Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

MASHABIKI wa soka wa Tanzania wanaofuatilia Ligi Kuu ya England (EPL) wamekatwa stimu kwani ule mkeka waliokuwa wamepanga kuukweka kwenye gemu ya Man United dhidi ya Jose Mourinho na chama lake la Tottenham Hotspur, watakwama baada ya ligi hiyo kusimamishwa.
 
Hata wale mashabiki waliokuwa na hamu ya kujua hatma ya Nahodha wao wa taifa, Mbwana Samatta na chama lake la Aston Villa inayopambana kuepuka kushuka daraja, pia hawatamuona kwani Virusi vya Corona vimetibua huko na Bodi ya Ligi ya nchini humo kusimamisha EPL.
 
Aston Villa ya Samatta ilikuwa ikutane na Chelsea kesho katika uwanja wa Villa Park, lakini mchezo huo na mingine yote tayari imeshaghaahirishwa kama ambavyo ule wa Man United dhidi ya Spurs uliokuwa unasubiriwa kwa hamu na mashabiki hasa wale wanaobeti.
 
Kupitia taarifa ya Bodi ya Ligi England ni kwamba mechi zote za Ligi Kuu, Ligi Daraja la kwanza na La Pili sambamba na michuano ya vikombe imesimamishwa kutokana na tishio za maambukizi ya Virusi vya Corona ambavyo vimeripotiwa kuwanasa nyota kadhaa akiwamo Meneja wa Arsenal, Mikel Arteta.
 
Tangu kugundulika na kuanza kusambaa kwa ugonjwa huo umeonekana kuathiri maeneo mengi ya Ulaya na mabara mengine ambayo michezo mbalimbali imekuwa ikisimamishwa ama mechi kuahirishwa kwa sababu ya kuepuka maambukizi.
 
Tayari Ligi ya Kikapu ya Marekani (NBA) nayo imetangazwa kuchezwa bila mashabiki, huku hali mbaya ikielezwa ipo Italia na Ujerumani inaelezwa mabosi wa soka wapo kwenye vikao kwa nia ya kutaka kusimamisha Bundesliga na kuwatangaza Bayern Munich kuwa mabingwa.
 
Hata hivyo licha ya tishio hilo la Corona, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limeendelea kusisitiza kuwa, mechi zao zitaendelea kama zilivyopangwa kwa madai hakuna tishio kubwa la ugonjwa huo na hii ni baada ya Kenya kutishia kutopelekea timu zake za taifa nje ya nchi kuhofia Corona.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…