Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

*HONGERA KWENU MIKIA*

[emoji2398] *Dr Beatus Chikoti*

1. Januari tuliuliza,
mmeipataje sare?
Ati mkatupuuza,
kuwa tunaona gere
Wenyewe mlipendeza,
hamkuipata bure
Hongera kwenu mikia,
siku yenu imefana.

2. Muro aliwaambia,
nanyi hamkusadiki
Tena akawatambia,
kuolewa kwenu haki
Kwamba tumewachumbia,
sare nne twahakiki
Hongera kwenu mikia,
siku yenu imefana.

3. Ikatolewa mahari,
Kila mtu akaona
Wala haikuwa siri,
hatukuwa na hiana
Arusi tukasubiri,
mwali akapakwa hina
Hongera kwenu mikia,
siku yenu imefana.

4. Machi tarehe ya nane,
arusi ikawadia
Uchumba miaka minne
kuwasomeni tabia
Sasa mambo tupeane,
Yanga tukajiambia
Hongera kwenu mikia,
siku yenu imefana.

5. Simba waliruka ruka,
Metacha kawadhibiti
Wavuni hawakuweka,
wakabaki hatihati
Mwisho wake wakachoka,
yakawajia mauti
Hongera kwenu mikia,
siku yenu imefana.

6. Nyoni kakwepa lawama,
nje akajiendea
Akatoka kwa heshima,
wakapagawa mikia
Lango tukaliandama,
Mkude akazingua
Hongera kwenu mikia,
siku yenu imefana.

7. Mzee wa kuupanda,
Morrisoni mtukuka
Mikia akawapanda,
kijasho kikawatoka
Bao tamu la kandanda,
Manyoni hadi Mkoka
Hongera kwenu mikia,
siku yenu imefana.

8. Marais wakiwepo,
Simba hupoteza sifa
Boli Zozo wa kichapo,
pale uwanja Taifa
Huondoka na makopo,
matundu pia maafa
Hongera kwenu mikia,
siku yenu imefana.

9. Yule mwanga wa hirizi,
pumzi ilimuisha
Kakimbilia mizizi,
nayo haikumtosha
Kafukuzwa kama mwizi,
benchi lamkaribisha
Hongera kwenu mikia,
siku yenu imefana.

10. Sasa watapoteana,
hawa mikia vilaza
Wameanza kugombana,
baada ya kuwaliza
Kombe litapiga kona,
nasi tutalituliza
Hongera kwenu mikia,
siku yenu imefana.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…