Manchester United huenda ikapigwa za mbavu kwenye mpango wake wa kumsajili beki wa kati, Kalidou Koulibaly baada ya staa huyo wa Senegal kununua jumba huko Paris, Ufaransa.
Lakini, baada ya kulipa Pauni 3.38 milioni kununua jumba huko Paris, ng'ambo tu ya Mto Seine akiutazama Mnara wa Eiffel, vyombo vya habari huko Ufaransa vinadai huenda hayo ni maandalizi ya kwenda kujiunga na PSG.
Jumba hilo la ghorofa hataweza kukaa hadi 2021 kutokana na sasa kuwa kwenye matengenezo na kwamba atatua PSG kwenda kuchukua mikoba ya nahodha, Thiago Silva kwenye safu ya ulinzi.
Beki Koulibaly alikuwapo uwanjani kwenye mchezo wa sare ya 1-1 dhidi ya Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa ni mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora uliopigwa Jumanne iliyopita.
Man United imekuwa ikimsaka Koulibaly kwa nguvu zote, lakini ikahamia kwa Harry Maguire, iliyemnasa kwa Pauni 85 milioni. Mkataba wa Koulibaly umedaiwa kuwa na kipengele kinachohitaji kulipiwa Pauni 127 milioni kuuvunja. PSG nayo inamtaka.
Mshambuliaji Mohamed Salah au Kylian Mbappe? Hicho ndicho wanachojiuliza mabosi wa Real Madrid wakati wakipanga kufanya usajili wa staa mkubwa katika dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Los Blancos bado hawafahamu wafanye nini kwenye mpango wao huo katika kunasa mchezaji mwenye uwezo mkubwa katika safu ya ushambuliaji, huku kwenye meza yao kukiwa na mastaa wawili, Mo Salah na Mbappe.
Kwenye mpango huo, Los Blancos wameripotiwa kuandaa mkwanja wa Pauni 127 milioni wakiamini kabisa utatosha kuinasa saini ya Mo Salah, lakini kama watahitaji huduma ya Mbappe, basi watalazimika kutoa pesa nyingi zaidi.
Hata hivyo, kwenye mpango huo hatima ya wachezaji wote hao wawili katika mpango wa kutua Bernabeu utatokana na bei atakayouzwa Gareth Bale, ambaye amekuwa akiteseka kupata nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza cha Kocha Zinedine Zidane.
Kwa mujibu wa El Desmarque, Bale akiondoka, basi Madrid itakuwa imepata pesa za kuongeza na kutimiza dhamira yake katika kuwanasa fowadi hao inaowataka.