Mara ya kwanza, Pogba alikuwa na mpango wa kutua Juventus na amekuwa akisema anataka kucheza pamoja na Cristiano Ronaldo lakini sasa Zidane ndio amemchanganya akili.
Pogba aliyeitumikia klabu hiyo ya Old Trafford kwa mafanikio kwa misimu mitatu sasa akitokea Juventus, alikuwa katika bifu kali na kocha wa zamani, Jose Mourinho na alikuwa na mpango wa kutimkia Barcelona.
Hata baada ya Mourinho kuondoka, Pogba akakomalia msimamo wake akisema anataka kuondoka Old Trafford na safari hii si kwamba amekorofishana na kocha wa sasa, Ole Gunnar Solskjaer ila alisema anataka kupata changamoto nyingine.
Solskijaer ambaye ni kocha wa sasa wa muda wa Man United, amemweka Pogba kwenye mipango yake ya muda mrefu kiasi cha kuwa kati ya wachezaji wake muhimu katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Hata baada ya kuondoka kwa Mourinho, Pogba aliyekuwa akiwekwa benchi, ameonyesha soka akiwa katika ubora wake kiasi cha kuibeba Manchester United ikicheza mechi zaidi ya nane za Ligi Kuu bila kupoteza na kuipeleka katika nne bora za Ligi Kuu.
Wakala wake, Mino Raiola anatambua kuwa mkataba wa mchezaji wake unamalizika Juni 2021, amekuwa akihaha kumtafutia timu Pogba na tayari amepiga chini mkataba mpya ambao Man United wamepanga kumpatia.
Wakati Raiola akipiga hesabu za mchezaji wake kutua Juventus, klabu hiyo ni kama haitaki ushindani na Real Madrid, ilisema imemsikia Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane akimtaja Pogba kuwa ni kati ya wachezaji walio katika mipango yake.
Klabu hiyo ya Serie A ilisema kuwa endapo Real Madrid itashindwa kumsajili, itapenda kumrudisha kundini mchezaji huyo aliyewahi kuitumikia miaka mitatu iliyopita.
Gazeti la Diario AS la Italia lilisema pamoja na Real Madrid kuwa katika mawindo makali ya Pogba, lakini Juventus bado ina imani ya kumnasa mchezaji huyo kwa kuwa Raiola ana uhusiano mzuri na klabu hiyo ya Italia.
Hata hivyo, klabu hiyo ilitia chachandu mbio za kumnasa Pogba ikisema, endapo Raiola atafanikiwa kumrudisha Pogba Juventus, basi atavuna Euro 48 milioni kama kamisheni yake.