihitaji kushinda mechi yake ya kwanza na mambo nusura yawe magumu baada ya kuanza kuruhusu bao kwenye mechi ya juzi Jumamosi dhidi ya West Ham United uwanjani Emirates.
 
Emery alisema amelazimika kufanya mabadiliko kadhaa ya kiufundi ndani ya mchezo huo kuhakikisha Arsenal inapata ushindi ambao utaamsha ari na nguvu ya kwenda kushindania ubingwa wa ligi hiyo kwa msimu huu.

Dakika ya 25 tu, tayari Arsenal ilikuwa nyuma kwa Bao Moja Bila, lililofungwa na straika Marko Arnautovic. Lakini, Nacho Monreal akaisawazishia Arsenal kabla ya mapumziko na kufanya mambo yanaonekane ushindi unawezekana.
 
Ile timu zinarejea kwenye kipindi cha pili, Emery alifanya mabadiliko huko huko nyumbani, akimwingiza Alexandre Lacazette kuchukua nafasi ya Alex Iwobi na Lucas Torreira aliingia kumbadili Matteo Guendouzi, mabadiliko ambayo ameyasema yalikuwa ya kiufundi zaidi baada ya kuwatazama wapinzani wake wanavyocheza.

Mabadiliko hayo yalileta matunda, kwani kipindi cha pili Arsenal ilikuwa tofauti na kufanikiwa kushinda 3-1. Shuti la Lacazette lilimbabatiza Issa Diop wa West Ham United na mpira kutinga wavuni kabla ya Danny Welbeck, aliyetokea benchi pia kunogesha na kuihakikishia ushindi Arsenal kwa kufunga bao la tatu.
 
Pointi hizi tatu ni muhimu sana. Kwenye mechi hii nimeona mambo mazuri sana, lakini nimeona pia mambo tunayotakiwa kuyafanyia kazi,” alisema Emery na kuongeza.

“Ni matokeo muhimu kwa mashabiki wetu. Baada ya kuwa nyuma 1-0, timu ilihitaji kubadilika uwanjani na kuongeza kiwango, ile sub yetu ilileta mabadiliko makubwa. Jambo hilo limenifanya nifurahi sana, hakika nimefurahi, lakini tunahitaji kuboresha pia kiwango chetu.

“Tulizungumza hilo vyumbani na tuliona tunahitaji kuwa na viungo wawili ndani kupata kitu kizuri. Ushindi huo unawapa wachezaji wangu hali ya kujiamini.”
 
Fundi wa mpira, Mesut Ozil hakucheza mechi hiyo na Kocha Emery alisema si kama ana ugomvi na mchezaji huyo, bali hakuwapo kwasababu ni mgonjwa.

Kwenye hatua nyingine, kocha huyo wa zamani wa Sevilla na Paris Saint-Germain amemtaka kiungo wake Aaron Ramsey afikirie kucheza mpira na mambo ya mkataba amwaachie wakala wake atamalizana nayo.

Arsenal sasa imekusanya pointi tatu katika mechi tatu ilizocheza kwenye Ligi Kuu England msimu huu, huku Liverpool ikiwa vinara kutokana na kushinda mechi zote tatu ilizocheza msimu huu na hivyo kuwa na mwanzo bora wa msimu kwa asilimia 100.
 
Bao la Mohamed Salah lilitosha kuwafanya wababe hao wa Anfield kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Brighton, ambao wikiendi iliyopita waliwaduwaza watu kwa kuwachama Manchester United mabao 3-2 kwenye mchezo wa ligi hiyo.

Ligi Kuu England itaendelea tena leo Jumatatu kwa mechi kali baina ya Man United ambao itakipiga na Tottenham uwanjani Old Trafford.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…