Kinachotakiwa kwa wanawake wote kuanzia miezi sita hadi mwaka mmoja kabla ya kupata mimba ni kuwa na madini hayo mwilini ili kupata faida zake ikiwa ni pamoja na kuzuia matatizo kama ya watoto kuwa na vichwa vikubwa na mgongo wazi… lakini kwa sababu mimba nyingi hazijulikani hubebwa lini, mama anaposhika ujauzito ndipo huanzishiwa dozi ya vidonge vya folic acid,” alisema.
Akifafanua zaidi kitaalam, Dk. Mwindah, alisema mwili wa binadamu una mafuta yenye vijisumu kama LDL na HDL na hayo, hupunguzwa kwa virutubisho vilivyomo katika korosho. Jambo hilo ndilo huwapunguzia walaji wa korosho uwezekano wa kupata maradhi ya moyo na mengineyo mengi.
Pia virutubisho vya korosho husaidia kutoziba kwa mishipa ya damu kwenye ubongo… mishipa hii ikiziba hufanya eneo la ubongo kukosa damu na hivyo kumsababishia mtu kupata ugonjwa wa pooza, kwa hiyo korosho zinasaidia kudhibiti ujio wa ugonjwa huo na magonjwa ya moyo,” alisema.
Alisema korosho pia zina madini ya potassium ambayo kazi yake mwilini ni kuimarisha ufanyaji kazi mishipa ya fahamu na kuimarisha ufanyaji kazi wa misuli.
ULAJI WAKE
Baadhi ya tafiti zinapendekeza kuwa ulaji mzuri wa korosho wenye faida zaidi mwilini ni ule usiohusisha kuzikaanga sana kwenye mafuta. Kwamba, zikiliwa zikiwa hazijakaangwa sana kwenye mafuta huwa na ubora zaidi mwilini kwa sababu virutubisho vyake hubaki katika ubora wake pasi na kuharibiwa na joto kali.